Ijumaa 18 Oktoba, 2017
Leo ni Ijumaa tarehe 25 Dhulqaada 1438 Hijria sawa na Agosti 18, 2017.
Siku kama ya leo miaka 1428 iliyopita Nabii Muhammad (saw) aliondoka Madina akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja na kuelekea Makka kwa ajili ya kutufu nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu al Kaaba. Tangu alipohamia Madina Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kutufu al Kaaba lakini alifanikiwa mara mbili tu kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija Mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada hiyo kwa njia sahihi. Baada ya kukamilisha ibada hiyo, Mtume Muhammad (saw) alirejea Madina na alipofika katika eneo la Ghadir Khum aliwakusanya masahaba zake na kwa amri ya Mola wake alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa khalifa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Widaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Mtukufu aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Siku kama ya leo miaka 1364 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasser Deen Shah Qajar na kufanikiwa kutoa athari zenye thamani kubwa za uchoraji.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.