Aug 24, 2017 00:42 UTC
  • Alkhamisi Agosti 24, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 2 Dhilhija 1438 Hijria sawa na Agosti 24 2017.

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas yalianza. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina.

Ukuta na Nudba, Baitul Muqaddas

Miaka 39 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha. 

Sayyid Andarzgu

Na siku kama leo miaka 26 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17 Miladia. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru wake.