Sep 14, 2018 04:23 UTC
  • Ruwaza Njema (1)

(Kumfuata al-Mustafa katika kikao chake)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni Kusikiliza sehemu ya kwanza ya kipindi cha Ruwaza Njema ambacho kinatutaka sisi Waislamu kufuata akhlaqi na tabia njema za mbora wa viumbe na bwana wa tabia tukufu, Muhammad al-Mustafa (saw). Hivyo kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni. Wapenzi wasikilizaji, mtu wa kwanza kushuhudia utukufu na ubora wa tabia za Mtume Muhamad (saw) ni Mwenyezi Mungu mwenyewe ambapo anasema katika Aya ya nne ya Surat al-Qalam anapomzungumzia Bwana wa Viumbe wake: Na hakika wewe una tabia tukufu.

Hivyo ni nani mwingine ambaye amesifiwa kwa sifa hizi tukufu na Mwenyezi Mungu Muumba wa mbingu na ardhi, anayeweza kuchukuliwa kuwa mfano bora na ruwaza njema zaidi kwa walimwengu isipokuwa Mtume Mtukufu (saw)?

*********

Wapenzi wasikilizaji, je, Mtume Mtukufu (as) alikuwa akionyesha tabia zipi katika vikao vyake ili na sisi tupate kufuata tabia zake hizo njema tunapokuwa kwenye vikao vyetu? Swali hili linajibiwa vizuri na mtu aliyekuwa karibu zaidi na Mtume Mtukufu (saw), ndugu, nafsi na wasii wake, al-Imam Amir al-Mu'mineen Ali bin Abi Talib (as). Imepokelewa katika kitabu cha Uyun Akbar ar-Ridhwa cha Sheikh Swadouq kutoka kwa Imam wa Nane katika kizazi cha Mtukufu Mtume (as) kutoka kwa Imam Hussein (as) kwamba alimuuliza baba yake ambaye ni al-Imam Ali al-Murtadha kuhusiana na tabia za Mtume Mtukufu (saw) alipokuwa akiketi kwenye majaalis, yaani vikao naye akasema (as): 'Mtume (saw) alikuwa haketi wala kusimama kwenye kikao ila kwa kumdhikiri (kumtukuza) Mwenyezi Mugu Mtukufu na wala hakuwa akijitengea sehemu maalumu kwenye vikao na akiwakataza wengine kufanya hivyo…… Alipokuwa akiingia kwenye kikao alikuwa akiketi sehemu ambayo watu walikuwa wamemalizikia kuketi na kuamuru watu wengine wafanye hivyo. Alikuwa akimpa kila aliyeketi kwenye kikao haki yake ili asihisi kuwa kulikuwa na mtu mwingine aliyekuwa bora zaidi kumliko yeye mbele ya Mtume. Kila mtu aliyekuwa akiketi naye au kufuatilia jambo fulani kutoka kwake, Mtume (saw) alikuwa akionyesha subira kubwa hadi aliyefika mbele yake mwenyewe alipoamua kuondoka. Alikuwa hamuachi hivihivi aliyekuwa amefika mbele yake kumuomba haja fulani ila alimtekelezea haja hiyo au kumwambia maneno ya kumfariji.'

 

Tunaendeea kusikiliza maneneo ya kuvutia ya Imam Ali al-Murtadha (as) akisifia tabia njema na tukufu ya ndugu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipokuwa akishiriki vikao tofauti ambapo anasifu tabia hizo njema za Mbora wa Viumbe kwa kusema: 'Kila mtu alinufaika na utu pamoja na tabia zake njema na hivyo kuwa mfano wa baba mwenye huruma kwao. Kuhusiana na suala la haki, kila mtu alikuwa sawa mbele yake. Vikao vyake vilikuwa ni vikao vya huruma, haya, ukweli na ulindaji amana. Hakuna makelele yaliyokuwa yakipigwa kwenye vikao vyake wala watu kuvunjiwa heshima katika vikao hivyo. Mitelezo na siri za watu hazikuwa zikifichuliwa katika vikao hivyo. Watu wote walikuwa ni sawa, wenye mshikamano na wanyenyekevu kwa msingi wa takwa. Walikuwa wakiwaheshimu watu wazima, kuwapenda watoto, kuwafadhilisha wahitaji juu ya nafsi zao na kuwapa hifadhi wageni wasiokuwa na wenyeji.'

**********

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe sote taufiki ya kuweza kumfuata kikweli Bwana wa Mitume (saw) katika harakati na mienendo yake yote maishani, Allahumma Amin.

Na kufikia hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki kwa juma hili. Basi hadi tutakapokutana katika kipindi kingine cha Ruwaza Njema panapo majaaliwa, tunakuogeni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.