Jul 31, 2017 22:04 UTC
  • Jumanne tarehe Mosi Agosti, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 8 Dhulqaada 1438 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Agosti, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1090 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Zubair, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo. Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake huyo katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha. Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa pia cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvieneza.

Siku kama ya leo miaka 1059 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran. Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad. Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika fani ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 1053 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Dar-Qutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu. Dar-Qutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kuweza kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Aidha msomi huyo alikuwa hodari pia katika tafsiri ya Qur’an Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘as-Sunan’, ‘Sunan Daru Qutni’ na ‘al-Mukhtalif wal-Mu’talif.’

Miaka 42 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helisinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979.

Na miaka 12 iliyopita katika siku kama ya leo Fahd bin Abdulaziz, mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh. Mwaka 1967 Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1982 Fahd bin Abdulaziz alichukua madaraka na kuwa mfalme wa tano wa silsila ya kizazi cha Aal Saud baada ya kifo cha kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Uhusiano wa Riyadh na Washington ulikuwa wa karibu sana wakati wa utawala wa mfalme Fahd. Fahd pia aliusaidia kwa hali na mali utawala wa Saddam Hussein wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.

Fahd bin Abdulaziz