Aug 26, 2017 03:52 UTC
  • Jumamosi, Agosti 26, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 4 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja 1438 Hijria mwafaka na tarehe 26 Agosti 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 671 iliyopita, mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia. Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa. Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa lmekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga. ***

Mfano wa silaha ya mzinga zamani

Miaka 274 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini Paris Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa. Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali. Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye. ***

Antoine Laurent Lavoisiere

Katika siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, askari wa utawala wa Othmania walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia. Waturuki wa Kiothmania walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Othmania. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmenia waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano. ***

Mauaji ya umati ya Waarmenia yaliyofanywa na askari wa utawala wa Othmania

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mahdi Iraqi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin. Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na aliendesha mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa shah na alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini kwa miaka kadhaa alifungwa jela na utawala wa Shah na kukumbana na mateso mengi.***

Mahdi Araqi akiwa na Imam Khomeini MA

Na siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Azimio nambari 620 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali

 

Tags