Dec 21, 2017 02:45 UTC
  • Alkhamisi tarehe 21 Disemba, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe Pili Rabiuthani 1439 Hijria sawa na Disemba 21, 2017

 Leo tarehe 30 Azar mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya usiku mrefu zaidi wa mwaka ambao hapa nchini Iran unaitwa Usiku wa Yalda. Usiku huo wa Yalda au Usiku wa Chelleh ndio usiku mrefu zaidi wa mwaka katika nusu ya kaskazini mwa dunia. Usiku huo huwa baina ya kipindi cha kuzama jua tarehe 30 mwezi wa Azar ambayo ni siku ya mwisho ya kipindi cha mapukutiko (Fall) hadi kuchomoza jua katika siku ya kwanza ya mwezi Dei ambayo huwa siku ya kwanza ya kipindi cha baridi kali (Winter). Wairani na mataifa mengine mengi hufanya sherehe maalumu katika usiku huu wa Yalda. Usiku huo katika nusu ya kaskazini mwa dunia husadifiana na mabadiliko ya kimaumbile na tangu wakati huo mchana huanza kuwa mrefu zaidi kuliko usiku.

Siku kama hii ya leo miaka 29 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Disemba 1988, watu 270 walipoteza maisha yao baada ya ndege ya abiria ya Marekani kuripuka katika anga ya Lockerbie huko Scotland. Marekani na Uingereza ziliwatuhumu raia wawili wa Libya kuwa ndio waliotega bomu katika ndege hiyo. Kufuatia mashinikizo ya nchi mbili hizo, mwaka 1992, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiwekea vikwazo vya mafuta, anga na kijeshi nchi ya Libya, kwa tuhuma za kuwaficha wananchi hao wa Libya. Hata hivyo kufuatia makubaliano kati ya Washington na serikali ya Tripoli, mwaka 1999 watuhumiwa hao walikabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC yenye makao yake The Hague, Uholanzi ambapo baada ya kesi hiyo mmoja kati ya watuhumiwa hao aliachiliwa huru baada ya kutopatikana na hatia, na wa pili alihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mabaki ya ndege Marekani iliyolipuka katika anga ya Lockerbie

Katika siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) iliasisiwa. PLO iliundwa kutokana na makundi manane ya mapambano, taasisi za kielimu, kijamii, kitiba na kiutamaduni. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) la Fat-h lilianza harakati zake. Mwaka 1974, PLO ilikubaliwa kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa, na hadi mwaka 1982, harakati hiyo ilikuwa na uhusiano rasmi na nchi zaidi ya 100 duniani.

Tarehe 30 Azar miaka 32 iliyopita Urusi ya zamani na utawala wa chama cha Baath huko Iraq zilitia saini makubaliano ya kuipatia Iraq silaha za kisasa wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran. Kupanuliwa uhusiano wa Urusi ya zamani na Iraq katika kipindi hicho kuliitayarishia Moscow mazingira mazuri ya kufikia malengo ya siasa zake mpya katika Mashariki ya Kati na mkabala wa Iran. Misaada ya Urusi ya zamani kwa Iraq katika kipindi hicho ilikuwa mikubwa sana kilinganisha na misaada ya nchi nyingine na ilikadiriwa kuwa Urusi ilikuwa ikidhamini asilimia 60 ya silaha na zana za kijeshi za Iraq.

 

Tags