Apr 21, 2018 10:31 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (42)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 42.

Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulieleza kwamba thamani na tunu za pamoja za kidini zilizopo baina ya Waislamu ni moja ya misingi muhimu ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Wakati nchi za kikoloni za Magharibi zilipobaini kuwa kwa kutumia mbinu za huko nyuma hasa za uingiliaji wa moja kwa moja hazitoweza kuingilia masuala ya nchi za Kiislamu na kusababisha utengano na mfarakano baina ya Waislamu, ziliamua kutumia nyenzo na mbinu mpya; muhimu zaidi kati ya hizo ikiwa ni ya hujuma za kiutamaduni. Katika hujuma hizo, silaha za kisasa za kivita sizo zilizowezesha kupata mafanikio na ushindi madola ya kikoloni, lakini fikra zilizopenyezwa ndani ya nchi za Kiislamu kupitia vyombo vya habari vya kimataifa ndizo zilizofungua mlango wa satua na ushawishi wa madola hayo. Ushawishi wa fikra hizo ambazo zilitokana pia na misingi imara ya akili na mantiki ulipelekea kujiri mageuzi na mgawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu. Hisia na radiamali zilizoonyeshwa na nchi za Kiislamu kwa fikra hizo zilikuwa katika moja ya hali tatu, ambazo ni kukubali kila kitu, kukataa kikamilifu au kutozikataa wala kuzikubali kikamilifu fikra hizo. Katika mazingira hayo Ulimwengu wa Kiislamu ulikumbwa na mpasuko na mgawanyiko uliosababishwa na jinsi mataifa ya Waislamu yalivyozipokea fikra hizo; kwa sababu harakati ya kati na kati ya utumiaji hekima na busara za Kiislamu ilikuwa na mori mdogo zaidi kulinganisha na mbili nyengine zilizokubali au kukataa kikamilifu fikra hizo.

 

Kinyume na dhana ya wachambuzi wengi waliokuwa wakiitakidi kuwa ukoloni wa kiutamaduni ni mtindo wa mwisho kabisa wa ukoloni duniani, ilipoingia karne ya ishirini na moja nchi za Kiislamu zilishuhudia nchi za Magharibi zikirudi tena kwa kutumia mitindo ileile ya awali ya Ukoloni sambamba na kuendeleza ukoloni wa kiutamaduni. Mashambulio na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Afghanistan na Iraq ambazo ni nchi mbili za Kiislamu ni kielelezo na ushahidi wa kubadilika tena mwenendo wa kikoloni wa madola hayo. Sambamba na mwamko wa Ulimwengu wa Kiislamu na msimamo uliochukuliwa kukabiliana na malengo ya kiutamaduni na kisiasa ya Magharibi; na baada ya hapo kuibuka mgogoro wa hali mbaya katika mfumo wa Ubepari, nchi za Ulaya ziliamua kuurejea tena mtindo wao awali wa kikoloni, yaani kujiingiza moja kwa moja katika nchi za Kiislamu, lengo likiwa ni kuzima wimbi la mwamko wa Ulimwengu wa Kiislamu na vilevile kuunasua mfumo wa Ubepari kwenye kinamasi cha mgogoro ulioukumba. Hatua hiyo, na hasa ya kuishambulia kijeshi Iraq ilikuwa na umuhimu wa pande kadhaa kwa nchi za Magharibi. Umuhimu wa kwanza ni kwamba kujiingiza moja kwa moja kijeshi Magharibi nchini humo kulikuwa kunakamilisha viungo vya mnyororo wa Mashariki ya Kati Kubwa uliokusudiwa kutengezwa na Marekani. Pili ni kwamba, kwa kuziuzia silaha na zana za kivita nchi za eneo hili viwanda vya utengezaji silaha huko Magharibi vilistawi. Na tatu ni kuwa nchi za Magharibi na hasa Marekani iliweza kuudhibiti mshipa mkuu wa uchumi wa dunia, yaani nishati ya mafuta.

Kufufua mizozo ya kimadhehebu katika nchi za Kiislamu na kukoleza cheche za moto wa hitilafu uliokuwa ukifukuta kwenye makumbi ni matokeo mengine muhimu na hatari pia ya uingiliaji wa moja kwa moja wa nchi za Magharibi katika Ulimwengu wa Kislamu. Kwa kweli kitu zilichoambulia nchi za Kiislamu katika uingiliaji wa nchi za Magharibi si chengine chochote zaidi ya mifarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu na kufufuliwa mizozo na malumbano ya kimadhehebu hususan ugomvi kati ya Shia na Suni. Kujitokeza harakati ya ukufurishaji, yaani utakfiri ni kielelezo na mfano halisi wa matokeo hayo, ambapo pasi na kuongeza chumvi inapasa tuseme kuwa harakati hiyo imezipiku harakati nyengine za kifikra na kisiasa katika zama zote za historia katika kuwasha na kueneza moto wa mifarakano baina ya Waislamu. Lakini suali linalohitaji kupatiwa jawabu makini na ya upembuzi ni je, kujitokeza na kupata nguvu harakati na magenge ya ukufurishaji, chimbuko na chanzo chake ni nje tu ya Ulimwengu wa Kiislamu? Tukifanya upembuzi yakinifu tutabaini kuwa kujitokeza kwa wimbi na harakati hiyo ni matunda na kielelezo dhahiri kabisa cha mfungamano wa sababu za ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu na nje ya ulimwengu huo katika kuleta mpasuko na mgawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu.

 

Kwa kuanzia tuitupie jicho harakati ya kifikra na kisiasa ya Utalibani, moja ya harakati muhimu zaidi za utakfiri ambayo imekuwa na taathira kubwa katika kuleta mgawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu. Harakati hii ni matunda ya mfungamano wenye nuhusi wa sababu za ndani na za nje ya Ulimwengu wa Kiislamu. Mtazamo wa kiuchambuzi juu ya suala hili unaonyesha ni jinsi gani ukata wa kiutamaduni na kiuchumi katika jamii za Kiislamu na ujinga na kutokuwa na ustahiki watawala wa nchi za Kiislamu kwa upande mmoja, na ulaji njama uliofanywa na maadui wa nje kwa upande mwengine, ulivyoweza kuuletea Ulimwengu wa Kiislamu hali mbaya zaidi ya misiba na maafa ya kiuchumi, kiusalama na kimataifa.

Jina la Taliban, likiwa ni kundi jipya la kifikra, kiitikadi na kisiasa na wakati huohuo la kijeshi lilisikika na kuonekana kwa mara ya kwanza mwaka 1994 katika ripoti zilizotolewa kuhusiana na matukio na mapigano yaliyojiri nchini Afghanistan. Mnamo wakati huo kundi hilo liliweza kuiteka pia miji ya Qandahar na Jalal Abad baada ya kutangulia kushika udhibiti wa baadhi ya maeneo ya mashariki na kusini mwa nchi hiyo yakiwemo ya Sang Hisar na njiapanda ya Spin Boldak. Mwaka 1995, wapiganaji wa Taliban walifanikiwa kusonga mbele kwa kasi katika maeneo mengine ya Afghanistan kama Herat na mikoa mingine kumi sambamba na kuuzingira mji mkuu Kabul. Ahmad Shah Masoud, Waziri wa Ulinzi wa serikali ya wakati huo iliyokuwa ikiongozwa na Burhanuddin Rabbani, aliweza kwa muda wa mwaka mmoja kuwazuia Taliban kusonga mbele na hivyo kuishia kwenye viunga vya mji mkuu huo wa Afghanistan; lakini baada ya hapo waliuteka mji wa Kabul na kujipanga na kujizatiti kwa lengo la kuyadhibiti maeneo mengine ya nchi hiyo hususan ya kaskazini likiwemo la Mazar Sharif.

Wasikilizaji wapenzi, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini kuwa mtakuja kujiunga nami tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo katika sehemu nyengine ya mfululizo huu. Nakuageni basi, huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags