Jumamosi, Septemba 16, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Tatu Dhulhaji 1438 Hijria ambayo inasadiafiana na tarehe 16 Septemba 2017 Miladia.
Miaka 281 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer. Msomi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 50. Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo wa Kijerumani alifanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, Mexico ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Mexico ni nchi yenye historia kongwe inayorejea karibu miaka elfu tano kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masiya AS. Wahispania waliwasili Mexico mwaka 1518 na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kutumia vibaya hitilafu za ndani na kutofahamu wananchi malengo waliyokuwanayo wavamizi hao. Mexico inapakana na Marekani na Guatemala na akthari ya wananchi wa nchi hiyo ni wakatoliki. Mji mkuu wa Mexico ni Mexico City na sarafu ya nchi hiyo ni Peso ya Mexico huku lugha ya nchi hiyo ikiwa ni Kihispania***
Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano dhidi ya wakoloni wa Italia. Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo Omar Mukhtar alilazimika kurejea nchini Libya. Mwaka 1911 Wataliano wakiwa na lengo la kuitawala Libya walianzisha vita na dola la Othmania. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano. Hata hivyo kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo.***
Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia. Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusoka akiwa huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba. Ufumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo. Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75. ***
Tarehe 16 Septemba 1939 yaani miaka 78 iliyopita, mji mkuu wa Poland Warsaw ulizingirwa na Wajerumani katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio ya Wanazi wa Ujerumani dhidi ya Poland yalianza siku 15 kabla. Licha ya kuwa Poland ilikabiliwa na mashambulio ya pande mbili ya Ujerumani na Umoja wa Kisovieti, lakini jeshi lake lilisimama kidete na kuuhami mji wa Warsaw. Hata hivyo baada ya siku 11 za kusimama kidete na kuuawa watu wengi waliokuwa wakiuhami mji wa Warsaw, mji huo ulidhibitiwa na kuangukia mikononi mwa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi. ***
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita utawala wa kidikteta wa Reza Khan nchini Iran uliangushwa na kukaanza kipindi cha utawala wa mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi. Baada ya mashambulio ya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti upande wa kaskazini na jeshi la Uingereza upande wa magharibi na kusini mwa Iran na kukaliwa kijeshi Iran wakati wa kujiri Vita vya Pili vya Dunia, Reza Khan alilazimika kujiuzulu katika siku kama ya leo baada ya kutawala kidikteta nchini Iran kwa muda wa miaka 15. Baada ya kubaidishwa Reza Khan, mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi aliingia madarakani kwa ushirikiano na Waingereza. Baada ya kubaidishwa kwa muda katika kisiwa cha Mauritius hatimaye alipelekwa Johannesburg Afrika Kusini. Aliishi huko hadi alipofariki dunia tarehe 26 Julai 1944. ***
Na miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 25 Sharivar 1357 Hijria Shamsia, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando ya mji huo. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.