Feb 12, 2018 07:22 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Feb 12

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya michezo yaliyojiri kitaifa na kimataifa, ndani ya siu saba zilizopita.....

Futsal: Iran yatwaa Kombe la Asia

Timu ya taifa ya Iran ya mpira wa miguu unaochezewa ukumbini maarufu kama futsal imetwaa ubingwa wa kombe hilo siku ya Jumapili kwa mataifa ya Asia baada ya kuigaragaza Japan kwa mabao 4 kwa mtungi. Mashindano hayo yaliyokuwa yakifanyika katika kisiwa cha Taiwan yamefunga pazia lake Jumapili ambapo katika mchezo wa fainali Iran iliitandika timu ya Japan mabao 4 kwa sifuri na kuendeleza ubabe wake katika mchezo wa Futsal barani Asia. Kwa ushindi huo, vijana wa Iran wamelipiza kisasi cha mwaka 2014 ambapo walitandikwa na Japan katika mchezo wa fainali kwa penalti na kupokonywa tonge mdomoni. Ubingwa huo wa Iran ni wa 12 katika kipindi cha duru 14 zilizopita za mashindano hayo. Mbali na Japan ambayo kwa kipigo ilichopata kutoka kwa Iran katika mchezo wa fainali imeshika nafasi ya pili, Uzibekstan iliyokuwa msambweni na Iraq, imeshika nafasi ya tatu baada ya kuibuka mshindi katika mtanange huo wa kutafuta mshindi wa tatu. Mshambuliaji hatari wa timu ya Futsal ya Iran Hussein Tayyibi amenyakua tuzo ya mfungaji bora baada ya kutikisa nyavu mara 14 katika mashindano hayo. Ali Asghar Hassanzadeh ametunukiwa tuzo ya mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi katika mashindano hayo.

Vijana wa Iran waliibamiza Myanmar magoli 14-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi C, kabla ya kuigaragaza China magoli 11-1 na kisha kuibakiza Uzbekistan 7-1 kwenye mechi ya nusu fainali.

Siasa za vikwazo kwenye Olimpiki ya Majira ya Baridi Korea Kusini

Kamati Andalizi ya Pyeongchang iliyoandaa Olimpiki ya Majira ya Baridi nchini Korea Kusini imeiomba radhi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya wanaridha wa taifa hili kunyimwa simu za rununu aina ya Samsung walizopewa wanariadha wote wanaoshiriki michezo hiyo. Kwenye barua kwa Reza Salehi Amiri, Mkuu wa Kamati Taifa ya Olimpiki ya Iran, Lee Hee-beom, Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Pyeongchang amesema suitofahamu iliyojitokeza na kupelekea wanariadha hao wa Kiirani kunyimwa siku hizo za rukono imetatuliwa. Mapema siku ya Jumatano, waandalizi wa mashindano hayo ya olimpiki nchini Korea Kusini walisema wanariadha kutoka Iran na Korea Kaskazini hawatopewa simu hizo erevu aina ya Galaxy Note 8, kutokana na vikwazo vya Umoja wa Mataifa zilivyowekewa nchi hizo.

Simu ya rununu ya Samsung

Baada ya tangazo hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilimuita Balozi wa Korea Kusini atoe maelezo kuhusiana na mkanganyiko huo. Kadhia hiyo hata hivyo imetatuliwa na tayari wanariadha wa Iran wamekabidhiwa simu hizo, ambazo zina ratiba na propgramu nyingine zinazohusu mashindano hayo. Tangazo hilo la kutopewa simu hizo wanariadha wa Iran liliibua ghadhabu hapa nchini kutoka kwa wananchi na maafisa wa serikali. Mohammad-Javad Azari Jahromi, Waziri wa Mawasiliano nusra apige marufuku uagizaji wa simu za Samsunga nchini, ambazo zina soko kubwa. Aidha siku ya Alkhamisi, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran alitishia kutoitumia simu yake ya Samsung iwapo waandalizi wa Olimpiki ya Korea Kusini hawatoomba radhi.

Klabu Bingwa Afrika

Klabu ya Simba ya Tanzania imeanza kwa kishindo michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa kuinyoa kwa chupa Gendermarie Nationale ya Djibout. Simba ambayo ilinguruma tangu mwanzoni mwa mchezo huo hadi mwisho, iliigeuza kichwa cha mwendawazimu timu hiyo ya Djibouti na kusagasaga mabao 4-0 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam Jumapili. Mabao ya Simba yalifungwa na Said Ndemla, Emanuel Okwi na mshambuliaji John Bocco aliyefunga mabao mawili katika mchezo huo.

Kwa matokeo hayo, Simba inahitaji sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano itakayochezwa wiki ijayo nchini Djibout ili kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo ya pili kwa ngazi ya klabu barani Afrika. Kwengineko, AFC Leopards ya Kenya imefungana bao 1-1 na Foisar Junior ya Madagascar, huku APR ya Rwanda ikiishinda Anse Reunion ya Ushelisheli kwa mabao 4-0. Mtanzania Simon Msuva anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco Jumamosi aliifungia timu yake mabao matatu ya hat-trick waliposhuka dimbani kwenye mechi yao yao ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika, dhidi ya Sport Bissau Benfica ya Guinea Bissau. Klabu hiyo ya Bissau ilichabangwa magoli 10-0 katika mchuano huo.

Komba la CAF

Magoli mengine ya Difaa El Jadid yalifungwa na Ahadad aliyefunga magoli matano, N’diaye na Bilal El Megri. Difaa El Jadida watakuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano kwani watakuwa wanahitaji sare tu au hata wakipoteza kwa idadi ya magoli 9-0 watakuwa wamefuzu. Huku hayo yakirifiwa, timu ya Yanga ya Tanzania imeanza michuano hiyo ya kikanda kwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya timu ya St.Louis ya Ushelisheli. Bao pekee la Yanga katika mchezo huo limefungwa na kiungo wake Juma Mahadhi baada ya kutokea purukushani iliyotokana na kona iliyopigwa na Geofrey Mwashiuya.

Kwenye michuano mingine, Cnaps ya Madagascar imeifunga Kampala City ya Uganda mabao 2-1. Gor Mahia imepata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Vegetarianos ya Guinea ya Istiwaa. Mabao ya Kogalo yalitiwa kimyani na wachezaji waliojiunga na klabu hiyo hivi karibuni, Kevin Omondi na Ephrem Guikan. Mkufunzi wa klabu hiyo Deylan Kerr amewapongeza vijana wake baada ya mtanange huo wa aina yake, uliopigwa katika uwanja wa Kenyatta kaunti ya Machakos nchini Kenya.

Wakati ambapo JKU ya Zanzibar ilikuwa inatoka suluhu na Zesco ya Zambia, Ngazi Sports ya visiwa vya Ngazija ilikuwa inalazimishwa sare ya 1-1 na Port KLouis ya Mauritius.

Nyota wa zamani wa Senegal kuwania urais?

Mchezaji kandanda nyota raia wa Senegal, El Hadji Diouf, mwenye umri wa miaka 36, sasa anasema atawania urais wa taifa hilo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2019. Diouf anasema kuwa amepewa motisha na ushindi wa George Weah huko Liberia. Diouf ambaye pia ana uraia wa Ufaransa, amesema kuwa kwa sasa yupo kwenye harakati za kupokea ushauri wa masuala ya uongozi, mikakati ya kiutawala na pia kutafuta umaarufu kabla ya kujitosa kwenye ulingoni wa kisiasa. Tafiti za hivi punde za maoni zinasema Diouf ni shakhsia wa 3 kwa umaarufu nchini Senegal. Mchezaji soka huyo alianza historia yake ugani kimataifa nchini Ufaransa mwaka wa 1998 akivalia jezi la timu ya Sochaux-Montbeliard. Alipanda hadhi na bei jinsi tajiriba yake ilivyoendelea kunoga na akajiunga na Sunderland, Blackburn, Bolton, Leeds United na pia Liverpool.  Mara ya mwisho kuonekana ugani ilikuwa 2015 akiwakilisha timu ya Sabah FA.