Jumatatu tarehe 11 Septemba 2017
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Dhulhija 1438 Hijria sawa na 11 Septemba 2017.
Miaka 16 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga ghorofa mbili pacha za Jengo la Biashara la Kimataifa mjini New York huku ndege nyingine ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ilitunguliwa na kuangushwa ikiwa katika anga ya Pensylvania. Baadhi ya ghorofa za Jengo la Biashara la Kimataifa ziliporomoka na shemu ya jengo la Pentagon pia likaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Jumla ya watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa kundi la al Qaida lililokuwa likiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia ndilo lililohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, aliuawa Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran wakati wa Swala ya Ijumaa. Shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na kikundi cha kigaidi cha Munafiqin (MKO). Ayatullah Madani alipata elimu kutoka kwa maulamaa kadhaa katika mji wa Qum na kisha akaelekea Najaf, Iraq ambako alipatia daraja ya juu ya Ijitihad. Msomi huyo alikamatwa na kuteswa mara kadhaa na askari wa utawala wa Shah nchini Iran kutokana na misimamo yake ya kuupinga utawala huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini alimteua Ayatullah Madani kuwa Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970.
Na miaka 69 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jannah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya wakubwa walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu.