May 11, 2018 03:02 UTC
  • Iran yazidi kujiimarisha katika teknolojia ya nano

Katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani na leo tutaanza na mafanikio ya wanasayansi Wairani katika uga wa teknolojia ya nano

Hivi karibuni katika uga wa teknolojia ya nano, wanasayansi Wairani waliweza kupata mafanikio mapya. Katika makala yetu ya leo tutaangazia mafanikio hayo mapya ya wanasayansi Wairani. Kwanza tunakumbusha kuwa, Nano ni teknolojia ya kisasa inayohusu matumizi ya vitu vidogo sana na miundo yake ambayo inapimwa kuwa kati ya nanomita 1-100. Asili ya Nano ni nanomita ambayo ni kipimo cha sehemu ya bilioni moja ya mita. Hii inamaanisha vitu ambavyo ni vikubwa kuliko atomu na vidogo mara 1000 kuliko upana wa unywele.

Teknolojia ya nano nchini Iran imestawi sana, na hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambulika duniani kama miongoni mwa nchi zilizostawi sana katika uga wa teknolojia ya nano.

Hivi sasa Iran inauza bidhaa zake za nano katika nchi muhimu za dunia kama vile Australia, Malaysia, Russia, Ujerumani, Uhispania, Italia, Uturuki n.k.

Vipuri vya magari vya teknolojia ya Nano

Watafiti Wairani katika uga wa teknolojia ya nano hivi karibuni walifanikiwa kupunguza gharama zinazotumika kuunda vipuri vya mashine kadhaa hasa vya magari. Katika mradi wa pamoja, wanasayansi wa vyuo vikuu vya Semnan na Shiraz wameunda vipuri kwa kutumia teknolojia ya nano ambavyo vinaweza kutumika katika sekta za viwanda vya magari, na kwa msingi huo kupunguza uzito wa kipuri kinachoundwa. Hali kadhalika mbali na kupunguza uzito, pia vipuri hivyo vinapunguza kiwango cha mafuta yanayotumika katika gari. Vipuri hivyo hadi sasa vimezalishwa katika maabara na bado kuna vizingiti vya kuzalishwa kwa wingi kiviwanda.

Chembe za nano 

Wasimamizi wa mradi huo, wamejitahidi kupunguza gharama katika utengenezaji vipuri ili hatimaye bei ya kipuri iwe ya chini sambamba na kupunguza gharama za mafuta ya petroli au umeme unaotumika katika gari. Hali kadhalika nukta muhimu iliyozingatiwa katika uundwaji wa vipuri kama hivyo ni kuhakikisha kuwa ni vya viwango vya juu kabisa.

Vifaa vya kieletkroniki vyahifadhiwa kwa teknolojia ya nano

Hivi karibuni watafiti wa Chuo Kikuu cha Tarbiat Modarres cha Tehran wamefanikiwa kutengeneza katika maabara aina ya vifuniko vya nano kwa kutumia mada ya chuma na nikeli ambayo huweza kufunuka vizuri vifaa vya kieletrononiki na kuviwezesha kustahamili pigo. Mada ya chuma na nikeli kwa kawaida hutumika katika vifaa vya kielektroniki kama vile kinasa sauti, hifadhi za kompyuta, vifaa vya kurushia matangazo, saa za mkononi n.k. Wakati mada iliyotumika kufunika vifaa hivyo vya kielektroniki inapoharibika,  basi chombo husika nacho pia huharibika.

Teknolojia ya nano katika kulinda vifaa vya kielektroniki

Moja ya mbinu za kulinda vifaa vya kielektroniki ili visiharibike vinapoanguka n.k ni kutumia mada maalumu za  kuvifunika. Katika uvumbuzi huo wa watafiti Wairani,  wameweza kubuni  mada ya chuma na nikeli yenye upana wa chini ya nanomita 100 kulinda vifaa vya kielektroniki.  Moja ya nukta za kipekee katika uvumbuzi huo wa watafiti Wairani ni kuwa mada waliyoweza kuunda kwa kutumia teknolojia ya nano ina uwezo bora zaidi wa kulinda vifaa vya kielektorniki na hivyo kuongeza muda wa kutumiwa vifaa hivyo kutokana na uwezo wa juu wa kustahamili iwapo vitaanguka, kugongwa n.k.

Teknolojia ya VR katika kutibu ubongo

Hivi karibuni msomi Muirani, ameweza kutumia teknolojia ya Virtual Reality au VR  ambayo kwa sekunde 60 hupata eneo ambalo limepata mtikiso katika ubongo ambao husababisha jeraha ambalo hupelekea ubongo kushindwa kufanya kazi kwa muda. Tatizo hilo la ubongo kwa Kiingereza linajulikana kama concussion.

Kwa kifupi hapa tunaweza kusema teknolojia ya Virtual Reality au VR ni teknolojia inayohusisha kuvaa kisanduku kilicho na matundu mawili usawa wa macho au headset, kupitia matundu hayo unaweza kuangalia sinema, kucheza michezo ya video na mambo mengine mengi kana kwamba uko katika ulimwengu halisi. Baadhi wanasema  VR ni teknolojia inayokuwezesha kuota ndoto zako ukiwa macho.

Sasa turejee katika mada yetu. Kwa kawaida madaktari hutumia wakati mwingi na huwa na kibarua kigumu wakati wa kuchunguza ubongo wa mtu aliyepata pigo katika ubongo. Kwa kawaida madaktari humtaka mgonjwa ahifadhi sentensi au huchunguza harakati zake za macho ili kubaini tatizo hilo la ubongo na hivyo huchukua muda mrefu na wakati mwingine matokeo huwa  si sahihi.

Headset ya VR

Ili kukabiliana na tatizo hilo la ubongo,  mwanasayansi Muirani, Jamshid Ghajar, anayefanya kazi na shirika la teknolojia ya ubongo la Synch Think la Marekani, akiwa na timu yake, wamefanikiwa kubuni njia ya kutibu tatizo la ubongo kupoteza fahamu kwa muda kwa kutumia teknolojia ya kufuatilia harakati za macho.

Ghajar ambaye ni mpasuaji  wa ubongo au neurosurgeon, ametumia teknolojia ambayo msingi wake ulikuwa ni utafiti wa kliniki ambao utaleta mabadiliko makubwa kutibu tatizo hilo la ubongo linalojulikana kama concussion kwa lugha ya Kiingereza.

Mbinu iliyobuniwa inajulikana kama teknolojia ya EYE-SYNC ambapo mgonjwa hutumia headset ya VR ambayo hufuatilia harakati za macho na kuripoti tatizo la ubongo katika kipindi cha sekunde 60. Mafanikio hayo yameidhinishwa na Shirika la Dawa na Chakula nchini Marekani (FDA) na sasa teknolojia hiyo tayari inatumika katika hospitali na shule ambazo hufunza soka ya Marekani. Shule hizo zimechaguliwa kwa sababu katika soka ya Marekani wachezaji hupata pigo la kichwa wakati wa mchezo.

Mashine ya kuangamiza seli za saratani kwenye damu

Wiki hii wanasayansi Wairani katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff cha Tehran wametangaza kuunda mashine ambayo ina uwezo wa kupata seli za donda la saratani ambazo huzunguka katika damu ya wagonjwa wa saratani. Seli zinazozunguka mwili mzima za donda la saratani maarufu kama CTCs ni seli ambazo zimejiondoa katika donda kuu la saratani ambalo liko sehemu maalumu mwilini na kuenea katika maeneo mengine ya mwili kupitia mishipa ya damu. Seli hizo ca CTCs kimsingi ni kama mbegu ambazo hueneza madonda mengine ya saratani katika viungo muhimu vya mwili na hivyo kuibua mchakato ambao hupelekea idadi kubwa ya wanaougua saratani kupoteza maisha. 

Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Shariff cha Tehran

Mmoja kati ya wanasayansi Wairani katika mradi huo amesema wakati mashine waliyovumbua inapowekwa katika chombo maalumu cha mzunguko, damu huingia katika masheni hiyo kwa kutumia mashinepewa au centrifuge na baada ya kupitia katika awamu mbili za kutenganishwa, seli za saratani huondolewa katika mfumo wa damu. Mbinu hii ya utenganishaji hutekelezwa na uga sumaku na mashinepewa kwa pamoja.

Mkutano wa ubunifu barani Afrika

Na Mkutano wa Kilele wa Ubunifu Barani Afrika maarufu kama The Africa Innovation Summit (AIS II), umepangwa kufanyika Juni 6-18 mwaka huu katika mji mkuu wa Rwanda Kigali. Wanasayansi na wabunifu barani Afrika wametakiwa kuwasilisha miradi yao ambayo inaweza kuwa na suluhisho kwa changamoto za  bara hilo kaatika sekta za nishati, maji safi, usalama wa chakula, mifumo ya afya na utawala. Mkutano huo unatazamiwa kuwaleta pamoja viongozi wa nchi, mawaziri, wakuu wa mashirika, wabunifu, wawekezaji, wasomi, watafiti na wataalamu wa sayansi na teknolojia kwa lengo la kuimarisha mazingira ya ustawi endelevu wa bara hilo.