Mar 14, 2018 08:10 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (21)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 21.

Katika kipindi cha juma lililopita tulieleza kuwa mijadala kuhusu suala la umoja wa Kiislamu inarejea kwa sehemu kubwa kwenye kipindi cha miaka 150 iliyopita na kwamba mijadala hiyo imefanyika zaidi kwa sura ya harakati na jibu dhidi ya mashinikizo ya Ukoloni na mapambano yaliyojiri baina ya Ulimwengu wa Kiislamu na Magharibi. Lakini tukaashiria kwamba kwa upande wa hitilafu kati ya Shia na Suni na juhudi zilizofanywa kwa madhumuni ya kuondoa hitilafu hizo, hilo ni suala lenye historia ndefu. Tukaeleza kuwa kwa kuzingatia nafasi na mchango muhimu uliotolewa na kitabu cha Al-Ghadir, katika sehemu hii ya 21 ya kipindi hiki cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu tutakuja kuzungumzia kwa muhtasari baadhi ya hitilafu za mitazamo baina ya Mashia na Masuni na kubainisha jitihada mbalimbali zilizofanywa na maulamaa wa Kishia za kutatua hitilafu hizo, hususan Allamah Amini, mwandishi wa Kitabu cha Al-Ghadir kinachohakiki tukio la Ghadir Khum kwa mujibu wa mapokezi ya Ahlu-Sunnah. Miongoni mwa wanafikra na maulamaa wa Kishia ambao tuliwaashiria katika kipindi kilichopita na mchango wao katika suala la kuuunganisha Ulimwengu wa Kiislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Shia na Suni ni Abdul-Jalil Qazwini Razi na Khaje Nasiir T’usi. Mbali na wanafikra na wanazuoni hao, Allamah Hilli, ambaye ni mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kishia, anaweza kwa namna fulani kutajwa kwa ni mwanafunzi wa Khaje Nasiir T’usi. Allamah Hilli ni mmoja wa wanazuoni ambao fikra zake zilikuwa na thamani kubwa sana katika kukamilisha fiqhi ya madhehebu ya Shia na ni mmoja wa watu waliofanya jitihada kubwa katika kupunguza ufa wa hitilafu za kimadhehebu baina ya Mashia na Masuni.

Mwito wa Umoja

 

Licha ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na maulamaa na wanafikra wa Kishia kwa madhumuni ya kufanikisha lengo la kufikiwa umoja baina ya Waislamu, baadhi ya watu wameitafsiri hatua iliyochukuliwa na maulamaa wakubwa kama Allamah Amini ya kutetea kimantiki na kwa hoja haki na ukweli wa madhehebu ya Shia kuwa ni kitendo cha kushadidisha hitilafu ndani ya umma wa Kiislamu. Al-Ghadir ni jina la kitabu kilichoandikwa na Allamah Amini kuthibitisha Wilayat ya Imam Ali bin Abi Talib (as). Kitabu hicho kimeandikwa kwa lugha ya Kiarabu; na kwa mtazamo wa baadhi ya wanazuoni ni kitabu chenye itibari kubwa zaidi kihoja kuthibitisha haki na ukweli wa madhehebu ya Shia. Ndani ya kitabu hicho, mwandishi ametaja majina ya masahaba 110 na matabiina 84, yaani watu walioishi pamoja na masahaba, ambao wameipokea Hadithi ya Ghadir, na jumla ya watu 360 ambao wameisimulia hadithi ya tukio hilo katika kipindi cha kuanzia karne ya pili hadi ya nne hijria. Si hayo tu, lakini mwishoni mwa kitabu hicho Allamah Amini ametaja mashairi yaliyotungwa na washairi mbalimbali kuhusiana na kadhia hiyo. Katika kualifu na kuandika kitabu cha Al-Ghadir, mwandishi alifunga safari na kufanya kazi ya kupitia maktaba za nchi tofauti za Kiislamu ikiwemo Iraq, India, Pakistan, Morocco, Misri pamoja nchi nyingine mbalimbali duniani. Kwa kutoa mfano, katika juzuu ya tatu ya kitabu cha Al-Ghadir, Allamah Amini amejibu tuhuma zilizotolewa na Rashid Ridha pale alipoeleza kwamba “Shia wanafurahia kila pigo na balaa la kushindwa linalowafika Waislamu, mpaka wakafika hadi ya kusherehekea ushindi wa Warusi dhidi ya Waislamu nchini Iran”. Katika jawabu aliyotoa kuhusiana na tuhuma hiyo, Allamah Amini amesema: “Huu ni uongo unaotungwa na kuandikwa na watu walio mfano wa Muhammad Rashid Ridha. Mashia wa Iran na Iraq ambao ndio zaidi wanaolengwa na tuhuma hii, na vilevile wataalamu wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki (Orientalists), watalii, wawakilishi wa mataifa ya Kiislamu na wengineo ambao wote hao wanafanya safari za kwenda na kurudi katika nchi za Iran na Iraq hawana habari yoyote kuhusu suala hilo. Pasi na kumtafautisha yeyote, Mashia wanazipa heshima nafsi, damu, hadhi na mali za Waislamu wote, wawe Mashia au Masuni. Kila ulipotokea msiba wowote ule katika Ulimwengu wa Kiislamu, katika pahala na eneo lolote na kwa madhehebu yoyote, Shia wameshirikiana na Waislamu wenzao katika ghamu na majonzi yao. Shia hawajawahi katu kuliwekea mpaka kwenye Ulimwengu wa Mashia tu suala la udugu wa Kiislamu ambalo limeelezewa ndani ya Qur’ani na Suna; na katika jambo hilo hawajapambanua na kutafautisha kati ya Shia na Suni”.

