Sura ya As-Sabaa, aya ya 14-17 (Darsa ya 764)
Sura ya As-Sabaa, aya ya 14-17 (Darsa ya 764)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 764 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 34 ya Sabaa. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 14 ambayo inasema:
فَلَمَّا قَضَيْنَا عَلَيْهِ الْمَوْتَ مَا دَلَّهُمْ عَلَىٰ مَوْتِهِ إِلَّا دَابَّةُ الْأَرْضِ تَأْكُلُ مِنسَأَتَهُ ۖ فَلَمَّا خَرَّ تَبَيَّنَتِ الْجِنُّ أَن لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ الْغَيْبَ مَا لَبِثُوا فِي الْعَذَابِ الْمُهِينِ
Na tulipo mhukumia kufa, hapana aliye wajuulisha kufa kwake ila mnyama wa ardhi aliye kula fimbo yake. Na alipo anguka, majini walitambua lau kuwa wangeli jua ya ghaibu wasingeli kaa katika adhabu hiyo ya kufedhehesha.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria mifano kadhaa ya sanaa na ustadi wa ufundi uliokuwepo katika zama za Nabii Suleiman (as) na ustaarabu wa zama hizo. Aya hii tuliyosoma inasema: Pamoja na jaha, adhama na utukufu aliokuwa nao Nabii Suleiman, wakati Mwenyezi Mungu alipomhukumia kufikwa na mauti, malaika wa mauti alikabidhi roho yake huku Mtume huyo akiwa ameegemea fimbo yake. Nabii Suleiman alibaki katika hali hiyohiyo mpaka mchwa walipoila fimbo yake ndipo alipoanguka chini na watu wakaweza kujua kama Suleiman bin Daud (as) ameshaaga dunia. Majini waliokuwa wakifanya kazi katika utawala wa Nabii Suleiman, nao pia kama walivyokuwa wafanyakazi katika kundi la wanadamu, walikuwa hawana habari juu ya jambo hilo. Ni wakati mwili wake ulipoanguka chini ndipo na wao pia walielewa kwamba ameshafariki. Kiasi kwamba laiti kama wangekuwa na elimu ya ghaibu na kujua mapema zaidi kuhusu jambo hilo wangeacha kuendelea kufanya kazi ngumu na nzito na zenye tabu kubwa ambazo walikuwa wakizitekeleza kwa amri ya Mtume huyo. Imam Ali (as) ameeleza katika hotuba ya 182 ya Nahjul-Balaghah: "Kama kungekuwa na mtu wa kuweza kuyaepuka mauti na kuishi milele duniani, basi angekuwa Nabii Suleiman, ambaye aliwatiisha majini na watu, alikuwa na hadhi ya Utume na mbele ya Allah alikuwa na ukuruba na daraja kubwa." Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hata kama mtu atafikia daraja ya Utume na ufalme hawezi kuyaepuka mauti. Kwa hivyo tusije tukaingiwa na ghururi kwa sababu ya cheo na hadhi au mali na suhula tulizonazo, kwani iko siku tutapaswa kuyaacha yote hayo na kuondoka peke yetu katika dunia hii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa licha ya nguvu, mamlaka, hadhi na adhama aliyokuwa nayo Nabii Suleiman (as), aliangushwa chini na mchwa; na hadi wakati huo si yeyote katika wanajeshi na wafanyakazi wake aliyekuwa na habari ya kifo chake.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 15 ambayo inasema:
لَقَدْ كَانَ لِسَبَإٍ فِي مَسْكَنِهِمْ آيَةٌ ۖ جَنَّتَانِ عَن يَمِينٍ وَشِمَالٍ ۖ كُلُوا مِن رِّزْقِ رَبِّكُمْ وَاشْكُرُوا لَهُ ۚ بَلْدَةٌ طَيِّبَةٌ وَرَبٌّ غَفُورٌ
Hakika ilikuwapo Ishara kwa (watu wa nchi ya) Sabaa katika maskani yao - bustani mbili, kulia na kushoto. Kuleni katika riziki ya Mola wenu, na mumshukuru. Mji mzuri na Mola Mlezi Mwenye maghufira.
Katika darsa iliyopita tulieleza machache kuhusu maisha ya Mitume wawili wa Allah, yaani Nabii Daud na Nabii Suleiman (as), ambao licha ya kufikia kilele cha uwezo, hadhi na mamlaka walikuwa washukurivu wa neema za Mola wao na wakawa wanazitumia neema hizo kwa ajili ya kuwahudumia watu na kulinda amani na usalama wao. Lakini kuanzia aya hii na nyengine zinazofuatia, zinazungumziwa habari za kaumu ya Sabaa ambayo watu wake walimiminikiwa na neema chungu nzima za Mwenyezi Mungu lakini wakazikufuru na kuwafanya wafikwe na adhabu ili wao wawe ibra na mazingatio kwa wanadamu wote. Watu wa kaumu ya Sabaa walikuwa wakiishi katika eneo lenye hali ya hewa nzuri sana katika ardhi ya Yemen. Kwa kujenga mabwawa makubwa na imara, watu wa kaumu hiyo waliweza kuhifadhi na kujiwekea akiba kubwa ya maji. Kwa sababu hiyo waliweza kujiimarisha sana katika kilimo na ufugaji na kuwa jamii yenye ustawi. Mito mirefu na mipana iliyorutubisha na kuitosheleza ardhi ya watu hao kwa maji ilikuwa ikitiririka kutokea kwenye mabwawa, na kila upande wa mto kulikuwa na konde na bustani za aina kwa aina ambazo katika kipindi chote cha mwaka zilikuwa zikitoa matunda na mazao ya kila aina. Eneo hilo lenye rutuba lilikuwa na hewa safi na miti iliyojaa matunda ambayo ilikuwa alama ya fadhila na ihsani ya Mwenyezi Mungu kwa watu wa kaumu hiyo. Lakini mbali na neema hizo walipata pia maghufira na rehma za Allah; Yeye Mola mrehemevu aliwasamehe makosa na madhambi yao wala hakuwapunguzia chochote katika riziki zao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba hali ya kuvutia ya maumbile, mandhari zake za kupendeza, miti pamoja na anuai za matunda na mazao yake, yote hayo ni katika aya, alama na ishara za adhama ya Muumba wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuinaiwirisha na kuistawisha ardhi kwa njia ya ukulima na upandaji mimea na miti kunavutia watu kupata fadhila na rehma za Allah na wala hakuna mgongano wowote na msingi wa watu kufikiria na kushughulikia akhera yao.
Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 16 na 17 ambazo zinasema:
فَأَعْرَضُوا فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ سَيْلَ الْعَرِمِ وَبَدَّلْنَاهُم بِجَنَّتَيْهِمْ جَنَّتَيْنِ ذَوَاتَيْ أُكُلٍ خَمْطٍ وَأَثْلٍ وَشَيْءٍ مِّن سِدْرٍ قَلِيلٍ
Lakini wakaacha. Basi tukawapelekea mafuriko makubwa, na tukawabadilishia badala ya bustani zao hizo mbili kwa bustani nyengine mbili zenye matunda makali machungu, na mivinje, na miti michache ya kunazi.
ذَٰلِكَ جَزَيْنَاهُم بِمَا كَفَرُوا ۖ وَهَلْ نُجَازِي إِلَّا الْكَفُورَ
Hayo tuliwalipa kwa sababu ya walivyo kufuru. Nasi kwani tunamuadhibu isipo kuwa anaye kufuru?
Watu wamegawanyika makundi mawili kwa namna wanavyotenda kuhusiana na neema za Mwenyezi Mungu, ziwe za kimaada au za kimaanawi. Kundi moja ni la watu washukurivu na kundi jengine ni la watovu wa shukurani. Kuna watu ambao wanaponeemeshwa, humkumbuka Allah na kuzitumia neema walizojaaliwa katika njia inayomridhisha Yeye Mola. Lakini kuna watu pia ambao hughafilika na kumsahau Allah; na pale wanaponeemeshwa, huzitumia neema walizonazo kwa ajili ya kujistarehesha na kukidhi matashi na matamanio ya nafsi zao hata kama ni kwa kumghadhibisha Mola wao. Kujiweka mbali na dhikri na utajo wa Allah, baadhi ya wakati hufanyika kwa kupinga aya na alama za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu wa maumbile, na wakati mwengine hufanyika kwa kuzikadhibisha na kuzipa mgongo aya za hukumu za sharia na maamrisho yake Mola. Watu wa kaumu ya Sabaa, ijapokuwa walijaaliwa neema za kila aina lakini walimwasi Mola wao wakayafanya matashi na matakwa yao kigezo na kipimo cha kufanyia kila jambo. Waliweka mbele matashi yao badala ya maamrisho ya Mola wao na wakaisahau Siku ya Kiyama ya kuhesabiwa kwa amali zao. Hawakujua thamani ya neema walizopewa wakawa watovu wa shukurani kwa Allah. Matajiri walikuwa wakijifaharisha na kujivuna mbele ya wahitaji na wanyonge, wakaghafilika na kuwasaidia masikini. Kwa ujumla nyoyo za watu zilitekwa na maisha ya dunia, wakamsahau Mwenyezi Mungu na akhera. Walisahau kwamba yale yote waliyonayo wamepewa na Allah na wanapaswa wawe waja wake Yeye Mola. Kuzikufuru kwao neema za Allah kuliwafanya wafikwe na adhabu kubwa ya mafuriko ya kutisha yaliyozipindua juu chini na kuzisomba konde na mabustani yao. Kutokana na athari ya mafuriko, ule udongo wa ardhi yenye rutuba ulisombwa na kutoweka, na miti ikabaki bila matunda mpaka ikafika hadi ikawa hayaonekani tena matunda na mazao ya misimu minne ya mwaka na badala yake ikawa inaota miti isiyozaa kabisa au yenye matunda machungu na yenye ladha mbaya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kutoshukuru neema kwa maneno na kuzikufuru kwa vitendo kuna malipo ya adhabu ya hapa duniani; na hiyo ni sehemu ya mfumo wa malipo ya thawabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa hatima za watu na kaumu ziko mikononi mwao wenyewe; na hii ndio kaida na utaratibu alioweka Allah kuhusiana na watu waliotangulia, wa sasa na watakaofuatia hadi mwisho wa dunia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kushupalia na kudumu katika kufanya madhambi humuandalia mtu mazingira ya kushukiwa na adhabu; lakini kama mtu atafanya dhambi kwa kuteleza tu na akajuta na kutubia Mwenyezi Mungu atamghufiria na kumsamehe madhambi yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 764 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atusamehe madhambi yetu, atukubalie toba zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…/