Jumanne tarehe 5 Septemba, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 14 Dhulhija 1438 Hijria sawa na tarehe 5 Septemba, 2017.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Septemba 1993, moja kati ya misikiti mikubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo umejengwa na mtaalamu wa Ufaransa aliyetumia teknolojia ya kisasa na usanifu majengo wa Kiislamu. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba kubwa na chuo kikuu cha kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja kati ya misikiti mikubwa na maridadi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu uliotekelezwa na kundi la kigaidi la munafiqeen MKO. Shahidi Quddusi alipata elimu kwa wasomi kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihadi. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi shule ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani. Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake kwa juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.
Miaka 112 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 5 Septemba mwaka 1905, mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kuhitimisha vita kati ya Russia na Japan. Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya majeshi ya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kuyadhibiti maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia. Russia ilipata vipigo mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia.
Na miaka 130 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha kutokana na mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto huo.