Jumanne, Novemba 7, 2017
Leo ni Jumanne tarehe 18 Mfunguo Tano Safar 1439 Hijria sawa na Novemba 7, 2017.
Tarehe 18 Safar miaka 1402 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Uways al Qarani, mmoja kati ya wafuasi waaminifu wa Mtume Mtukufu SAW na Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika vita vya Siffin. Uways Qarani aliishi katika eneo la Qaran lililoko Yemen na alikuwa mchamungu mkubwa. Licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa Mtume Mtukufu SAW, Uways Qarani hakubahatika kumuona mtukufu huyo, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Baada ya Mtume Mtukufu SAW kufariki dunia, Uways Qarani alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali (as). Shakhsia huyo akiwa pamoja na wapiganaji wengine katika jeshi la Imam Ali (as), alishiriki kikamilifu kwenye vita vya Siffin kati ya jeshi la Imam Ali na lile la Muawiya na akauawa shahidi katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 150 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland. Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne. Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.
Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa. Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la kanali hiyo. Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdul-Nassir, kuutaifisha mfereji huo.
Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi kote nchini Iran walifanya maandamano makubwa wakipinga kuingia madarakani serikali ya kijeshi ya Jenerali Golam Reza Azhari aliyekuwa kibaraka wa utawala fasidi wa Kipahlavi. Katika maandamano hayo wananchi Waislamu wa Iran walitangaza azimio wakisema kuwa mabadiliko ya kimaonyesho na kubadilisha nafasi za vibaraka wa Marekani hakuwezi kuzuia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Siku hiyo pia Kiongozi wa harakati za Mapinduzi hayati Imam Khomeini alitoa ujumbe kwa mnasaba wa mauaji yaliyofanywa na utawala wa Shah dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu tarehe 13 Aban mwaka huo huo akiwaambia wananchi kwamba: “Ninyi taifa shujaa, mumethibitisha kwamba vifaru, mitutu ya bunduki na mikuki imeota kutu na kwamba haiwezekani kukabiliana na irada ya chuma ya wananchi.”