Mar 14, 2018 08:24 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (22)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 22.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia nafasi ya umoja wa Kiislamu kwa mtazamo wa baadhi ya maulamaa na wanafikra wa Kishia na tukatupia jicho nafasi na mchango wa kitabu cha Al-Ghadir kilichoandikwa na Allamah Amini katika suala hilo. Katika mazungumzo yaliyopita tulieleza kuwa licha ya dhulma mbalimbali walizofanyiwa katika zama zote za historia, Waislamu wa madhehebu ya Shia siku zote wamekuwa wakitetea na kupigania umoja wa Waislamu; na katika zama zote, maulamaa na wanafikra wa Kishia wamefanya jitihada mbalimbali kwa kushirikiana na wanafikra wa Kisuni kuondoa baadhi ya mambo yanayochochea mifarakano na kulipa nguvu zaidi suala la umoja baina ya Mashia na Masuni. Nukta nyengine tuliyoizungumzia katika kipindi kilichopita ni kujaribu kujibu suali hili, kwamba hima iliyofanywa na Allamah Amini kuandika kitabu cha Al-Ghadir ilikuwa na lengo la kuimarisha umoja kati ya Shia na Suni au dhamira yake ilikuwa ni kuzidisha mpasuko na hitilafu baina yao? Baada ya kulifanyia uchambuzi suala hilo tulifikia hitimisho kuwa Allamah Amini anazivunja hoja za madai na tuhuma za watu wanaosema kuwa kitabu cha Al-Ghadir kinazidisha mfarakano baina ya Waislamu na kuthibitisha kuwa ni kinyume cha hivyo; Al-Ghadir kinaondoa suitafahamu nyingi na kuwafanya Waislamu wakaribiane zaidi.

Katika kipindi chetu cha leo na kuanzia sehemu hii ya 22 ya mfululizo huu tutazungumzia fikra na mitazamo ya Imam Khomeini (MA), akiwa ni mrekebishaji umma mkubwa wa Kishia katika Ulimwengu wa Kiislamu ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imam Khomeini (MA), kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin Asad Aabad amelishughulikia suala la umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa uzito mkubwa kwa upande wa fikra na nadharia na vilevile katika uga wa hatua za kivitendo. Isitoshe, Imam Khomeini (MA) alikuwa mmoja wa wanafikra wachache, ambaye alilipa umuhimu maalumu suala la kuunda utawala kwa ajili ya kufanikisha dhana ya umoja wa Kiislamu; na kwa mafanikio aliyopata katika kuunda utawala, alianzisha wimbi kubwa la vuguvugu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Hata katika zama za uongozi wake pia Imam Khomeini aliendelea kufuatilia utekelezaji wa dhana ya umoja na kutoa changamoto kali kwa watawala wa nchi za Kiislamu. Imam Khomeini (MA) ambaye aliweza kuithibitisha kivitendo ndoto na tarajio tukufu la kuunda utawala wa Kiislamu katika sehemu moja ya ardhi kubwa ya Ulimwengu wa Kiislamu, hakughafilika hata mara moja na dhana kuu ya kuunda Umma wa Kiislamu, kwa ajili ya kuasisi utawala wa ulimwengu mzima wa Kiislamu; na daima alikuwa akilipa umuhimu na kulitilia mkazo jambo hilo. Imani ya dhati aliyokuwa nayo Imam Khomeini kwa kadhia ya “umoja” sio tu ilimbadilisha kuwa shakhsia mtajika zaidi wa kimapinduzi wa Ulimwengu wa Kiislamu, lakini pia ilimfanya awe na nafasi maalumu na ya juu mbele ya harakati na madhehebu tofauti za Kiislamu.

 

