Mar 06, 2018 06:14 UTC
  • Maulamaa katika kongamano la Umoja wa Kiislamu
    Maulamaa katika kongamano la Umoja wa Kiislamu

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipita hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 13.

Katika kipindi kilichopita ambapo tulimalizia kumzungumzia Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi tulieleza kuwa baada ya mwanamageuzi na mrekebishaji huyo wa umma kubaini sababu za kudhoofika nchi za Kiislamu na vizuizi vinavyokwamisha kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu alifikia hitimisho kwamba kurejea kwenye Uislamu halisi wa asili, kuondoa khurafa na mambo ya uzushi kwenye imani na itikadi za dini, kuachana na mienendo michafu ya kiakhlaqi na badala yake kujipamba kwa maadili na akhlaqi njema za kidini na kiutu, kuweka kando hitilafu za kikaumu, kikabila, kimadhehebu na za kiutaifa, kufanya juhudi maalumu za kupambana na watawala madikteta wa ndani, kujishughulisha wananchi na upitishaji maamuzi ya kisiasa, kujitutumua Waislamu kielimu ili kuweza kufikia ustawi na maendeleo na kujengeka utambulisho wa Kiislamu wa kukabiliana na Ukoloni wa Magharibi ndio siri ya kuwezesha nchi za Kiislamu kuwa na nguvu na kupiga hatua mbele na kuzifanya ziwe na umoja wa kukabiliana na Ukoloni wa Magharibi.

Kama nilivyokuahidini wapenzi wasikilizaji katika sehemu iliyopita ya 12 ya kipindi hiki, leo tutaanza kutupia jicho fikra na mitazamo ya mrekebishaji mwengine wa umma katika Ulimwengu wa Kiislamu. Na huyo si mwengine ila ni Iqbal-e Lahori.

Muhammad Iqbal-e Lahori, alizaliwa tarehe 9 Novemba mwaka 1877 katika mji wa Sialkot ulioko kwenye jimbo la Punjab la Pakistan ya leo. Alipata elimu yake ya msingi katika mji huo alikozaliwa kisha akaelekea mjini Lahore kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya shahada ya Uzamili alichaguliwa kuwa mhadhiri wa Falsafa na Siasa katika Chuo cha Mashariki cha mji wa Lahore. Mnamo mwaka 1905, Iqbal-e Lahori alielekea London, Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Hotuba alizokuwa akitoa kuhusiana na maudhui za Kiislamu zilimpa umashuhuri barani Ulaya. Mwaka 1908, alirejea nchini kwao na kuongoza kitivo cha Falsafa cha Chuo Kikuu cha Lahore.

Vita vya mwaka 1910 vilivyotokea katika maeneo ya Balkan na Tripoli vilimwathiri na kumuungulisha mno Iqbal na kuifanya nafsi yake iwe na chuki na uadui mkubwa na Magharibi na Ulaya. Kuanza Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia katika mwaka 1914, kusambaratika dola la Othmaniyyah, kugawanywa vipande vipande Ulimwengu wa Kiislamu, kudhibitiwa maeneo mbali mbali ya Ulimwengu wa Kiislamu na madola ya Ulaya na dhulma na jinai zisizohesabika walizofanyiwa Waislamu wa maeneo hayo vilileta mabadiliko makubwa katika nafsi na fikra za Iqbal-e Lahori na kujenga msingi wa mitazamo na mielekeo yake kuhusiana na Magharibi. Mwaka 1930, mwanafikra na mrekebishaji huyo wa umma wa Ulimwengu wa Kiislamu aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa mkutano wa kila mwaka wa Chama cha Muslim League, na kwa mara ya kwanza akapendekeza wazo na mpango wa kuundwa nchi ya Pakistan na kuanza kulifuatilia suala hilo kwa uzito mkubwa. Japokuwa ndoto ya kuwa huru Pakistan haikuthibiti wakati wa uhai wa Iqbal-e Lahori, lakini hatimaye taifa huru la Pakistan liliundwa, na yeye akawa maarufu kwa lakabu ya msanifu wa Pakistan.

Mrekebishaji huyo wa umma alikuwa akiyaelewa kwa karibu matatizo ya maeneo tofauti ya Ulimwengu wa Kiislamu na akajaribu kuioanisha elimu, ujuzi na falsafa yake na matukio yaliyokuwa yakijiri katika Ulimwengu wa Kiislamu na kutafuta njia za ufumbuzi wa matatizo ya kisiasa na kijamii yaliyokuwa yakiutaabisha. Iqbal hakutosheka na ufundishaji na utafiti tu katika falsafa lakini aliipa elimu na ujuzi wake muelekeo wa kiidiolojia, akaiunganisha na matukio ya kisiasa na kijamii ya Ulimwengu wa Kiislamu na kuitumia kwa ajili ya kuwaamsha Waislamu na kuuokoa Ulimwengu wa Kiislamu.

Iqbal-e Lahori, kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi, naye pia ni mmoja wa wana nadharia wa dhana ya Umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu japokuwa tafsiri na mtazamo wa Iqbal kuhusu umoja baina ya nchi za Kiislamu hauko sawa na ule ya Sayyid Jamaluddin. Iqbal-e Lahori alikuwa akiamini kuwa hakuna hitilafu za msingi na tofauti kubwa baina ya Waislamu, bali wote wanakubaliana pamoja katika usuli na misingi ya dini yao. Kwa mtazamo wa mrekebishaji huyo wa umma, mhimili mkuu wa umoja baina ya Waislamu ni Tauhidi, Qur’ani na Sunna; kwa sababu Tauhidi inajenga umoja usiotetereka na kuwaunganisha Waislamu katika fikra na matendo. Iqbal-e Lahori anaanzia umoja wake katika mfumo wa uumbaji na kufikia kwenye umoja wa Waislamu; na fikra ya umoja ameijenga kutokana na msingi wa Qur’ani na Sunna za Bwana Mtume Muhammad SAW. Katika fikra ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, bila kujali hisia na taasubi na ubaguzi wa rangi na asili wa kuwatenga na kuwadunisha wasio Waislamu kwa msingi wa utaifa wa Kiislamu, Iqbal-e Lahori aliyaangalia kwa pamoja mataifa manne ya Wairani, Waafghani, Waturuki na Waarabu, kisha akazihakiki nukta zao chanya na hasi kwa ajili ya kuleta umoja wa Uimwengu wa Kiislamu. Kwa mtazamo wa mwanafalsafa huyo ambaye alikuwa malenga na mshairi pia aliyebobea, Waislamu wote ni taifa moja; na umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu haukomei na kuishia kwenye nchi na taifa maalumu.

Kongamano la Umoja wa Kiislamu Tehran, Iran

 

Kwa mtazamo wa Iqbal, mielekeo ya utaifa huwa chanzo cha taasubi pale inapotaka kuipa elimu au dini utambulisho maalumu kwa msingi wa kijiografia na kuukana utambulisho wake wa kiutu na kibinadamu. Mwanamageuzi huyo alikuwa akiitakidi kuwa taifa lenye ghururi na majivuno huiona elimu na sayansi milki yake na kuyazuilia mataifa mengine; na taifa lenye taasubi huona elimu na sayansi ni kitu kitokacho kwa maajinabi, makafiri, ulimwengu wa Mashariki au Magharibi na hivyo kujitenga na kujiweka mbali nayo. Huku akiwa na imani kwamba iko siku umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu utathibiti kwa sura ya hakika ya kisiasa na kijiografia, Iqbal-e Lahori alikuwa akizitaka nchi za Kiislamu lizipe uzito maalumu suala la umoja; na kwa mtazamo wake kulikuwa na sababu mbili zilizokuwa zikidhoofisha dhana ya kufikiwa umoja huo. Ya kwanza ni nchi ya Waislamu kupuuza misingi ya dini yake na kukumbatia baadhi ya kanuni za kisiasa na kiuchumi; na ya pili ni nchi moja ya Waislamu kuishambulia kijeshi nchi nyengine ya Waislamu. Kwa sababu hiyo alikuwa akiitakidi kuwa zinapotokea hitilafu tu baina ya nchi za Kiislamu, inapasa zifanyike juhudi za haraka kutatua hitilafu hizo. Kwa ushauri wa Iqbal, badala ya nchi za Kiislamu kukumbatia zaidi masuala kama rangi, asili za watu na utaifa ziungane na kuwa na umoja kwa kufuata miongozo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu iliyosimama juu ya msingi wa imani na umoja.

Kwa kuzingatia mazingira ya kieneo na kimataifa ya zama zake, Iqbal alipendekeza njia tatu za kuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu na kutilia mkazo zaidi moja kati ya njia hizo. Njia ya kwanza ni nchi za Kiislamu kuendeshwa chini ya usimamizi wa kiongozi mmoja, jambo ambalo uwezekano wake ni mdogo. Njia ya pili aliyopendekeza ilikuwa Ulimwengu wa Kiislamu kuwa na muundo wa shirikisho, ambapo kutokana na kutokuwepo uratibu na hali inayofanana kati ya nchi za Kiislamu, wazo hilo pia lisingewezekana kuthibiti kivitendo. Na njia ya tatu ambayo mrekebishaji huyo wa umma aliipendekeza na akaitilia mkazo zaidi kwa ajli ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu ilikuwa ni nchi za Kiislamu kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu kupitia mikataba na mafungamano ya kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kijeshi baina yao.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 13 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 14 ya mfululizo huu. Nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani…/

  

 

Tags