Aug 21, 2017 22:14 UTC
  • Jumanne, Agosti 22, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 30 Dhilqaada 1438 Hijria sawa na Agosti 22, 2017.

Katika siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi (as) mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.

Miaka 390 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kukaliwa kwa mabavu La Rochelle. 

Vita vya La Rochelle

Katika siku kama ya leo miaka 319 iliyopita, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Sharel XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Sharel XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.  Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda. 

Mfalme kijana wa Sweden, Sharel XII

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada thabiti aliyokuwa nayo ilimuwezesha kuendelea na masomo yake ya fizikia hadi akafika Chuo Kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kilikuwa na uwezo wa kurusha mawimbi ya televisheni hadi umbali wa mita 30 tu na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.