Katika fikra za Imam Khomeini, umoja unajumuisha aina ya mwafaka unaotambulika na wa thamani ambao una chimbuko la kidini na kimaanawi; na mifano yake ya kimaadili na kimwenendo kwa upande wa nadharia na matendo imepangwa na kubainishwa ndani ya Kitabu kitukufu cha Qur’ani na Suna. Umoja wa aina hii unatokana na nishati ya kiupendo, hima na imani ya pande mbili baina ya watu na makundi ambapo mhimili mkuu wa sharia za dini huwa sababu ya wao kuwa na nguvu na wenzo kwao wa kuleta marekebisho, kupiga hatua za maendeleo na kuzuia ufisadi na uharibifu katika jamii. Katika ukurasa wa 309 wa kitabu cha Hadithi Arubaini, Imam Khomeini anasema: “Moja ya makusudio makubwa ya sharia za dini na manabii waadhamu, ambao mbali na wenyewe kuwa kusudio la kujitegemea na wenzo wa kuwezesha kufikia malengo makubwa na kuwa na nafasi kamili katika kujenga Jamii Timilifu, ni kuwa na Umoja wa Kalima na Umoja wa Itikadi na kuungana pamoja katika mambo yote na kuzuia uchupaji mipaka wa kidhalimu wa viranja wa wachupaji mipaka, ambao udhalimu wao ndio unaofisidi kizazi cha wanadamu na kuiharibu Jamii Timilifu. Na lengo hili kubwa, ambalo lina maslaha kwa jamii na kwa mtu binafsi, haliwezi kufikiwa isipokuwa kwa kuthibiti umoja mtukufu, kuungana, kupendana na kuwepo udugu, usafi wa nyoyo na mapenzi ya batini na dhahiri baina ya Waislamu. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini, kuungana na kuwa wamoja Waislamu chini ya mhimili wa dini tukufu ya Uislamu ndiyo siri ya nguvu na ushujaa usio wa kawaida waliokuwa nao Waislamu wa zama za mwanzoni mwa Uislamu; na anaizungumzia nukta hiyo kwa kusema: “Ikiwa Waislamu watakuwa nayo tena ile izza na adhama waliyokuwa nayo mwanzoni mwa Uislamu, wakaushika Uislamu na kalima ya umoja, wajue kwamba ni mshikamano huo chini ya mhimili wa Uislamu ndio uliopelekea kupatikana nguvu na ushujaa ule usio wa kawaida” (Loho ya Nuru, Juzuu ya 5, ukurasa wa 32).

Umoja wa Kiislamu

 

Katika kubainisha chanzo cha kutokuwepo msimamo na muelekeo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu, Imam Khomeini anataja sababu mbili muhimu na za msingi, mojawapo ikiwa ni: Kuwepo mpasuko baina ya watu na utawala na hitilafu kati ya watawala wa nchi za Kiislamu. Kuhusiana na jambo hilo anasema: “Sisi tunajua, Waislamu pia na serikali zote za nchi za Kiislamu, wote kwa jumla wanajua kwamba, yanayotusibu na yaliyotusibu yametokana na matatizo mawili: moja ni tatizo lililopo baina ya serikali zenyewe, ambazo kwa masikitiko hadi sasa hazijaweza kutatua tatizo hili… na tatizo la pili ni la baina ya serikali na wananchi, ambapo serikali zimeamiliana na wananchi kwa namna ambayo wananchi hawazipi msukumo na kuziunga mkono; serikali zinatingwa na matatizo mbalimbali na inapasa matatizo hayo yatatuliwe na wananchi”. (Loho ya Nuru, Juzuu ya 9, Ukurasa wa 546-547). Aidha anaashiria nafasi ya maajinabi na mabeberu wa dunia, kama sababu nyengine muhimu sana katika kuleta mpasuko baina ya Waislamu na kati ya nchi za Kiislamu. Kuhusiana na nukta hiyo anasema: Mfarakano uliopo kati ya nchi za Waislamu unatokana na ima usaliti wa viongozi wa Kiislamu au ujinga na kutokuwa kwao na uelewa…si suala la Usuni na Ushia; hakuna suala la Ukurdi na Ufarsi katika Uislamu; katika Uislamu, sisi sote ni ndugu na sote ni wamoja. Kundi moja katika Waislamu; katika Suni kuna tapo ni Hanafi na kuna tapo ni Akhbariyyun…haifai kushikilia masuala haya katika jamii ambayo, watu wote wanataka kuutumikia Uislamu na kuwepo kwa ajili ya Uislamu. Sisi sote ni ndugu na sote ni wamoja…hayo siyo sababu ya kutafautiana na kuhitilafiana. Haifai sisi kutafautiana au kuwapo mgongano kati yetu. Ndugu wa Shia na Suni wanapaswa kujiepusha na kila hitilafu na tofauti. Leo wanaonufaika na hitilafu baina yetu ni wale tu wasioamini madhehebu ya Shia wala wasioamini madhehebu ya Suni; wasioamini madhehebu ya Hanafi au madhehebu nyinginezo. Wao wanataka isiwepo hii wala ile; njia sahihi ya kufuata kwao wao ni kuchochea hitilafu baina ya madhehebu mbili hizi”.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 22 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 23 ya mfululizo huu. Nakuageni basi na kukutakieni kila la heri maishani.

Tags