Mar 07, 2018 12:09 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (18)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 18.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulizungumzia sababu za mifarakano na kuwa dhaifu Waislamu na njia za kukabiliana na hali hizo kwa mtazamo wa fikra na mitazamo ya wanafikra na warekebishaji umma wawili wa Ulimwengu wa Kiislamu ambao ni Sheikh Muhammad 'Abdou na Rashid Ridha; na tukaashiria kwamba kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi, Muhammad 'Abdou, naye pia alikuwa akiitakidi kuwa moja ya sababu kuu za kuwepo mfarakano na mgawanyiko ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu ni mpasuko wa kimadhehebu baina ya Shia na Suni. Kwa sababu hiyo aliandika sherhe ya Nahjul-Balaghah ili kujaribu kujenga msingi wa umoja wa Kiislamu kupitia utatuzi wa hitilafu za kimadhehebu kati ya Shia na Suni. Katika nadharia yake kuhusiana na umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, Sheikh Muhammad ‘Abdou alikuwa akitilia mkazo misingi mitatu: Wa kwanza ni ulazima wa kuleta mlingano na uwiyano kati ya akili na dini katika Uislamu. Pili, udharura wa ijtihadi katika masuala ya kidini kwa kushikamana na msingi wa tauhidi, utangulizi wa kiakili na mahitaji ya zama. Na msingi wa tatu ni kufungamanisha uhuru na irada ya mtu pamoja na mas-ulia na wajibu. Aidha tulipozungumzia mitazamo ya Rashid Ridha tuliashiria nukta hii kwamba wakati wanamageuzi na wanafikra waliokuwa na fikra mpya wa Ulimwengu wa Kiarabu wa zama zake walikuwa wakipigia upatu fikra kama ya Umajimui wa Kiarabu, Uzalendo wa Kiarabu, na Vuguvugu la Kiarabu, Rashid Ridha alikuwa akisisitiza kwamba, njia pekee ya kujiondoa kwenye hali ya kulemaa na kubaki nyuma kimaendeleo na kufikia ustawi ni kupatikana umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu. Katika kipindi chetu cha leo, na kama nilivyoahidi, tutazungumzia sababu za mifarakano na kuwa dhaifu Waislamu na njia za kukabiliana na hali hizo kwa mtazamo wa fikra na mitazamo ya mwanafikra na mrekebishaji umma mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu ambaye ni Abdurahman Al-Kawakibi.

Mkutano wa Wahda, Tehran, Iran

 

Abdurahman Al-Kawakibi ambaye asili yake ni Muirani alizaliwa katika mji wa Halab au Aleppo nchini Syria mwaka 1854 na akaaga dunia mwaka 1902. Alilelewa na kukulia Syria na akashiriki katika harakati za uandishi wa magazeti na jumuiya zilizokuwa zikijishughulisha na masuala ya elimu. Kwa muda fulani, Al-Kawakibi aliwahi kuwa meya wa mji wa Halab. Harakati za mwanafikra na mwanamageuzi huyo wa Ulimwengu wa Kiislamu zilikita zaidi katika kupinga udikteta wa Waturuki wa Kiothmaniyya, suala ambalo hakughafilika nalo katika hali na mazingira yoyote aliyokuwa. Kutokana na harakati zake za kisiasa na mbinyo na mashinikizo ya Waturuki, hatimaye Abdurahman Al-Kawakibi alihama Syria na kuelekea Misri ambako ndiko alikofia.

Japokuwa mwanafikra huyo aliathiriwa na Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi na kutaka kuendeleza fikra zake kuhusiana na umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, lakini alitafautiana naye kimtazamo katika baadhi ya mambo. Wakati Sayyid Jamaluddin alikuwa akiuchukulia uingiliaji wa maajinabi na madola ya kigeni katika ardhi za Kiislamu kuwa ndio chanzo kikuu cha masaibu ya Waislamu, mpaka akawa anazishambulia vikali sera na siasa za dola la kikoloni la Uingereza kupitia jarida lake la Al-Urwatul-Wuthqa; Al-Kawakibi aliziangalia sababu za ndani jinsi zilivyochangia kuwafanya Waislamu wabaki nyuma kimaendeleo na kuwatolea wito wa kubadilika na kujirekebisha wao wenyewe. Alikuwa akiamini kuwa kutengemaa Waislamu wenyewe kutazuia hatamu za kuamua juu ya mustakabali wa nchi za Kiislamu kuangukia mikononi mwa maajinabi; na kwa sababu hiyo, Abdurahman Al-Kawakibi alikuwa akiwahimiza sana Waislamu kwenda madrasa na skuli na kuwa na hima kubwa ya kujifunza elimu.

Al-Kawakibi amealifu vitabu viwili muhimu kuhusiana na kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu, vizuizi vya maendeleo na suala la umoja wa Kiislamu, ambapo katika kila kimoja kati ya vitabu hivyo amegusia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuhusu maudhui ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu. Vitabu vyenyewe ni T'abayiu'l-Istibdad na Ummul-Quraa. Maudhui kuu ya kitabu cha T'abayiu'l-Istibdad wa Masariu'l-Isti'ibad ni uimla na udikteta. Inasemekana kuwa katika kualifu kitabu hicho Al-Kawakibi alichota pia fikra na mitazamo ya mwanafikra mashuhuri wa Kitaliana na kiranja wa mielekeo ya utaifa katika nchi hiyo Vittorio Alfieri. Alfieri, ambaye yeye mwenyewe alitekwa na fikra na mitazamo ya Montesquieu, mwanafalsafa wa siasa mashuhuri wa Kifaransa, alijulikana kama adui mkubwa wa udikteta. Katika maandiko yake, Vittorio Alfieri alikuwa akieleza bayana kuwa lengo kuu la fikra, kauli na maandiko yake ni kupambana na udikteta wa namna yoyote ile iwayo.

Hatukukutuma (Ewe Muhammad) ila uwe rehema kwa viuombe wote (Wiki ya Umoja)

 

Katika kitabu cha T'abayiu'l-Istibdad, Abdurahman Al-Kawakibi amemwashiria mwanafikra huyo wa Kitaliana na kuzitolea tafsiri fikra zake kwa kutumia misingi ya Kiislamu. Aliuelezea uimla na udikteta kama balaa kubwa zaidi kwa wanadamu ambao unakitumia kila kitu kwa manufaa yake, unafisidi akhlaqi, unazuia elimu na ustawi, unaangamiza utu, unaitumia dini kama wenzo wa kutawalia, unasababisha matabaka ya kiuchumi kupitia urundikaji mali, unazuia kuwepo malezi sahihi ya jamii, unaangamiza uhuru na unawafanya watu watumwa na wajakazi wake.

Kwa mtazamo wa Al-Kawakibi, udikteta ndio mama wa ufisadi; na chanzo chake ni Waislamu wenyewe kuwaiga na kuwafuata kibubusa viongozi wa Kikristo. Mwanafikra huyo alikuwa akiamini kuwa ujinga na utovu wa uelewa waliokuwa nao Waislamu na kushindwa kuwakemea na kuwawajibisha madikteta wanaowatawala ndio sababu ya kurithiwa ugonjwa huo ulio mithili ya ukoma na kizazi cha watawala wanaofuatia. Kwa hivyo elimu na uelewa ndio adui mkuu wa udikteta. Katika kanuni alizopanga kwa ajili ya kuupatia dawa na kuuondoa udikteta, mwanafikra huyo alikuwa hakubaliani asilani na njia za utumiaji nguvu, bali akiitakidi kwamba inapasa utumike upole na njia ya ueleweshaji na uelimishaji watu kidogo kidogo na kuwatambulisha hali iliyopo ili yapatikane mazingira ya kulifanya kasri bandia la udikteta liporomoke lenyewe kwa lenyewe kutokea ndani kwa mikono ya madikteta wenyewe. Abdurahman Al-Kawakibi, kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi alikuwa akisisitiza ulazima wa Waislamu kuwa na uelewa wa kisiasa, na akiamini kwamba mwisho wa yote, kitu kitakachoweza kuzuia na kukabiliana na udikteta ni mwamko na uelewa wa kisiasa na kijamii pamoja na usimamizi wa Waislamu wenyewe.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 18 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kusita hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 19 ya mfululizo huu. Nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags