Jumapili, 10 Septemba, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 19 Dhul-Hajj mwaka 1438 Hijiria, sawa na tarehe 10 Septemba 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita vilianza vita kati ya Ujerumani na Russia kando ya ziwa linaloitwa kwa jina la Mazori. Vita hivyo vilitokea kufuatia kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia na hatua ya Russia kujiunga na upande wa waitifaki wake. Katika vita vya Mazori, Ujerumani na chini ya uongozi wa Hindenburg, kamanda wa majeshi ya nchi hiyo na kwa kutumia mbinu na silaha mpya, iliweza kuibuka mshindi huku karibu askari elfu 20 wa Russia wakiuawa na watu elfu 45 kushikiliwa mateka. Baada ya kujiri mapinduzi ya mwezi Oktoba mwaka 1917 nchini Russia, hatimaye nchi hiyo iliamua kujiondoa katika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita kulitiwa saini Mkataba wa Saint Germain kati ya washindi wa Vita vya Kwanza vya Dunia na mfalme wa Austria. Kwa mujibu wa mkataba huo, ufalme wa Austria uligawanyika katika nchi tatu za Austria yenyewe, Hungary na Czechoslovakia, huku baadhi ya maeneo yake mengine yakiunganishwa na mataifa ya Italia, Yugoslavia, Urusi ya zamani, Poland na Romania. Katika upande mwingine ni kwamba kutiwa saini mkataba wa Saint Germain kulipelekea kubatilishwa umoja wa Austria na Ujerumani, ambao ulitiwa saini mwanzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia na bunge la Austria. Aidha nchi hizo zilizuia aina yoyote ya umoja wa kisiasa na kijeshi kati yao.
Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, kulitokea tetemeko kubwa la ardhi katika mji wa Orleansville, kusini magharibi mwa Algeria. Katika tukio hilo mji huo uliokuwa na watu elfu 30 ulifunikwa kikamilifu na udongo huku watu elfu 10 wakipoteza maisha. Mbali na hapo makumi ya maelfu ya raia wa Algeria walikosa makazi baada ya nyumba zao kuharibika na hivyo kuisababishia matatizo makubwa serikali ya Algiers.
Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita yaani tarehe 19 Shaharivar aliaga dunia Sayyid Mahmoud Talaqani kiongozi wa kidini, mwanaharakati wa Kiirani, mwanamapambano na mfasiri wa Qur'ani Tukufu. Ayatullah Talaqani alikuwa akifuatilia kwa karibu matukio ya kisiasa ya Iran tangu akiwa kijana mdogo. Kipindi fulani alitiwa nguvuni na kufungwa jela miaka miwili na utawala wa Kitaghuti wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu aliteuliwa na Imam Khomeini kuwa Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Imam wa Sala ya Ijumaa ya Tehran.