Aug 08, 2018 04:07 UTC
  • Jumatano,Agosti 8, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 25 Dhulqaada 1439 Hijria mwafaka na tarehe 8 Agosti mwaka 2018.

Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita Nabii Muhammad (saw) akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja aliondoka Madina na kuelekea Makka kwa ajili ya kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ya al Kaaba. Tangu alipohamia mjini Madina, Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kwa ajili ya kuzuru al Kaaba, lakini ni mara mbili tu ndizo alizofanikiwa kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada hiyo kwa njia sahihi. Wakati akirejea Madina, Mtume Muhammad (saw) alifika katika eneo la Ghadir Khum na hapo akawakusanya masahaba zake na kwa amri ya Mola wake akamtangaza Imam Ali bin Abi Twalib kuwa Khalifa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hajjatul Wadaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Mtukufu aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Siku kama ya leo miaka 2351 iliyopita sawa na tarehe 8 Agosti 333 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, ilianza kazi ya ujenzi wa mji wa Alexandria nchini Misri, ambao leo hii unahesabiwa kuwa moja kati ya bandari muhimu kusini mwa Bahari ya Mediterranean. Ujenzi huo ulifanyika kwa amri ya Alexander Macedon huko kaskazini mwa Misri.

Alexandria

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita mwafaka na tarehe 17 Mordad 1371 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu duniani, akiwa na umri wa miaka 96. Mwanachuoni huyo mashuhuri alizaliwa katika mji wa Khoui ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na akiwa katika umri wa ubarobaro, alifuatana na baba yake mjini Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Katika zama za umarjaa wake, Ayatullahil Udhma al Khoui alitoa fatwa inayosisitiza udharura wa kuilinda Palestina na kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu. Alimu huyo mkubwa ameacha vitabu vingi vikiwemo 'Jawaahirul Usuul', 'Muntakhabu Rasaail', 'al Bayaan Fii Tafsiiril Qurani' na "Misbahul Faqaha".

Ayatullahil Udhma Alhaj Sayyid Abul Qassim al Mussawi al Khoui

Na miaka 20 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 8 Agosti 1998, wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Mazar Sharif ulioko kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji huo, wanamgambo wa Taleban waliushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji huo na kuwauwa shahidi wanadiplomasia 8 wa Kiirani na mwandishi mmoja wa habari. Kundi la Taliban liliasisiwa mwaka 1994 kwa ufadhili na usaidizi wa Marekani na Pakistan na kufanikiwa kuikalia sehemu kubwa ya ardhi ya Afghanistan.

Mazar Sharif

 

Tags