May 27, 2017 02:44 UTC
  • Jumamosi, Mei 27, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe Mosi Ramadhan 1438 Hijria sawa na tarehe 27 Mei mwaka 2017 Miladia.

Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qurani Tukufu. Ni mwezi wa rehema na baraka za kiroho. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi huu ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za kiroho za mwezi huu. Allah SW anasema: ((Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.))Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa Imam Hassan AS ni katika matukio muhimu katika mwezi huu. Aidha siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu kitakatifu cha Suhf cha Nabii Ibrahim AS. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za kimaanawi za mwezi huu na kwa fadhila za mwezi huu mtukufu tuwe karibu na rehema na msahamaha wake. ***

Katika siku kama ya leo miaka 1010 alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa Wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai."***

Abu Ali Sina

Siku kama ya leo miaka 706 iliyopita,  alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu. Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu ambapo maisha yake ya awali aliyatumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji nchini ambapo kutokana na njama za maadui zake, alifungwa jela. Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Tangu hapo ndipo ilianza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria. ***

Ibn Khaldun

Katika siku kama ya leo miaka 180 iliyopita, , ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdul-Qadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdul-Qadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa. Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru. ***

Amir Abdul Qadir

Na miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67 Robert Koch, mtaalamu wa vijuimbe maradhi na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB. Daktari Robert Koch alianza kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu, baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya tiba. Mwaka 1882 Miladia, Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudu maradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu. Ili kukamilisha uchunguzi wake tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kufanya utafiti wa magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa tuzo ya Nobel katika uwanja wa tiba. ***

Robert Koch