Mar 14, 2018 07:32 UTC
  • Umoja wa Kiislamu
    Umoja wa Kiislamu

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 19.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia fikra na mitazamo ya mrekebishaji umma mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu ambaye ni Abdurahman Al-Kawakibi. Tukasema kuwa, kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi Al-Kawakibi alikuwa akisisitiza ulazima wa Waislamu kuwa na uelewa wa kisiasa, na akiamini kwamba mwisho wa yote, kitu kitakachoweza kuzuia na kukabiliana na udikteta ni mwamko na uelewa wa kisiasa na kijamii pamoja na usimamizi wa Waislamu wenyewe. Yeye kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi na kinyume na Muhammad 'Abdou, alikuwa akizipa kipaumbele cha kwanza harakati za kisiasa na kuwa na kiwango cha juu zaidi cha upeo wa uelewa wa kisiasa Waislamu wa kawaida kabla ya kurekebisha masuala mengine yanayohusiana na maisha yao; na alikuwa akiitakidi kwamba mwamko wa uelewa wa kisiasa unapasa uchochewe na uelewa wa kidini. Ili kurekebisha hali iliyokuwa ikitawala katika zama hizo, Abdurahman Al-Kawakibi alikuwa akiusia kurejea kwenye Uislamu wa asili; lakini kama walivyokuwa aghalabu ya warekebishaji umma wengine hakuuweka Uislamu kwenye migongano na mivutano na ustaarabu wa Magharibi.

Katika kitabu chake cha T'abayiu'l-Istibdad, tulichoanza kukizungumzia katika kipindi kilichopita, Al-Kawakibi ameushambulia vikali udikteta lakini hakuuelezea moja kwa moja kuwa kizuizi na kikwazo cha umoja wa Kiislamu, bali amebainisha kuwa athari, matokeo na madhara ya uimla na udikteta ni katika vizuizi vya kupatikana umoja wa Kiislamu. Yeye alitilia mkazo nafasi ya Uislamu na hasa msingi wa tauhidi katika kukana udikteta na kutilia nguvu uhuru unaofuatiwa na tauhidi na umoja wa Waislamu wote duniani na akabainisha kwamba, maadamu Waislamu wako kwenye makucha ya dhulma na udikteta na kuwa watumwa wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, hawatoweza kuungana na kuwa wamoja. Kwa hakika katika mtazamo wa Al-Kawakibi, udikteta uko katika daraja moja na shirki kwa sababu ya kusababisha mgawanyiko na utengano ndani ya umma wa Kiislamu; na kwa mtazamo wa kisiasa, mawili hayo yako dhidi ya uhuru na tauhidi. Abdurahman Al-Kawakibi alikuwa akiitakidi kwamba Uislamu ni dini ya tauhidi na umekuja, ili kutokomeza shirki na kuleta umoja. Huku akiashiria sisitizo la Qur’ani kuhusu shura na mashauriano, aliichambua nafasi ya udikteta katika kuleta mfarakano wa kidini na mgawanyiko wa umma na kuweka vizuizi vya kukwamisha umoja na kusisitiza kuwa imani ya tauhidi ni chimbuko la kuwa huru na kukomboka na vitu vingine na sababu ya kuimarika, kukamilika na kuunganika umma mmoja wa Uislamu; na shirki au kukosekana tauhidi ni kizuizi cha umoja na sababu ya kuwepo dhulma na ufisadi na utengano na mfarakano.

Waislamu wa India

 

Katika kitabu chake cha pili alichokipa jina la Ummul-Quraa, Abdurahman Al-Kawakibi amezungumzia mkakati wa kuleta umoja wa Kiislamu, ambao kitovu na makao yake makuu ni mji mtakatifu wa Makka. Katika mpango wake huo ambao inasemekana kuwa si wa uhalisia bali uliotokana na ndoto na matamanio tu aliyokuwa nayo juu ya jambo hilo, mwanafikra huyo alibuni majimui, jumuiya ya kimataifa au ya ulimwengu wa Waislamu huko Makka, ambapo katika hadhara yao hiyo wanazungumzia sababu za udhaifu na kupotoka Waislamu, chanzo chake pamoja na kutafuta njia za utatuzi sambamba na kuanzisha ushirikiano na mashauriano kati ya wawakilishi wa mataifa yote ya Waislamu. Kimsingi Al-Kawakibi alikuwa anafuatilia lengo tukufu na tamanio kuu la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu kupitia uondoaji hatua kwa hatua hali ya upotokaji na kubaki nyuma kimaendeleo Waislamu na kuleta mwamko na umoja wa Kiislamu. Msingi wa kongamano hilo la kidhahania lililobuniwa na Al-Kawakibi ni kutafuta chanzo na sababu za kudhoofika na kuacha Waislamu njia yao ya asili na kupendekeza njia za kukabiliana na hali hiyo. Na inavyotarajiwa, wawakilishi wanaoshiriki kongamano hilo watakuwa watu wenye uelewa sahihi juu ya hali na mazingira ya Ulimwengu wa Kiislamu na changamoto zilizopo na kisha kupendekeza mipango na njia mwafaka za kutatua au kwa akali kupunguza matatizo ya kisiasa na kijamii ya Ulimwengu wa Kiislamu. Hima kubwa aliyokuwa nayo Al-Kawakibi ya kubuni kongamano hilo la kidhahania ilikuwa ni kutaka kubainishwa nukta za udhaifu na changamoto zilizopo katika nchi za Kiislamu. Na sababu yake ni itikadi na imani aliyokuwa nayo kwamba tatizo hilo kubwa na sugu litaweza kutatuliwa ikiwa tu umma wa Kiislamu utashikamana pamoja kupitia kongamano la kimataifa la Kiislamu.

********

Katika kitabu hicho cha Ummul-Quraa, Abdurahman Al-Kawakibi amezungumzia masaibu ya jamii ya Kiislamu na sababu ya kubaki nyuma Waislamu, na akaashiria kwa njia isiyo ya wazi ulazima na udharura wa umoja na mshikamano wa Waislamu; ambapo kongamano hilo lilikuwa kama nembo ya harakati hiyo. Kutokana na tija iliyopatikana katika mazungumzo ya kongamano hilo mpigania umoja huyo wa Ulimwengu wa Kiislamu alifikia hitimisho kwamba ufahamu pogo na potofu na kuwa mbali na hakika ya Uislamu; kila mmoja kung’ang’ania rai yake na kukataa mashauriano na fikra ya mwenzake; kutokuwepo uhuru katika nyanja zote ikiwemo wa kutoa mawazo na maoni, katika masuala ya elimu na ya Kiislamu; kuacha Waislamu msingi wa kuamrisha mema na kukataza mabaya; upuuzaji unaofanywa katika masuala ya dini na kuyatumia kwa malengo ya binafsi; satua na ushawishi walionao mashekhe wa majina na wenye ukuruba na watawala ndani ya jamii ya Kiislamu; fikra mgando zilizopo katika kuzungumzia elimu za kidini na kutoshughulikia elimu za kisasa; kuvunjika moyo na hisia za kukata tamaa na kupoteza matumaini zilizoenea baina ya Waislamu; kutokuwepo kiongozi mahiri, mwenye tadbiri na ikhlasi anayestahiki kufuatwa na Waislamu wote; ufakiri na ukata pamoja na ushari, ujinga na hulka mbovu zinazotokana na masaibu hayo; watawala waimla na madikteta na wenye kiburi; kuachwa hukumu za Uislamu na kutotekelezwa sheria za adhabu pamoja ujinga na utovu wa uelewa uliotawala ndani ya mataifa ya Waislamu ni miongoni mwa sababu kuu za kulemaa na kubaki nyuma kimaendeleo jamii ya Kiislamu.

 

Hitimisho la mwisho analofikia Al-Kawakibi katika kitabu cha Ummul-Quraa limejikita juu ya misingi mitatu: Wa kwanza ni kuwa, Waislamu wako dhaifu na wamebaki nyuma kimaendeleo; na ni jambo la wajibu na lenye ulazima kuondoa udhaifu huo. Msingi wa pili ni kuwa chimbuko na chanzo cha masaibu iliyonayo jamii ya Kiislamu ni ujinga; na dawa yake ni utaalamishaji kwa njia ya elimu na ushajiishaji kuelekea ustawi. Na msingi wa tatu ni kuwepo haja na ulazima wa kuitisha kongamano la kuyatafutia dawa masaibu hayo na wajibu na mas-ulia aliyonayo kila Muislamu hususan shakhsia wakubwa na maulamaa wa umma wa Kiislamu juu ya suala hilo. Kwa muhtasari tunaweza kusema kuwa udikteta uliokuwa umetawala katika jamii za Kiislamu ndilo suala kuu lililokuwa limeishughulisha akili na fikra za Abdurahman Al-Kawakibi, lakini umoja, mshikamano na mwamko wa Waislamu na nchi za Kiislamu nayo pia ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakipewa umuhimu na mwanafikra huyo.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 19 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 20 ya mfululizo huu. Nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags