Mar 14, 2018 07:48 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (20)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 20.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tumezungumzia sababu za mifarakano na kuwa dhaifu Waislamu, na njia za kukabiliana na matatizo hayo kwa mtazamo wa maulamaa wa Kisuni. Kuanzia kipindi chetu hiki na vyengine vichache vijavyo tutazungumzia jinsi suala la umoja wa Kiislamu lilivyopewa nafasi na maulamaa na wanafikra wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia.

Kama mjuavyo wasikilizaji wapenzi mijadala kuhusu suala la umoja wa Kiislamu, inarejea kwa sehemu kubwa kwenye kipindi cha miaka 150 iliyopita; na mijadala hiyo imefanyika zaidi kwa sura ya harakati na jibu dhidi ya mashinikizo ya Ukoloni na mapambano yaliyojiri baina ya Ulimwengu wa Kiislamu na Magharibi. Amma kuhusu hitilafu kati ya Shia na Suni na juhudi zilizofanywa kwa madhumuni ya kuondoa hitilafu hizo, hilo ni suala lenye historia ndefu. Kwa kuzingatia nafasi na mchango muhimu uliotolewa na kitabu cha Al-Ghadir, kuanzia sehemu ijayo ya 21 ya kipindi hiki cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu tumekusudia kuashiria kwa muhtasari baadhi ya hitilafu za mitazamo baina ya Mashia na Masuni na kubainisha jitihada mbalimbali zilizofanywa na maulamaa wa Kishia za kutatua hitilafu hizo, hususan Allamah Amini, mwandishi wa Kitabu cha Al-Ghadir kinachohakiki tukio la Ghadir Khum kwa mujibu wa mapokezi ya Ahlu-Sunnah.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki, mtakuwa mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi vyetu vya utangulizi tulidokeza kuwa hitilafu baina ya Masuni na Mashia zinarejea tangu zama za mwanzoni mwa Uislamu na zilianza baada ya kuibuka suala la Khalifa wa Bwana Mtume Muhammad SAW baada ya kuaga dunia mtukufu huyo. Lakini kushika madaraka ya utawala Bani Umayyah kulipanua wigo na kukoleza moto wa hitilafu hizo. Kabla ya utawala wa Bani Umayyah, hitilafu hizo hazikusababisha kutokea ugomvi na mzozo mkubwa baina ya Waislamu, lakini dhamira ya Bani Umayyah ilikuwa ni kutangaza na kuonyesha uadui wa dhahiri shahiri na wa utumiaji nguvu dhidi ya Ahlul-Bayt wa Mtume SAW na Mashia; na hatua hiyo ilisababisha hitilafu hizo kuwa kubwa zaidi na kufuatiwa na matukio ya umwagaji damu. Ukweli ni kwamba Bani Umayyah ndio waasisi wa harakati ya kuwatusi na kuwavunjia heshima Maimamu watoharifu wa kizazi cha Bwana Mtume Muhammad SAW na wafuasi wao, yaani Mashia.

 

Katika zama za utawala wa Bani Abbas pia, japokuwa wao wenyewe walikuwa wakijinasibu kuwa wametokana na ukoo wa Bwana Mtume na Maimamu, lakini ukweli ni kwamba watawala wa Bani Abbas walishadidisha mashinikizo kwa Mashia au kwa jina jengine Maalawi. Bani Abbasi walishika hatamu za madaraka kwa kutumia kaulimbiu za Maalawi na fikra zinazoafikiana na Shia, lakini kutokana na tamaa za kisiasa, baada ya muda wakabadilika na kuanzisha uadui dhidi ya Mashia na kuendeleza harakati ya mauaji dhidi ya Maalawi. Na jambo hilo likawa sababu ya kushtadi hitilafu ambazo zilianzia katika miji ya Kufa na Basra, zikasambaa na kuenea ulimwengu mzima wa Kiislamu. Bani Abbas walikuwa wakizisaidia kifedha madhehebu zilizokuwa wapinzani na maadui wa Mashia ili kuwaudhi na kuwanyanyasa wafuasi hao wa Ahlul-Bayt wa Bwana Mtume SAW. Hatua hizo tab’an hazikunyamaziwa kimya na Mashia; bali nao pia walichukua hatua mkabala dhidi ya baadhi ya hujuma hizo. Pamoja na yote hayo, maulamaa wa Kishia, ambao walikuwa na kusudio la kuunganisha na kuufanya kitu kimoja Ulimwengu wa Kiislamu, kama walivyokuwa baadhi ya maulamaa wa Kisuni wanaofikiria maslahi ya umma, waliwausia wafuasi wao wasali Sala za jamaa nyuma ya maimamu wa Kisuni na kuwatembelea wagonjwa hao, mbali na jitihada nyingine nyingi walizofanya za kupunguza hitilafu baina ya madhehebu hizo.

Kwa msingi huo tunaweza kuthubutu kusema kuwa, licha ya dhulma kadha wa kadha walizofanyiwa, Mashia wamekuwa siku zote wakitetea na kupigania umoja wa Waislamu; na kwa kushirikiana na wanafikra wa Kisuni, maulamaa na wanafikra wa Kishia katika zama zote wamejitahidi kutatua baadhi ya masuala yanayochochea mifarakano na kutilia nguvu suala la umoja baina ya Mashia na Masuni. Kwa kutoa mfano, wakati katika kipindi cha karne ya nne na tano hijria baadhi ya maulamaa wa Kishafi na Kihanafi walichukua hatua ya kuandika vitabu kadhaa kuhusu Imam Hussein (as), kikiwemo kitabu cha Maqtalul-Hussein cha Khawarazmi Al-Hanafi kwa madhumuni ya kufidia dhulma zilizotendwa huko nyuma, mnamo karne ya sita hijria, baadhi ya wanafikra wa Kishia waliokuwa katika mji wa Rei, kama Abdul-Jalil Qazwini Razi, walijitahidi kupunguza na kupoza moto wa baadhi ya fikra za Ushia kuhusiana na Masuni. Abdul-Jalil Qazwini, ni mmoja wa wanafikra wa Kishia wa mwaka 560 hijria aliyekuwa akiishi katika mji wa Rei ambao ulikuwa moja ya vitovu vya Waislamu wa Kishia katika ulimwengu wa zama hizo. Yeye alikuwa mmoja wa watu wa mwanzo waliozungumzia kinadharia na kwa uzito mkubwa suala la umoja baina ya Shia na Suni na akafanya jitihada kubwa za kupunguza mpasuko uliokuwapo kati ya madhehebu hizo mbili. Katika kitabu chake kiitwacho An-Naqdh, Abdul-Jalil Qazwini Razi alikihakiki na kukichambua kitabu kilichopewa jina la “Ba’dhu Fadhaaihir-Rawaafidh. Katika uhakiki wa kiukosoaji aliofanya, alizikosoa baadhi ya itikadi za kufurutu mpaka za Masuni kuhusiana na Ushia na vilevile akazimua moto wa baadhi ya fikra za Ushia katika mtazamo wa kisiasa. Kwa upande wa kisiasa pia, Abdul-Jalil Qazwini alifanya juhudi za kuikurubisha harakati ya Shia na utawala wa zama hizo wa Wasaljuqi.

Kongamano la umoja wa Kiislamu mjini Tehran

 

Kwa upande wa kifikra na kimtazamo, Abdul-Jalil Qazwini Razi, ni mmoja wa wananadharia muhimu wa Kishia katika suala la udharura wa kujengwa umoja baina ya madhehebu zote za Kiislamu na kuwaunganisha Waislamu hususan katika karne za katikati mwa historia ya Iran. Hata hivyo yeye si mwanazuoni na mwanafikra pekee wa Kishia aliyezungumzia fikra hizo. Nukta moja ya kupewa nadhari na mazingatio maalumu juu ya suala hilo, ni kwamba kujitokeza kwa Tasawwuf yaani Usufi katika karne ya sita, saba na ya nane, nako pia kulisaidia sana katika kuleta umoja baina ya madhehebu hizo. Kutokana na kutokuwa na ukereketwa wa kimadhehebu, Masufi waliandaa mazingira mwafaka ya kuwakurubisha Masuni na Mashia na kuwafanya maulamaa wa Kishia wa zama hizo wawe waamilifu na wenye harakati zaidi. Mnamo karne ya saba, na hasa wakati wa utawala wa kaumu ya Wamongolia, Khaje Nasiir T’usi, mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Shia aliweza kujikurubisha na utawala, ambapo sambamba na kujenga kituo cha uangaliaji sayari cha Maragheh katika eneo la Azerbaijan Mashariki hapa nchini Iran, aliwakutanisha pamoja baadhi ya wanafikra na wanasayansi wa Kishia na Kisuni; na bila ya kufanya upendeleo wowote, akawapa idhini ya kutangaza na kueneza fikra na mitazamo yao.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 20 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 21 ya mfululizo huu. Nakuageni na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags