Jumanne tarehe Pili Mei, 2017,
Leo ni Jumanne tarehe 5 Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe Pili Mei, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1400 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Siku kama ya leo miaka 1125 iliyopita alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.
Siku kama ya leo miaka 497 iliyopita alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia Leonardo da Vinci. Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Baada ya kufanya safari katika miji kadhaa ya Italia, mwaka 1506 Da Vinci alielekea Ufaransa na kuwa mchoraji wa Mfalme Louis xii. Aliishi katika kipindi cha mchoraji mwingine mashuhuri wa Italia Michelangelo na wasanii hao wawili mashuhuri walitoa mchango mkubwa katika sanaa na kipindi cha mwamko wa Ulaya (Renaissance). Miongoni mwa michoro maarufu ya Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa" na kazi yake kubwa zaidi katika usanifu majengo ni jengo la Kanisa Kuu la Milan.
Miaka 60 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Seneta wa chama cha Republican huko Marekani Joseph McCarthy. Katika kipindi cha vita baridi McCarthy alikuwa kiongozi wa moja ya kamati za Baraza la Seneti la Marekani. Mwanasiasa huyo aliwasilisha orodha ya majina ya wafanyakazi 205 wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani akidai kwamba wanafanya ujasusi kwa maslahi ya Urusi ya zamani. Hatua hiyo ilikuwa mwanzo wa harakati iliyopewa jina la McCarthyism ambayo kwa mujibu wake wasomi, wasanii na maafisa wengi serikalini walifuatiliwa na kuswekwa jela kwa kutuhumiwa kwamba wanafanya ujasusi kwa maslahi ya Urusi na kwamba wana fikra za kikomunisti. Tume ya McCarthy ilifukuza maelfu ya wafanyakazi wa serikali na kuwasweka jela wasanii na waandishi wengi kwa tuhuma zisizo na msingi wowote. Miongoni mwa wasanii mashuhuri walioswekwa jela na tume hiyo ni Charlie Chaplin na Alfred Hitchcock.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, mwafaka na tarehe 12 Ordibehesht 1358 Hijria Shamsia, mwanachuoni na mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Murtadha Mutahhari, aliuawa shahidi baada ya kufyatuliwa risasi na wanachama wa genge la kigaidi la Furqan hapa nchini. Shahidi Mutahhari alijistawisha kielimu kutoka kwa maulamaa wakubwa wakiwemo Ayatullahil Udhma Burujerdi, Allamah Tabatabai na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Mutahhari alifundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran kwa muda wa miaka 23 na ameandika makumi ya vitabu katika taaluma mbalimbali za Kiislamu.
Katika siku kama ya leo miaka 6 iliyopita Usama bin Laden kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda aliuawa na vikosi vya Marekani huko nchini Pakistan. Usama aliyekuwa mmoja wa waasisi wa al-Qaeda alizaliwa Machi mwaka 1957 huko Riyadh nchini Saudi Arabia na kusoma katika Chuo Kikuu cha King Abdul-Aziz. Kundi la kigaidi la al-Qead linahusishwa na mauaji mengi duniani likiweko shambulio ya Septemba 11mwaka 2001 na mashambulio ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani Dar es Salaam Tanzania na Nairobi Kenya.