Sura ya Al-Ahzab, aya ya 9-12 (Darsa ya 746)
Sura ya Al-Ahzab, aya ya 9-12 (Darsa ya 746)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 746 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 33 ya Ahzab. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya tisa ambayo inasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَاءَتْكُمْ جُنُودٌ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا وَجُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا ۚ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا
Enyi mlio amini! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu. Pale yalipo kufikilieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyo yaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.
Aya hii na nyengine 16 zinazofuatia zinazungumzia vita vya Ahzab, ambavyo vilitokea katika mwaka wa tano hijria. Katika vita hivyo, makundi na matapo yote yanayoupinga Uislamu yaliungana pamoja kwa nia ya kuumaliza Uislamu na Waislamu. Mayahudi wa Madina, washirikina wa Makka pamoja na makabila mbalimbali walikubaliana kuunda jeshi kubwa, ili baada ya kuishambulia na kuiteka Madina wamuue Bwana Mtume Muhammad SAW na Waislamu wengine wote. Lakini kwa irada ya Allah SW, njama yao hiyo ikashindwa, kwa Waislamu kupata ushindi na wao kudhoofishwa na kukata tamaa. Inafaa kuashiria kwamba katika vita vya Ahzab, baada ya Bwana Mtume SAW kupata habari ya njama za maadui za kuishambulia Madina, aliwakusanya Waislamu msikitini ili kushauriana na kubadilishana nao mawazo kuhusu namna ya kukabiliana na adui. Kwa ushauri uliotolewa na sahaba Salman al-Farsi, ikapangwa kuwa wachimbe mahandaki kuzunguka mji wa Madina ili maadui wasiweze kuingia mjini humo kwa urahisi. Kwa sababu hiyo, vita hivyo vilikuwa maarufu pia kwa jina la vita vya Khandak. Aya hii tuliyosoma ambayo ni ya kwanza inayozungumzia habari za vita vya Ahzab inawataka Waislamu wakumbuke kila mara auni na msaada wa Mwenyezi Mungu katika kukabiliana na maadui na wala wasilegee, kuwa dhaifu au kuhofu chochote. Wakumbuke kuwa katika vita vya Ahzab, japokuwa idadi ya maadui ilikuwa kubwa zaidi mara kadhaa kuliko wao, lakini Mwenyezi Mungu, kwanza aliwapelekea upepo mkali ambao uliwasambaratisha na kuzitia nyoyo zao hofu na mshtuko, na kwa upande mwengine akawateremsha malaika wa kuwapa moyo na kuwatia nguvu ili wasiingiwe na woga na hofu kwa sababu ya wingi wa maadui. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu na kufanya jitihada na juhudi kubwa ni sharti la kuweza kupata msaada wa Mola katika masuala mbalimbali ya maisha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kukumbuka mtu neema alizopewa na Mwenyezi Mungu huko nyuma ni wenzo wa kumpa subira na istiqama ya kuhimili na kuyakabili matatizo ya sasa na ya siku za usoni. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Allah SW yuko tayari muda wote kuwasaidia na kuwanusuru waumini. Hilo huweza kufanyika kupitia vitu vya kimaumbile kama upepo na kimbunga, na pia masuala ya nje ya ulimwengu wa kimaada kama kuteremka malaika. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kuwa kuamini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anayaona na anayajua mambo yetu yote, kunatufanya tudhibiti mwenendo na matendo yetu, na pia kutupa hima na motisha ya kufanya jitihada na juhudi zaidi katika njia ya Allah.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 10 na 11 ambazo zinasema:
إِذْ جَاءُوكُم مِّن فَوْقِكُمْ وَمِنْ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَإِذْ زَاغَتِ الْأَبْصَارُ وَبَلَغَتِ الْقُلُوبُ الْحَنَاجِرَ وَتَظُنُّونَ بِاللَّـهِ الظُّنُونَا
Walipo kujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipo kodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbali mbali.
هُنَالِكَ ابْتُلِيَ الْمُؤْمِنُونَ وَزُلْزِلُوا زِلْزَالًا شَدِيدًا
Hapo Waumini walijaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali.
Aya hizi zinaashiria hali ngumu na ya misukosuko ya vita vya Ahzab na kueleza kuwa, idadi ya wapiganaji wa jeshi la adui ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba waliuzingira kila upande mji wa Madina na kukawa na uwezekano wakati wowote kuingia ndani ya mji na kufanya mauaji na uporaji. Ilikuwa jambo la kutarajia kwa watu wa Madina kujawa na hofu kubwa, kiasi kwamba macho yao yalidhihirisha woga na hofu kubwa iliyokuwa imetanda katika nyoyo zao. Ilikuwa utadhani roho zinakaribia kuwatoka huku wakiyangojea mauti yawafike wakati wowote. Ukweli ni kwamba kwa watu ambao hawakuwa na imani juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu walikuwa wakihisi ahadi alizokuwa amewapa Bwana Mtume SAW za ushindi wa Uislamu dhidi ya ukafiri na haki mbele ya batili, hazikuwa za kweli na kwamba kwa kushindwa Waislamu, nuru ya Uislamu itazimika moja kwa moja. Hali hiyo ilikuwa mtihani mkubwa ulioletwa na Allah ili ipambanuke na kubainika ni nani wanaziamini kikwelikweli ahadi zake, wakawa tayari hata kuyakabili mauti, na nani ambao baada ya kuuona umati mkubwa wa jeshi la maadui watapatwa na hofu na kulegea na kuyumba kiimani. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Waislamu wanapaswa daima wawe wamejiandaa na kujiweka tayari kujilinda na njama za maadui na kuichunga mipaka yote ya ardhi zao isije ikavamiwa na kuathiriwa na satua na ushawishi wa maadui. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa vita na Jihadi ni moja ya mitihani migumu ya majaribu ya Mwenyezi Mungu, ambapo kama hakutokuwa na umakinifu, baadhi ya watu hutetereka na kuyumba kutokana na udhaifu wa imani. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wakati wa tabu na misukosuko ndipo wanapojipambanua waumini halisi na wale wa kimaonyesho, kwa sababu kuwa na istiqama na kusimama imara kuyakabili matatizo na misukosuko kunahitaji imani thabiti na ya kweli.
Darsa ya 746 ya Qur'ani inahitimishwa na aya ya 12 ambayo inasema:
وَإِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ مَّا وَعَدَنَا اللَّـهُ وَرَسُولُهُ إِلَّا غُرُورًا
Na walipo sema wanaafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao: Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu.
Katika aya iliyopita, Mwenyezi Mungu amewazungumzia watu miongoni mwa waumini ambao waliyumba na kutetereka kiimani katika vita vya Ahzab. Aya hii ya 12 inaashiria chimbuko la uyumbaji huo na kueleza kwamba, kundi miongoni mwa watu hao walikuwemo wanafiki, ambao walikuwa kidhahiri wakijifanya kuwa ni Waislamu wakati kiuhalisia hawakuwa na imani ya Uislamu. Kundi jengine ni la watu wenye imani dhaifu ambao mapenzi ya dunia na mambo ya kidunia yaliwafanya wakwepe kwenda kupigana jihadi na maadui. Hao, si wao wenyewe tu walioamua kurudi nyuma, lakini walikuwa wakiwashawishi na wenzao pia wafanye hivyo kwa kuwaambia, Mtume, ambaye ametupa sisi ahadi ya ushindi ametuhadaa tu ili tumsaidie kupambana na maadui. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba unafiki ni hatari inayotishia kila mara jamii za Kiislamu. Inapasa kuitambua hatari hiyo na kujiweka tayari kukabiliana nayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa wanafiki wanaiathiri jamii ya Kiislamu kutokea ndani kwa kuidhoofisha na kuikatisha tamaa kwa kuwavunja moyo waumini katika kukabiliana na adui. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba masahaba wote wa Bwana Mtume hawakuwa na hali sawa. Baadhi yao walikuwa na imani thabiti na baadhi yao walipatwa na unafiki na hali ya nyuso mbili. Wapenzi wasikilizaji, kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atusamehe madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.