Jumatano tarehe 11 Oktoba, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 20 Mfunguo Nne Muharram 1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 11 Oktoba, 2017.
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, vilianza vita vya umwagaji damu kati ya wazungu wa Kiholanzi kwa jina la Boers wakazi wa Afrika Kusini na Waingereza. Wanajeshi wa Uingereza waliwasili Afrika Kusini mwaka 1841 lengo likiwa ni kuikoloni Afrika. Waingereza walidhibiti Afrika Kusini baada ya kujenga maeneo ya kiraia nchini humo. Wahamiaji wengine kutoka Ulaya hususan Waingereza walimiminika huko Afrika Kusini baada ya kugunduliwa madini ya dhahabu na Almasi. Wazungu wa Uholanzi yaani Maboers waliwasili Afrika Kusini katika karne ya 19 na kupinga kuwasili wahamiaji wapya nchini humo. Sababu hiyo ilipelekea kuanza vita kati ya Wazungu hao na wahamiaji wa Kiingereza, lakini uungaji mkono wa serikali ya Uingereza kwa wahamiaji hao, ulitoa pigo kwa Maboers na kwa msingi huo Afrika Kusini ikaloloniwa na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita alifariki dunia Jean Henri Fabre msomi wa elimu ya sayansi na bingwa wa elimu ya wadudu au entomolojia. Fabre alizaliwa mwaka 1823 nchini Ufaransa. Msomi huyo ambaye pia alikuwa mwandishi amefanya utafiti mkubwa na kuandika vitabu kadhaa kwenye uwanja wa elimu ya wadudu.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu. Ayatullah Kamarei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika chuo cha kidini cha mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein (as) na mashahidi wengine wa Karbala.

Siku kama hii ya leo ya tarehe 11 Mehr miaka 27 iliyopita kwa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia iliasisiwa Jumuiya ya Kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu nchini Iran kwa amri ya Ayatullah Ali Khamenei. Jumuiya hiyo ilikuwepo katika zama za Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa akituma ujumbe mjini Cairo huko Misri na kukutana na maulamaa wakubwa wa madhehebu za Suni kwa ajili ya kufanya jitihada za kukurubisha pamoja Waislamu wa madhehebu tofauti. Safari na mazungumzo hayo yalikuwa na matunda mazuri kwa kadiri kwamba, katika kipindi cha uongozi wa Sheikh Mahmoud Shaltut katika Chuo Kikuu cha al Azhar, wanazuoni wa madhehebu ya Suni waliitambua rasmi madhehebu ya Shia.
Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu iliyoanzishwa na Ayatullah Khamenei inaendeleza malengo ya kujenga umoja na mshikamano baina ya Waislamu na kutayarisha uwanja mzuri wa kuwepo maelewano na kukurubiana zaidi katika nyanja za teolojia, fiqhi, na kadhalika.

Na katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita yaani sawa na tarehe 11 Oktoba mwaka 1991 Miladia, shughuli za Shirika la Ujasusi la Urusi ya zamani (KGB) zilifikia kikomo muda mfupi baada ya kusambaratika Muungano wa Sovieti. KGB iliundwa mwaka 1954 kwa lengo la kukabiliana na harakati zilizokuwa na lengo la kuuangusha mfumo wa Kikomonisti wa Urusi ya zamani. Shirika hilo aidha lilikuwa na majukumu kama vile kuwakandamiza wapinzani wa chama cha Kikomonisti na kuendesha operesheni za kijasusi na zile zilizo dhidi ya ujasusi ndani na nje ya Muungano wa Kisovieti.
