Aug 17, 2017 12:19 UTC
  • Leo ni Agosti 17, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Dhulqaada 1438 Hijria sawa na Agosti 17, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1238 iliyopita, Imam Ali bin Mussa Ridha (AS) alianza safari kutoka katika mji mtakatifu wa Madina kuelekea Marv, eneo ambalo wakati huo lilikuwa kaskazini mwa Iran ya zamani. Safari hiyo ilifanyika kwa kulazimishwa na kutokana na mashinikizo ya mtawala Maamun, khalifa wa 7 wa utawala wa Kiabbasi, kwa lengo la kumdhibiti mjukuu huyo wa Mtume SAW. Huko Marv, Maamun alimtaka Imam Ridhaa akubali pendekezo la kuwa mrithi wa kiti chake cha ukhalifa. Kiongozi huyo alifanya hivyo ili ajionyeshe kwamba alikuwa mpenzi wa Watu wa Nyumba tukufu ya Bwana Mtume. Hata hivyo Imam alionyesha katika minasaba mbalimbali kwamba hangeshirikiana na utawala wa Bani Abbas na daima aliitambua serikali yao kuwa isiyo halali. Imam Ridha A.S daima alikuwa akifichua na kuweka wazi dhulma na uonevu wa watawala wa Kiabbasi. Baada ya kushindwa kumshawishi Imam Ridhaa, hatimaye Maamun aliamua kumuua shahidi kwa kumpa sumu hapo mwaka 203 Hijria.

Njia ya harakati ya Imam Ridha (as) kutoka Madina hadi Marv

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, wananchi wa Indonesia walianzisha mapambano ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mkoloni Mholanzi. Mapambano hayo yaliyoongozwa na Ahmad Sukarno yaliendelea kwa miaka minne huko Indonesia. Baada ya kushadidi mapambano hayo ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Indonesia, Umoja wa Mataifa uliiamuru serikali ya Uholanzi kuuasisi utawala kwa jina la "Umoja wa Indonesia na Uholanzi". Jamhuri ya Indonesia ilivunja umoja huo mwaka 1956 na kutangaza uhuru wa nchi hiyo na Sukarno akawa Rais wa kwanza wa taifa hilo.

Ahmad Sukarno

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Gabon iliyoko magharibi mwa Afrika na katika pwani ya bahari ya Atlantiki, ilipata uhuru wake. Wareno walifika huko Gabon kwa mara ya kwanza mwishoni mwa karne ya 15 Miladia. Hata hivyo nafasi ya kijiografia ya Gabon ilizuia kugunduliwa nchi hiyo hadi karne ya 19. Katikati ya karne ya 19 Wafaransa waliwasili Gabon na kuidhinishwa kuitawala nchi hiyo katika mkutano uliofanyika huko Berlin Ujerumani. Hatimaye mwaka 1960 Gabon ilipata uhuru. Kijiografia nchi ya Gabon inapakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, Cameroon na Equatorial Guinea.

Bendera ya Gabon

Miaka 30 iliyopita katika siku kama ya leo, Rudolf Hess makamu wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolf Hitler alijiua akiwa jela nchini Uingereza. Hess ambaye alizaliwa mwaka 1894, alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha Kinazi na miongoni mwa viongozi wakuu wa serikali ya Hitler. Rudolf Hess alihukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya jinai za kivita ya Nuremberg nchini Ujerumani baada ya nchi hiyo kushindwa katika Vita vya Pili vya Dunia. Hess alijiua akiwa jela mwaka 1987.

Rudolf Hess akiwa pamoja na Hitler

Tarehe 26 Murdad miaka 27 iliyopita kundi la kwanza mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa katika magereza za kutisha za Saddam Hussein liliwasili katika ardhi ya Iran. Kuachiwa huru mateka hao ilikuwa hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Iran na Iraq. Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa chini ya mashinikizo kutokana na kuivamia Kuwait alikubali kuwaachia huru mateka hao wa Iran na kurejea katika mipaka inayokubalika kimataifa ya nchi mbili baada ya kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria.

Mateka wa Kiirani baada ya kuwasili nchini

 

Tags