Jumanne, Agosti Nane, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 15 Dhulqaada1438 Hijria sawa na Agosti 8, 2017.
Siku kama ya leo miaka 2350 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean. Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri.

Siku kama ya leo miaka 938 iliyopita, alifariki dunia Ibn Fakhir, msomi na mtaalamu mkubwa wa lugha wa Kiislamu mjini Baghdad. Akiwa kijana Ibn Fakhir alifanya safari mjini Makkah na Yemen na kukutana na maulama wakubwa wa zama hizo ambapo alitokea kuwa alimu mkubwa wa lugha na hadithi. Msomi huyo alitumia njia ya kufikisha ujumbe kupitia mashairi yaliyokuwa na ufasaha wa hali ya juu. Miongoni mwa athari za Ibn Fakhir ni pamoja na kitabu kinachoitwa ‘Jawaabul-Masaail.’

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita muwafaka na tarehe 17 Mordad 1371 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Haj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96. Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza juu ya udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu. Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail' na 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani'.

Na miaka 19 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi wa habari mmoja. Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.
