Mar 06, 2018 06:22 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (14)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipita hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 14.

Katika kipindi kilichopita tulianza kumzungumzia mwanafikra na mrekebishaji umma mwengine katika Ulimwengu wa Kiislamu ambaye ni Muhammad Iqbal, maarufu kama Iqbal-e Lahori. Tulisema kuwa kuanza Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia katika mwaka 1914, kusambaratika dola la Othmaniyyah, kugawanywa vipande vipande Ulimwengu wa Kiislamu, kudhibitiwa maeneo mbali mbali ya Ulimwengu wa Kiislamu na madola ya Ulaya na dhulma na jinai zisizohesabika walizofanyiwa Waislamu wa maeneo hayo vilileta mabadiliko makubwa katika nafsi na fikra za Iqbal-e Lahori na kujenga msingi wa mitazamo na mielekeo yake kuhusiana na Magharibi. Tukabainisha pia kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kieneo na kimataifa ya zama zake, Iqbal alipendekeza njia tatu za kuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu na kutilia mkazo zaidi moja kati ya njia hizo. Njia ya kwanza ni nchi za Kiislamu kuendeshwa chini ya usimamizi wa kiongozi mmoja, jambo ambalo uwezekano wake ni mdogo. Njia ya pili aliyopendekeza ilikuwa Ulimwengu wa Kiislamu kuwa na muundo wa shirikisho, ambapo kutokana na kutokuwepo uratibu na hali inayofanana kati ya nchi za Kiislamu, wazo hilo pia lisingewezekana kuthibiti kivitendo. Na njia ya tatu ambayo mrekebishaji huyo wa umma aliipendekeza na akaitilia mkazo zaidi kwa ajli ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu ilikuwa ni nchi za Kiislamu kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu kupitia mikataba na mafungamano ya kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kijeshi baina yao.

Iqbal alikuwa akiitakidi kuwa ili kutatua matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu, nchi za Kiislamu zinapaswa kuungana kulingana na mafundisho ya Bwana Mtume SAW na hapo ndipo zitaweza kunusurika na balaa la kusambaratishwa. Sisitizo la mrekebishaji huyo wa umma juu ya njia hiyo ya tatu linadhihirisha nukta moja muhimu, nayo ni kwamba mtazamo wake juu ya umoja ni wa kioganiki yaani unaozingatia hali halisi.

Baraza la Umoja wa Kiislamu

 

 Iqbal-e Lahori alikubali kuwa kufutwa ukhalifa wa dola la Othmaniyyah lilikuwa jambo lisiloepukika. Iqbal alikuwa akiamini kuwa ukhalifa ulikuwa na ufanisi na faida wakati dola kuu la Kiislamu lilipokuwa na umoja na mshikamano. Lakini wakati ilipofika hadi Iran na Uturuki zikawa kila moja na lake kutokana na kuhitilafiana kimtazamo juu ya suala la Khilafa; Morocco ikawa inazitazama pande mbili zote hizo kwa jicho baya huku Saudi Arabia nayo ikiwa inawaza haya na yale kwenye ulimwengu wake wa njozi na faragha, Ukhalifa hauwezi kuwa taasisi inayofaa na yenye faida; na kwa sababu hiyo Ukhalifa hauwezi kuwa mwakilishi wa Waislamu wote duniani. Iqbal-e Lahori alikuwa akiitakidi kwamba kwa kuzikaribisha kwa mikono miwili na kwa moyo mkunjufu harakati za kupigania uhuru na kwa kuweza kujitawala na kufikia ustawi, jamii za Kiislamu zinapaswa kuwa na ustahiki wa kuwa sehemu ya familia kubwa ya Kiislamu. Na ni baada ya kufikia hatua hiyo ndipo zitaweza kufikia kwenye umoja unaokusudiwa ambao ni mpana na unaovuka mipaka bandia ya kubuniwa pamoja na kuwapambanua watu kwa rangi na asili zao. Mwanamageuzi na mrekebishaji huyo wa umma alikuwa akibainisha waziwazi kuwa kwa mtazamo wake, kuunda dola kubwa la ulimwengu mzima lililo chini ya uongozi wa nchi moja na kuwa na vuguvugu la kisiasa la Kiislamu (Ummul-Quraa) ni nadharia ya kujipanulia mipaka ya nchi, ya kujipa nguvu na mamlaka ya juu zaidi ya wengine na ya kibeberu. Na sambamba na kuipinga fikra hiyo alikuwa akisisitiza kwamba Uislamu si dini ya utaifa, na si dini ya ukoloni na ubeberu, bali ni dini ya jamii ya mataifa ambayo inaikubali mipaka bandia na tofauti za rangi kwa sababu tu ya kurahisisha kuwajua na kuwatambua watu, si kuwa sababu ya kubana na kufinya upeo wa uono wa wanajamii.

Sambamba na kuupinga utaifa kwa sababu ya ardhi ya asili anakotoka mtu, Iqbal-e Lahori alikuwa akizungumzia utaifa unaotokana na Uislamu na kusisitiza kuwa inapasa kuweka kando fikra ya utaifa inayofuata misingi ya nchi na badala yake kuufanyia kazi umoja wa kidini katika jamii ya Kiislamu. Mtazamo wa utaifa wa kidini aliokuwa nao Iqbal-e Lahori umeakisiwa pia katika mashairi yake kwa kusisitiza kuwa Muislamu anapaswa afungamane kwanza na Uislamu wake na si ardhi na mipaka ya nchi yake. Mwanafikra na malenga huyo amezungumzia pia katika mashairi yake uwepo wa jamii nyingi za Kiislamu kama chachu ya kufikia kwenye umoja wa Kiislamu.

 

Iqbal-e Lahori aliguswa na kushughulishwa sana na mparaganyiko uliokuwa ukitawala katika Ulimwengu wa Kiislamu, machungu na mateso yaliyokuwa yakiwapata Waislamu na hali ya masaibu iliyokuwa imezikumba nchi za Kiislamu; na kwa hakika aliumia na kuhuzunishwa sana na upotokaji na kudhoofika kisiasa na kiakhlaqi Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na matatizo na masaibu yaliyoupata ambayo yalisababishwa na hali hiyo. Kwa mtazamo wa mwanamageuzi na mrekebishaji huyo wa umma, sababu hasa ya kubaki nyuma, kuwa dhaifu na kupotoka Ulimwengu wa Kiislamu ilikuwa ni kujiweka mbali na tunu na thamani za kimaanawi na kifikra za Uislamu. Kwa sababu hiyo alipendekeza fikra ya kile alichokiita "Kurejea kwenye Nafsi" kwa kutoa wito kwa Ulimwengu wa Kiislamu kushikamana na utamaduni na ustaarabu wake wa asili. Iqbal-e Lahori aliwataka Waislamu kurejea kwenye nafsi na asili yao na kutosheka na ustaarabu, utamaduni na Kitabu chao cha mbinguni.

Katika hali ambayo wanafikra wataalamishaji wengi waliokuwa katika zama za Iqbal-e Lahori walionekana zaidi kutekwa na kukubali fikra za Kimagharibi, mwanamageuzi huyo alikuwa mkosoaji wa Magharibi na akawa anatilia mkazo nukta hii, kwamba Waislamu wanapaswa kujitathmini na kurejea tena kwenye shakhsia na utambulisho wa Kiislamu na kuishika tena kamba ya umoja iliyowaponyoka. Iqbal-e Lahori alizichambua na kuzipembua sababu za kupotoka na kukengeuka Waislamu mkondo wa njia yao ya asili katika mambo yafuatayo:-

Mosi: Kutoendana utamaduni wa Waislamu na mahitaji mapya.

Pili: Kushindwa kuelewa maslahi yao ya kitaifa na kutoyashughulikia na kuyafanyia kazi.

Tatu: Kasoro na upungufu mkubwa uliokuwepo kwenye mfumo wa mafunzo na malezi.

Nne: Mfarakano na kutokuwepo usawa katika jamii za Kiislamu.

Tano: Kuenea mielekeo ya Usufi ndani ya jamii za Kiislamu.

Sita: Kufuata mambo kwa kuiga na kutii tu.

Saba: Tafsiri na ufahamu usio sahihi kuhusu kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Nane: Kukosa kuwa na kiongozi mwema na mjuzi.

Na tisa kuwepo ufahamu potofu na usio sahihi wa kigeni katika utamaduni wa Kiislamu.

Iqbal-e Lahori alipendekeza mpango wa misingi minne kwa ajili ya kuasisi harakati ya Kiislamu ili kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Msingi wa kwanza ni kuwa na mapenzi na Qur’ani na kushikamana na mafudisho ya kitabu hicho cha mbinguni. Alikuwa akisisitiza katika mashairi yake kuwa haiyumkiniki mtu kuishi maisha ya Kiislamu pasina kuishi kwa kufuata Qur’ani. Msingi wa pili ni kurejea kwenye suna na mafundisho ya Kiislamu. Mrekebishaji huyo wa umma alikuwa akiitakidi kuwa kitu pekee cha kuulinda na kuuokoa umma ulio katika hali ya kuporomoka ni kushikamana kwake na suna, utamaduni na mafundisho yake yaliyopita na ya asili.

Msingi wa tatu ni kufuata hukumu na sharia za Kiislamu. Iqbal alikuwa akikumbusha kuwa siku Waislamu walipoyasahau mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW walipoteza nguvu na hamasa iliyojenga shakhsia yao na kuporomoka hadi kiwango cha chini kabisa cha kuwa duni na wanyonge.

Na msingi wa nne ni wa kuwepo kitovu na kituo kikuu cha kitaifa. Kwa mtazamo wa Iqbal-e Lahori ni msikiti mtukufu wa Makka au Al-Kaaba ndivyo vyenye nguvu isiyomalizika ya kuiunganisha jamii ya Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 14 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Inshallah katika sehemu ijayo ya 15 ya mfululizo huu tutakuja kuzungumzia fikra na mitazamo ya mrekebishaji mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu. Mwanafikra huyo si mwengine ila ni Muhammad Abdou. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags