Mar 06, 2018 06:31 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (15)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipita hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 15.

Kwa wale wasikilizaji wetu wanaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila ya shaka mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulikamilisha mazungumzo yetu kuhusu fikra na mitazamo ya Iqbal-e Lahori, mmoja wa wanamageuzi na warekebishaji umma wa Ulimwengu wa Kiislamu. Tulisema kuwa Iqbal alikuwa akiamini kuwa sababu hasa ya kubaki nyuma, kuwa dhaifu na kupotoka Ulimwengu wa Kiislamu ilikuwa ni kujiweka mbali na tunu na thamani za kimaanawi na kifikra za Uislamu. Kwa sababu hiyo alipendekeza fikra ya kile alichokiita "Kurejea kwenye Nafsi" kwa kutoa wito kwa Ulimwengu wa Kiislamu kushikamana na utamaduni na ustaarabu wake wa asili. Tukaashiria pia kwamba katika hali ambayo wanafikra wataalamishaji wengi waliokuwa katika zama za Iqbal-e Lahori walionekana zaidi kutekwa na kukubali fikra za Kimagharibi, mwanamageuzi huyo alikuwa mkosoaji wa Magharibi na akawa anatilia mkazo nukta hii, kwamba Waislamu wanapaswa kujitathmini na kurejea tena kwenye shakhsia na utambulisho wa Kiislamu na kuishika tena kamba ya umoja iliyowaponyoka. Mwanamageuzi na mrekebishaji huyo wa umma alipendekeza mpango wa misingi minne kwa ajili ya kuasisi harakati ya Kiislamu ili kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Msingi wa kwanza ni kuwa na mapenzi na Qur’ani na kushikamana na mafudisho ya kitabu hicho cha mbinguni. Msingi wa pili ni kurejea kwenye suna na mafundisho ya Kiislamu. Msingi wa tatu ni kufuata hukumu na sharia za Kiislamu. Na msingi wa nne ni kuwepo kitovu na kituo kikuu cha kitaifa. Kama nilivyokuahidini katika kipindi kilichopita leo tutazungumzia fikra na mitazamo ya Muhammad 'Abduh pamoja na Muhammad Rashid Ridha kuhusu maudhui ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Muhammad 'Abduh na Rashid Ridha walikuwa miongoni mwa wanafikra muhimu Waislamu ambao walifuatilia na kuendeleza fikra ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Sheikh Muhammad 'Abduh, aliyezaliwa mwaka 1266 na kuaga dunia mwaka 1323 hijria ni mmoja wa wanafikra wa Misri waliokuwa na ushawishi mkubwa. Fikra na misimamo yake ya kuendeleza na kustawisha dhana ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu iliathiriwa na mafundisho ya Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi. Sheikh Muhammad 'Abduh ambaye alihesabiwa kuwa mwanafunzi na muridi wa Sayyid Jamaluddin, kutokana na kuathiriwa na mafundisho ya mwalimu wake, alihuisha fikra ya kidini na akafanya juhudi kubwa kupitia utoaji tafsiri mpya kuhusu Uislamu ili kuyapatia majibu maswali ya Waislamu kulingana na mahitaji ya zama. Wakati ambapo Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi alichanganya fikra ya umoja na jitihada za kurekebisha fikra za kidini na kisiasa za Waislamu kwa kuchukua hatua za kivitendo kwa kuilenga mihimili ya utawala na uongozi, Muhammad 'Abduh, yeye badala ya kulipa kipaumbele suala la kupambana na udikteta wa ndani na ukoloni wa maajinabi, kama vizuizi vya kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, mikakati yake mikuu kuelekea umoja huo ililenga kuleta marekebisho na mageuzi ya kifikra, kiutamaduni na kimafunzo ndani ya jamii za Waislamu wenyewe.

Sheikh Muhammad 'Abduh, kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin, alikuwa akiamini kuwa moja ya sababu kuu za mfarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu ni mpasuko wa kimadhehebu uliokuwepo baina ya Shia na Suni. Kwa sababu hiyo aliandika sherhe ya Nahjul-Balaghah kama jitihada ya kujenga nadharia ya umoja wa Kiislamu kwa msingi wa kutatua hitilafu na tofauti za kimadhehebu kati ya Shia na Suni. Katika nadharia yake ya umoja na kuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu, Sheikh Muhammad 'Abduh alitilia mkazo misingi mitatu ifuatayo: Kwanza ni ulazima wa kuleta mlingano na uwiyano kati ya akili na dini katika Uislamu. Pili, udharura wa ijtihadi katika masuala ya kidini kwa kushikamana na msingi wa tauhidi, utangulizi wa kiakili na mahitaji ya zama. Na msingi wa tatu ni kufungamanisha uhuru na irada ya mtu pamoja na mas-ulia na wajibu. Katika hali ambapo kuongezeka nguvu na ushawishi wa kiutamaduni wa Ulaya kwenye nchi za Kiislamu katika karne ya 19 kulikuwa kumeandaa mazingira ya kuibuka vuguvugu la mwamko wa Kiislamu wa kukabiliana na ufisadi na upotofu wa ndani na vitisho vya nje, Sheikh Muhammad 'Abduh alikuwa akifanya jitihada za kutumia fikra za Kimagharibi ili kuleta mageuzi katika jamii ya Kiislamu. Katika kipindi cha baina ya vita viwili vikuu vya dunia, mwanafikra na mlinganiaji huyo wa Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu aliweza kuleta vuguvugu la mageuzi ya Kiislamu ndani ya Misri ambayo katika kipindi hicho ilikuwa kitovu cha mashinikizo kinzani ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiidiolojia.

Waislamu wa madhehebu mbalimbali wakisali pamoja Sala ya Jamaa nyuma ya Mufti wa Syria

 

Harakati ya kuhuisha fikra ya kidini hususan dhana ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu iliendelezwa pia na Rashid Ridha, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Muhammad 'Abduh. Rashid Ridha alitokana na kizazi cha wahajiri kutoka Syria ambao mnamo mwishoni mwa karne ya 19 waliifanya Misri kuwa wat’ani na nchi yao na kitovu cha harakati zao za kifikra na kiutamaduni na hata wakaweza kupata mwanga mpana zaidi kuhusiana na malengo ya mustakabali wa Ulimwengu wa Kiislamu. Rashid Ridha alikuwa akilaani taasubi za kikaumu; na kwa sababu hiyo alikuwa akimlaumu Ibn Khaldoun kwa mtazamo wake wa kusifia na kuenzi taasubi. Licha ya kukosoa mielekeo ya kikaumu na kupenda utaifa kupindukia alikuwa mtetezi mkubwa wa mielekeo ya utaifa wa Kiarabu wa Syria kiasi kwamba mnamo mwaka 1920 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kongresi ya Taifa ya Syria iliyomtawaza Faisal kuwa mfalme wa nchi hiyo. Rashid Ridha alikusanya na kuchanganya pamoja katika fikra zake hamasa na mafunzo ya utaifa wa Kiarabu pamoja Umajimui wa Kiislamu, kwa kimombo Pan-Islamism.

Rashid Ridha, ambaye kwa upande wa sha’ar na misingi ya urekebishaji wa dini alikuwa akiwafuata Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi na Sheikh Muhammad 'Abduh, kinyume na mwalimu wake 'Abduh, alikuwa akitilia mkazo sana umoja wa Kiislamu sambamba na kuendelezwa Ukhalifa. Alikuwa akitaka kurejeshwa Ukhalifa katika muundo uleule wa zama za mwanzoni mwa Uislamu sambamba na kufanyiwa marekebisho na kuondolewa kasoro ulizokuwa nazo. Kutokana na nafasi maalumu aliyokuwa amelipa jopo la wapitisha maamuzi ambalo katika historia ya Uislamu lilijulikana kama "Ahlul-Halli wal-Aqd", Rashid Ridha alikusudia kuutatua mgogoro wa Ukhalifa katika zama zake. Kwa tathmini yake, Khilafa ya Waturuki ilikuwa na upotofu uliokengeuka misingi ya haki na uadilifu wa Kiislamu, hivyo akataka mapokezano ya ukhalifa yafanyike kwa kutumia utaratibu wa jopo la wapitisha maamuzi ambalo ni mwakilishi wa umma. Kiini cha fikra kuu za Rashid Ridha kuhusu Ukhalifa, badala ya kukita zaidi katika kumzingatia Khalifa mwenyewe, kinatilia mkazo kwenye "Ahlul-Halli wal-Aqd", yaani jopo la wawakilishi wa umma ambalo ndiyo msingi mkuu unaojenga utawala wa Kiislamu unaozungumziwa na mwanafikra huyo.

 Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 15 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kusita hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 16 ya mfululizo huu. Nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags