Aug 28, 2017 23:53 UTC
  • Jumanne 29 Agosti, 2017

Leo ni Jumanne tarehe 7 Dhilhija 1438 Hijria sawa 91 Agosti 2017.

Tarehe 7 Dhulhija miaka 1324 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir", yaani mchimbua elimu. Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhimain na Najaf nchini Iraq. Miongoni mwa athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko katika mji wa Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake na ina vitabu zaidi laki tatu.

Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi

Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, msanii na mchoraji maarufu wa katuni wa Palestina Naji al Ali ambaye alikuwa ameshambuliwa na maajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD huko London, Uingereza alifariki dunia baada ya siku 38 za kuwa katika hali ya kupoteza fahamu. Al-Ali alizaliwa mwaka 1937 huko Palestina na alilazimika kukimbia nchi yake akiwa bado mtoto akiwa pamoja na familia yake na kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Ain al-Halwa kusini mwa Lebanon kutokana na ukatili na unyama wa Wazayuni. Alishuhudia kwa karibu mashaka na masaibu ya Wapalestina na akaamua kutumia kipawa chake cha usanii kufichua unyama na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia sanaa ya uchoraji vibonzo. Hatimaye magaidi wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD walimshambulia na kumuua mwanamapambano huyo akiwa njiani kuelekea ofisini kwake mjini London. Miezi sita baada ya kufariki kwake dunia Jumuiya ya Kimataifa ya Wachapishaji ilimtunuku msanii huyo tuzo ya Kalamu ya Dhahabu ya Uhuru. 

Naji al Ali

Na siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Urusi ya zamani ilifanya majaribio ya siri ya bomu lake la kwanza la nyuklia. Kwa utaratibu huo Urusi ikawa nchi ya pili yenye mabomu ya nyuklia baada ya Marekani suala ambalo liliibua mlingano wa nguvu kati ya nchi hizo mbili ambao ulipewa jina la “Mlingano wa Hofu.” Kwani katika hali hiyo kila mmoja wao aliogopa kutumia silaha hizo za nyuklia dhidi ya mwenzake kwa kuogopa kushambuliwa pia na silaha kama hizo. Tangu wakati huo Marekani na Urusi ya zamani ziliingia katika vita vya kipropaganda. Vita hivyo vilipewa jina la "Vita Baridi" au Cold War kwa kimombo. Vita hivyo vya kati ya kambi ya Mashariki na Magharibi viliendelea hadi wakati wa kusambaratika Urusi ya zamani mwaka 1991.

Bomu la kwanza la nyuklia la Urusi ya zamani