Mar 12, 2018 06:55 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Machi 12

Hujambo mpenzi mwanaspoti wa RT na karibu katika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyogonga vichwa vya habari ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa, karibu……

Basketboli ya walemavu, Iran yatinga fainali za dunia

Timu ya taifa ya wanawake ya mpira wa kikapu ya walemavu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya bara Asia ya basketboli ya viti vya magurudumu baadaye mwaka huu 2018 nchini Indonesia. Hii ni baada ya kuzigaragaza mfululizo timu tano za bara hili, katika mashindano ya kieneo ya mchezo huo yanayofahamika kwa Kimombo kama Asia and Oceania Qualification Tournament, yaliyofanyika huko Bangkok, mji mkuu wa Thailand. Siku ya Ijumaa, wanawake hao wa Kiirani waliwachabanga mahasimu kutoka Afghanistan vikapu 40-23, katika mchezo wa nusu fainali, na hivyo kuingia kwa kishindi kwenye fainali. Iran ilivaana na mwenyeji Thailand katika mchuano wa mwisho siku ya Jumamosi na kuibuka kidedea. Timu hiyo ya basketboli ya walemavu ya Iran ilitandika Thailand katika mchuano wa ufunguzi mnamo Machi 5, na kuidhalilisha timu hiyo mwenyeji kwa vikapu 45-30, kabla ya kuigeuza India kichwa cha mwendawazimu na kuinyoa kwa chupa kwa kuisagasaga vikapu 74-4. Kabla ya hapo, timu hiyo ya Iran iliziumiza timu za Thailand na Cambodia vikapu 53-14 na 58-17 kwa usanjari huo. Kwa ushindi huo, wanawake hao wa Kiirani watashiriki mashindano ya kikanda yajulikanayo kama Asian Para Games yatakayofanyika huko Jakarta, mji mkuu wa Indonesia kuanzia Oktoba 6 hadi 13 mwaka huu.

Ligi ya Klabu Bingwa Afrika

Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika, TP Mazembe imeanza kwa kishindo kampeni ya kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuizamisha UD Songo ya Msumbiji mabao 4-0. Mechi hiyo ya hatua ya kwanza ilichezwa jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika Uwanja wa Frederic Kibassa Maliba. Mabao ya mazembe ambao ni mabingwa wa taji hilo mwaka 2015 yalifungwa na Malango Ngita aliyefunga mabao matatu ya hatrick na Muleka J aliyefunga bao moja. Katika mchezo mwingine Difaa Al Jadida ya Morocco iliicharaza Vita Club ya DRC kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji kutoka Tanzania Simon Msuva.

TP Mazembe, mabingwa watetezi

Gor Mahia ya Kenya ilitoshana nguvu na Esperance ya Tunisia kwa sare ya bila kufungana wakati Zanaco ya Zambia ilishindwa kwa mabao 2-1 na timu ya mbabane Swallows ya Swaziland. Wawakilishi wengine wa Afrika Mashariki, Rayon Sports ya Rwanda ilishindwa kutamba nyumbani kwa kutoka suluhu na mabingwa wa mwaka 2016, Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini.

Matokeo ya michezo mingine ya Ligi ya mabingwa Afrika yalikuwa kama ifuatavyo;

Zesco ilifungwa bao 1-0 na Asec Mimosas ya Ivory Coast. St. George ya Ethiopia ilitosha nguvu kwa sare ya bila kufungana na KCCA ya Uganda. Waydad Casablanca iliishinda Williumsville ya Ivory Coast kwa mabao 7-2. Premeiro de Agosto ya Angola iliishinda Bidvest Wits ya Afrika Kusini kwa bao 1-0. Adouana Stars ya Ghana iliishinda Entente Setif ya Algeria kwa bao 1-0. Mechi za marudiano zinatarajiwa kuchezwa katikati ya mwezi huu wa Machi. Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika matokeo ya mechi za hivi karibuni; Simba ilitoka sare ya kufungana mabao 2-2 na Al-Masry ya Misri, katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la shirikisho barani Afrika.

Umeme ulikatika wakati mchezo huo ukiwa unaendelea kutokana na kunyesha mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali, na kupelekea waamuzi wa mchezo huo kusitisha mchezo zikiwa zimesalia dakika 7 mchezo kumalizika ikiwa ni dk 83 kipindi cha pili kutokana na uwanja kujaa maji na kugubikwa na giza totoro. magoli ya Al Masry yalifungwa na Ahmed dakika ya 12 na Abdalraof aliyefunga kwa penati dakika ya 25, magoli ya Simba yote yamepatikana kwa penati zilizopigwa na John Bocco dakika ya 9 na Emmanuel Okwi dakika ya 74.

 

Olimpic Stars ya Burundi iliotoka sare ya bila kufungana na Hilal El Obeid ya Sudan. Waleyta Dicha ya Ethiopia ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zamalek ya Misri. AS Maniema ya DRC ilifungana mabao 2-2 na USM Alger ya Algeria. Enyimba ya Nigeria iliishinda Energie Sports ya Benin mabao 2-0. APR ya Rwanda ilifungwa na Djoliba ya Mali kwa bao 1-0. Coast do Sol ya Msumbiji ilifungwa bao 1-0 na Cape Town City ya Afrika Kusini.

Bao la Wanyama lashinda tuzo

Mchezaji nyota wa soka raia wa Kenya Victor Wanyama ameshinda tuzo ya goli bora la mwezi wa Februari mwaka 2018 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, Ijumaa. Nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, aliwapiku mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2017 Mohamed Salah (Liverpool & Misri) pamoja na Sergio Aguero (Manchester City & Argentina), Jose Izquierdo (Brighton & Hove Albion & Colombia), Adam Smith (Bournemouth & Uingereza) na Mario Lemina (Southampton & Gabon). Kiungo huyu mkabaji wa Tottenham Hotspur alivuta kiki zito kutoka nje ya kisanduku lililosaidia klabu yake kutoka 2-2 dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield hapo Februari 4. Katika mchuano huo, Wanyama aliingia kama nguvu-mpya katika dakika ya 79 akijaza nafasi ya Mbelgiji Mousa Dembele. Aliona lango dakika moja baadaye akiisawazishia Spurs 1-1.

Mvamizi hodari Harry Kane alikosa nafasi ya kuweka Spurs 2-1 juu alipopoteza penalti dakika ya 87 kabla ya Salah kupachika bao tamu dakika ya 91 lililowania tuzo ya goli bora la Februari. Kane alipata nafasi nyingine ya kufuma penalti dakika ya 95 na akaifunga, huku mechi hiyo ikatamatika 2-2. Salah alifunga mabao yote ya Liverpool dhidi ya Tottenham siku hiyo. Bao la Aguero lilikuwa dhidi ya Leicester City mnamo Februari 10.

Na tunatamatisha kwa kutupia jicho baadhi ya matokeo ya mechi zilizopgwa karibuni hivi katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Jumamosi ya March 10 2018 katika uwanja wa Old Trafford, Man United waliikaribisha Liverpool kucheza mchezo wa kumaliza ubishi kati ya Jurgen Klopp na Jose Mourinho. Katika mchuano huo, mwenyeji Man U ilipata ushindi wa magoli 2-1, yaliyofungwa na Marcus Rashford dakika ya 14 na 24 wakati goli pekee la Liverpool kilipatikana kwa beki wa Man United Eric Bailly kujifunga dakika ya 66 baada ya kushindwa kuzuia mpira uliopigwa na Sadio Mane.

Huo unakuwa ni ushindi wa 88 wa Man United dhidi ya Liverpool toka wakutane kwa mara ya kwanza April 28 1894 katika mchezo uliyomalizika kwa Liverpool kushinda kwa magoli 2-0. Arsenal imemaliza kipindi cha kushindwa mfululizo katika ligi ya Premier kwa kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Watford Jumapili. Shkodran Mustafi alitumbukiza wavuni free-kick ya Mesut Ozil na kuwapa Gunners bao la kwanza dakika ya nane kabla ya Pierre-Emerick Aubameyang kutumbukiza pasi yake Henrikh Mkhitaryan bao la pili. Mkhitaryan aligonga msumari wa mwisho kwa jeneza la Watford na kuipa Arsenal ushindi wa kwanza tangu wawalime Everton 5-1 tarehe tatu Februari.

Arsene Wenger

Ushindi huo unaiweka Arsenal nafasi ya sita katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 10, na cha muhimu zaidi, umepunguza mashinikizo ya kumtaka mkufunzi wa klabu hiyo Arsene Wenger ajiuzulu.

Kwengineko New Castle iliichabanga Southampton mabao 3-0 namna ambavyo Westham iligaragazwa na Burnley.

……………………..TAMATI…………………