Ulimwengu wa Spoti, Machi 5
Hujambo mpenzi mwanaspoti wa na karibu tuangazie mawili matatu yaliyojiri kwenye uga wa michezo ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.....
Rais wa Iran ataka kutoingizwa siasa kwenye masuala ya michezo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelitaka Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuhakikisha kuwa siasa haziingizwi kwenye michezo na kwamba michezo itumiwe kuimarisha uhusiano wa mataifa ya dunia badala ya kujenga chuki na uhasama. Rais Rouhani aliyasema hayo hapa mjini Tehran katika mkutano wake na Rais wa FIFA, Gianni Infantino siku ya Alkhamisi. Dakta Rouhani amemshauri Infantino kwa kumuambia, "Chombo hiki ambacho ndicho kikuu zaidi cha kusimamia mpira wa miguu duniani, kinapaswa kuhakikisha kuwa mambo ambayo hayahusiana na michezo hayaingzwi kwenye michezo. Rais wa Iran amebainisha kuwa, "Serikali ya Iran imekuwa ikijitihidi kuhakikisha kuwa wanamichezo wa Iran wanashiriki katika mashindano mbali mbali ya dunia hususan kandanda na riadha. Hii leo, wanawake wa Iran wamekuwa wakishiriki kwa wingi na kwa hamasa kwenye michezo mbalimbali ya kitaifa, kieneo na kimataifa. Iran ina wanariadha 23 elfu wanawake." Kuhusu masuala ya usalama, Dakta Rouhani amesema nchi hii ni pahala salama na ipo tayari kuwa mwenyeji wa mashindano mbalimbali ya kieneo na kimataifa. Amesisitiza kuwa, mashirikisho ya michezo ya kieneo yanapaswa kuyaleta mataifa karibu na kuimarisha urafiki.
Itakumbukwa kuwa, Saudia imekuwa ikilitumia Shirikisho la Soka Asia kueneza uchochezi na propaganda dhidi ya Iran, kiasa cha kulifanya lipange mechi zote za Iran dhidi ya Saudia kupigwa nje ya Iran. Kwa upande wake, Rais wa FIFA, Gianni Infantino sambamba na kuwapongeza Wairani kwa kuvalia njuga michezo, lakini pia amesisitiza kuwa shirikisho hilo linapania kuimarisha uhusiano wa nchi mbali mbali duniani kupitia michezo na kwamba lipo tayari kuimarisha kiwango cha soka cha Iran. Aidha ameipongeza timu ya taifa ya soka ya Iran maarufu kama team melli, na kuongeza kuwa, "Wairani kama watu wa nchi nyingine, wana haki ya kushangilia timu zao katika viwanja vya hapa nchini, na shirikisho hili litahakikisha kuwa linapigania suala hilo."
Debi: Perspolis yazabwa moja la uchungu na Esteghlal
Siku ya Alkhamisi, timu mbili hasimu za soka hapa nchini zilishuka dimbani kuvaana katika debi la aina yake linalofahamika hapa nchini kama Sarkhobi, au debi la wekundu na buluu. Katika kitimutimu hicho cha aina yake kilichofuatiliwa na makumi ya maelfu ya mashabiki wa soka hapa nchini, vijana wa The Blues walifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Wekundu wa Tehran, katika mchuano uliofuatiliwa kwa karibu pia na Rais wa FIFA. Bao la kipekee na la ushindi la Esteqlal lilitiwa kimyani na kiungo aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo Vouria Ghaffouri kunako dakika ya 40, na kuwanyanyua mashabaki kutoka vitini huku uwanja ukihinikiza kwa shangwe, nderemo na vifijo.
Licha ya The Reds kuonyesha mchezo mzuri na kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha pili, lakini walishindwa kuona wavu wa Esteqlal. Kichapo hicho kimeitoa tonge mdomoni Persepolis, ambao wangelitoka sare, wangetwaa mapema ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka nchini (Ligi ya Wataalamu), kwa kuzingatia Zoba Ahab, ambao wapo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa sasa, waliambulia sare tasa walipovaana na Pars Junubi. Licha ya kuchabangwa, Persepolis wanasalia kileleni mwa ligi, wakiwa na alama 57, wakifuatia na Zob Ahan wenye alama 42. Esteqlal licha ya ushindi huo wanasalia katika nafasi ya tatu wakiwa ana alama 41.
Mieleka: Iran yaibuka ya pili
Kwengineko timu ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya kieneo ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Kyrgyzstan. Uzbekistan iliibuka kidedea katika mashindano hayo yanayofahamika kama Asian Wrestling Championships, kwa kuzoa alama 178, huku Iran ikitwaa nafasi ya pili kwa kuchota pointi 157. Siku ya mwisho ya mashindano hayo Jumapili, Muirani Hassan Yazdani Charati alimsagasaga Mmongolia na kumshinda kwa alama 10-0 katika mieleka mtindo wa Free Style.
Mshindi wa tatu wa mashindano hayo ya kikanda yaliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Kozhomkul katika mji mkuu wa Kyrgyzstan, Bishkek ilikuwa timu ya Kazakhstan iliyopata alama 146. Mashindano hayo yalianza Februari 27 na kufunga pazia lake Machi 4.
Dondoo za Soka: Mechi zijazo katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika
Mabingwa mara 27 wa Tunisia klabu ya Esperance watakabana koo na mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor Mahia katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Klabu Bingwa barani Afrika Jumatano ya Machi 7, katika Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos. Kogalo watalazimika kujitahidi kupata ushindi nyumbani kwa kuwa kibarua kigumu kjnawasubiri watakpoalikwa na Esperance jijini Tunis mnamo Machi 17. Nayo klabu ya Yanga ya Tanzania na Towship Rollers ya Botswana zitakutana siku ya Jumanne, Machi 6 katika mchezo wa raundi ya kwanza ya klabu bingwa barani Afrika ambao utafanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga itakuwa na kibarua kigumu, kwani vijana hao wa Botswana waliidhalilisha timu ngumu ya al-Merreikh ya Sudan kwa kuichabanga jumla ya mabao 4-2 katika mchezo wa hatua ya awali. Klabu ya Simba nayo itashuka dimbani Jumatano kuvaana na al-Masry ya Misri. Waarabu hawa wa Port-Said wanakuja kuchuana na Simba baada ya kuigaragaza Green Buffalo ya Zambia. Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara anasisitiza kuwa wamejiandaa kuwavaa Waarabu. Bingwa wa mashindano hayo ya kikanda ataondoka na dola milioni 1.25 za Marekani.
Kombe la Dunia Afrika Mashariki
Kombe halisi la dunia litakalokabidhiwa mshindi wa mashindano ya soka ya mwaka huu, yatakayofanyika nchini Russia kuanzia mwezi Juni linazuru maeneo mbalimbali duniani. Utamaduni huu ulianza mwaka 2006, wakati fainali ya wakati huo ilipoandaliwa nchini Ujerumani. Mwishoni mwa wiki iliyopita, wakaazi wa jiji la Khartoum nchini Sudan walipata nafasi ya kulitazama kombe hilo na kupiga nalo picha kwa mara ya kwanza.
Baada ya kuwa nchini Ethiopia, siku ya Jumatatu na Jumanne, kombe hilo lilisafirishwa jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo wapenzi wa soka walipata nafasi ya kupiga picha nalo huku Rais Uhuru Kenyatta akilinyanyua. Kombe hili linazuru mataifa 10 pekee ya bara Afrika, ikiwa ni pamoja na Uganda, Ivory Coast, Misri, Msumbiji, Nigeria, Senegal na Afrika Kusini.
Wenger azidi kushinikizwa ajiuzulu, lakini mwenyewe kishipa
Baada ya klabu ya Arsenal kupokea vipigo vitatu mfululizo chini ya wiki mbili, mkufunzi wa klabu hiyo ya Uingereza, Arsene Wenger anazidi kukabiliwa na mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu. Kipigo cha magoli 3 bila jibu kutoka kwa Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa nyumbani katika uwanja wa Emirates na kichapo kama hichi cha wiki iliyopita kutoka kwa vijana hawa hawa wa City katika fainali ya Kombe la Carabao, na kutia msumari moto kwenye kidonda, kichapo cha mabao 2-1 kutoka klabu ya Brighton ni miongoni mwa matokeo ya hivi karibuni ambayo yameshadidisha ghadhabu za mashabiki wa klabu hiyo. Msururu wa vichapo hivyo na kutotwaa ubingwa wowote katika miaka ya hivi karibuni kumewapelekea mashabiki wa klabu hiyo mjini London na meneo mengine ya Uingereza wafanya maandamano ya kumtaka Wenger aachie ngazi.
Mwenyekiti wa zamani wa Arsenal, Peter Hill-Wood amemtaka Wenger ajiuzulu, akisisitiza kuwa hilo tu ndilo linalomfaa kwa sasa. Hill-Wood aliyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Daily Star. Rais wa zamani wa klabu ya Barcelona ya Uhispania Joan Laporta anaamini kuwa, Arsenal wanaweza kuiga mfano wa Barca kwa kumteua staa wao wa zamani Thierry Henry kuwa kocha wao kama ambavyo Barcelona waliwahi kufanya hivyo kwa Pep Guardiola na walifanikiwa kupata mataji mbalimbali. Sio mashabiki wa Gunners wa bara Ulaya na nchi nyingine za Magharibi tu wanaomtaka Wenger ajiuzulu, bali pia wakereketwa wa timu hiyo barani Afrika wanahisi kuchoshwa naye, ila kuna baadhi wanamuunga mkono.
Licha ya mashinikizo hayo, Wenger ambaye amewanoa Wabeba Bunduki kwa zaidi ya miongo miwili, anasisitiza kuwa anahitaji muda kurekebisha mapungufu yaliyoko. Anasema anaufahamu kuhusu uchungu na vilio vya mashabiki, lakini wanachotakiwa kufanya ni kuendelea kumshajiisha na kumtia moyo, badala ya kumponda kila uchao.
…………………….TAMATI………………..