Jumamosi, 6 Oktoba, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 26 Mfunguo Nne Muharram 1440 Hijria sawa na tarehe 6 Oktoba 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1376 iliyopita, mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa kwa mabomu baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala mal'uni wa kizazi cha Bani Umayyah, Yazid bin Muawiyya. Baada ya kumuua shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika medani ya Karbala na Watu wa Nyumba ya Mtume wakachukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa mabomu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 417 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika Hawza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari. ***
Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel vilianza. Katika siku hiyo, jeshi la Misri lilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu huko katika mfereji wa Suez na kufanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai baada ya kuvunja kikosi cha ulinzi cha mstari wa mbele cha utawala wa Kizayuni . Vikosi vya Misri na Syria vililisababishia hasara kubwa jeshi la Israel katika vita hivyo ambapo ndege nyingi za utawala wa Kizayuni ziliangamizwa. ***
Miaka 38 iliyopita sawa na tarehe 14 Mehr 1359 Hijria Shamsia, Bandari ya Aqabah ya Jordan ilikabidhiwa kwa Iraq kwa ajili ya kuandaa suhula za vita dhidi ya Iran. Sambamba na kuanza vita vya kulazimishwa Iran na Iraq, mfalme Hussein wa wakati huo wa Jordan alifanya safari ya siku moja huko Iraq na kutangaza kikamilifu uungaji mkono wake kwa dikteta Saddam Hussein. ***
Na siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri aliuawa na maafisa kadhaa wa kundi moja la wanamapambano wa Kiislamu wa Misri lililojulikana kwa jina la al-Jihad. Sadat aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano maovu ya Camp David mwaka 1978 na utawala wa Kizayuni wa Israel na akautambua rasmi utawala huo ghasibu na haramu. Kwa kitendo hicho Anwar Sadat alisaliti malengo ya Waislamu na Waarabu. Hatua hiyo ya Anwar Sadat ilipelekea kutengwa Misri miongoni mwa nchi za Kiislamu. Sababu hiyo iliyapelekea makundi ya Waislamu na wanamapambano wa Misri kumuuwa Sadat, ambaye walimuona kuwa ni msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala wa maghasibu wanaoikalia kwa mabavu Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Kiongozi wa mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri. ***