 

Aidha katika sehemu ya mwisho ya juzuu ya tatu ya Kitabu cha Al-Ghadir na baada ya kuvifanyia upembuzi wa kiukosoaji vitabu vya wanazuoni wa karne zilizopita na wa sasa, Allamah Amini anasema: “Lengo letu sisi la kunukuu vitabu hivi na kuvifanyia upembuzi wa kiukosoaji ni kuutangazia Ulimwengu wa Kiislamu hatari inayoukabili, na kuwataka Waislamu waamke kwa kuelewa kwamba vitabu hivi vinailetea hatari kubwa zaidi jamii ya Kiislamu; na sababu ni kwamba vinauteteresha umoja wa Kiislamu na unaziparaganya safu za Waislamu. Kabla ya vitabu hivi, hakujawahi kuwepo kitu chochote kile ambacho kimevuruga safu za Waislamu, kuuvunja umoja wao na kuusambaratisha msingi wa udugu wa Kiislamu kiasi hiki”.

Katika utangulizi wa juzuu ya tano ya kitabu cha Al-Ghadir, ambao una anuani isemayo “Nadhariyatun Kariimah” kutokana na barua aliyoandikiwa kutoka Misri kutoa pongezi kuhusiana na kitabu cha Al-Ghadir, Alllamah Amini amebainisha kwa uwazi kabisa mtazamo na rai yake kuhusu umoja wa Kiislamu na kueleza kwamba: “Itikadi na rai kuhusu madhehebu ni jambo huru, na wala haiudhuru katu udugu wa Kiislamu ambao Qur’ani tukufu imeubainisha kwa maneno ‘hakika waumini wote ni ndugu’. Hata kama midahalo ya kielimu na mijadala ya masuala ya itikadi na madhehebu inaweza kufikia kilele cha kupamba moto, lakini hivi ndivyo ulivyokuwa mwenendo wa waliotangulia hasa masahaba na matabiina. Kwa hivyo licha ya hitilafu zote watakazokuwa nazo katika masuala ya msingi na madogomadogo, waalifu na waandishi katika kila pembe na kona ya Ulimwengu wa Kiislamu wana kitu kikuu kinachowaunganisha pamoja ambacho ni imani ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ndani ya mwili mmoja wa umma wa Kiislamu mna roho moja ndani yake ambayo ni Uislamu na kalima ya ikhlasi. Katika utangulizi wa juzuu ya nane ya kitabu cha Al-Ghadir, wenye kichwa cha maneno kisemacho “Al-Ghadir yuwahhidus-Sufufah Fil-malail-Islamiy”, Allamah Amini ameingia moja kwa moja kuzungumzia nafasi ya tukio la Ghadir katika kuleta umoja wa Kiislamu, ambapo anazipinga vikali tuhuma za watu wanaosema kuwa tukio la Ghadir linawafarakanisha zaidi Waislamu. Badala yake Allamah Amini anathibisha kuwa ni kinyume chake; Ghadir inaondoa sutafahamu nyingi zilizopo na kuwafanya Waislamu wazidi kukaribiana.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 21 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 22 ya mfululizo huu. Nakuageni basi na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags