Nov 03, 2018 10:33 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (68)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 68.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mnakumbuka katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba wanajeshi vamizi wa Saudi Arabia waliopata baraka kamili za Aal Khalifa na serikali ya Marekani, na kwa kutumia mwavuli wa vikosi vya Ngao ya Kisiwa, waliingia nchini Bahrain na kuendeleza kazi iliyoanzishwa na askari wa utawala wa Aal Khalifa ya kuwakandamiza wananchi wa Bahrain.

Lakini uwepo wa kivamizi wa majeshi ya utawala wa Aal Saud nchini Bahrain kwa lengo la kuuhami na kuulinda utawala wa Aal Khalifa si tu haukuweza kurejesha uthabiti kwa hali ya kuyumbayumba ya utawala huo lakini pia ulishadidisha na kukoleza moto wa mapambano ya wananchi wa Bahrain na kuzidisha ghadhabu na chuki za wananchi hao dhidi ya utawala huo wa kiimla. Kutokubali utawala wa Aal Khalifa kuridhia matakwa halali na ya kisheria ya wananchi yaliyokuwa yakipiganiwa kwa njia za amani na badala yake kushadidisha hatua zake kandamizi dhidi ya wapinzani ikiwemo kutumia majeshi ajinabi kuzima sauti za malalamiko hayo ya umma viliubadilisha mkondo wa harakati ya wapinzani ya kupigania marekebisho na mageuzi na kulifanya suala la kuangushwa utawala kuwa takwa kuu la wananchi.

Kwa muktadha huo, maandamano ya mwanzo ya waungaji mkono wa harakati ya uasi kwa jina la "kimbunga cha uasi" dhidi ya utawala wa Aal Khalifa yalifanyika tarehe 14 Agosti mwaka 2013 katika maeneo tofauti ya Bahrain. Katika maandamano hayo yaliyosadifiana na maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Bahrain, waungaji mkono wa harakati hiyo ya uasi walitoa miito ya shime kama "utawala uangushwe" wakitilia mkazo haja ya kuamuliwa hatima na mustakabali wa nchi hiyo na Wabahraini wenyewe. Baada ya umma kuhamasika na kuanzishwa uasi wa kiraia na Harakati ya Uasi, askari wa utawala wa Aal Khalifa walichukua hatua kali za usalama nchini kote; na ili kuwakandamiza wananchi, walitumia risasi za marisawa na gesi ya sumu kiasi cha kusababisha waandamanaji kadhaa kupaliwa na pumzi na kushindwa kupumua.

 

Harakati ya uasi wa umma nchini Bahrain iliundwa kufuatia ongezeko la hatua kandamizi za utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi na kwa lengo la kupigania uhuru na demokrasia. Kwa mujibu wa taarifa za vyama na jumuiya za upinzani nchini Bahrain, tangu lilipoanza vuguvugu la maandamano ya amani ya upinzani wa umma tarehe 14 Februari mwaka 2011, askari wa utawala wa Aal Khalifa wameua shahidi mamia ya watu, wamewajeruhi zaidi ya elfu kumi, wamewaweka kizuizini watu wasiopungua 2,900 na kuwaachisha kazi wafanyakazi wanaokaribia elfu moja kwa sababu ya kushiriki kwenye maandamano hayo ya amani.

Lakini si hayo tu, bunge la Bahrain limechukua hatua ya kuifanyia mabadiliko sheria ya mikusanyiko na maandamano. Kwa mujibu wa sheria mpya iliyopitishwa na bunge hilo, ni marufuku kukusanyika na kufanya maandamano ya aina yoyote katika mji mkuu wa nchi hiyo Manama; na watu watakaoandaa au kushiriki maandamano yatakayofanywa katika mji huo watanyang'anywa uraia wao. Kufuatia kupitishwa sheria hiyo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alikosoa vikali hatua hiyo ya bunge la Bahrain na kueleza kupitia taarifa kwamba: "mabadiliko ya sheria ambayo bunge la Bahrain imeyafanya kuhusiana na mikusanyiko, na kwa kisingizio cha kuilinda jamii na harakati za kigaidi yana taathira hasi kwa hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo." Mbali na taarifa hiyo kuashiria sheria ya kuvuliwa uraia wale watakaoandaa na watakaoshiriki katika maandamano yatakayofanywa katika mji wa Manama, ilisisitiza pia kwamba uraia ni haki ya msingi ambayo imetiliwa mkazo kwenye kifungu cha 15 cha haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa.

Kuvuliwa uraia raia wa Bahrain ni mkakati unaokamilisha mpango na stratejia ya kuwapatia uraia wa nchi hiyo raia wa kigeni na ni moja ya mikakati muhimu zaidi ambayo imekuwa ikifuatiliwa kutekelezwa na utawala wa Aal Khalifa. Kwa kuweka sheria hiyo, Bahrain imeshika nafasi ya kwanza kati ya nchi za Kiarabu na hata kati ya nchi zote duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya raia waliofutiwa uraia. Kwa kuzingatia utukufu wa haki ya uraia, kitendo cha kumnyang'anya mtu haki yake hiyo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu.

 

Kuhusu kiwango cha ukiukaji wa haki za binadamu na haki za kiraia unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa kupitia utumiaji mkakati wa kidhalimu wa kuwavua uraia wapinzani wa utawala huo, Nidhal Aal Salman, wa kituo cha haki za binadamu nchini Bahrain amesema, tangu mwaka 2012 hadi sasa raia wanaokaribia elfu moja wamevuliwa uraia. Katika mwendelezo wa sera hiyo, utawala wa Aal Khalifa kupitia wizara yake ya mambo ya ndani umemvua uraia pia Sheikh Issa Ahmad Qassem, kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo kwa tuhuma eti za kueneza hisia za kikoo na za kuleta fitna katika jamii. Hatua hiyo ya utawala wa Bahrain ambayo iliungwa mkono na utawala wa Aal Saud, kwa upande mmoja ilizidi kuweka wazi sera za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa na waungaji mkono wake; na kwa upande mwengine kuzidisha mfarakano, mpasuko na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Sababu ni kwamba badala ya utawala wa Aal Khalifa kutekeleza matakwa halali na ya kisheria yanayopiganiwa kwa njia za amani na watu wake, umeamua kuelekeza kidole cha tuhuma kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba eti inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Ukweli ni kwamba licha ya mafungamano makubwa ya kidini, kimadhehebu na kiutamaduni yaliyopo baina ya nchi mbili, Iran inakanusha kuingilia kwa namna yoyote ile masuala ya ndani ya Bahrain. Kwa mtazamo wa Iran, serikali ya Bahrain inapaswa izuie uingiliaji wa madola ajinabi hususan Saudi Arabia katika masuala yake ya ndani sambamba na kuzitambua haki za wazi na za kisheria za wananchi wake ili kuandaa mazingira ya kuuzima moto wa malalamiko ya ndani na kuepusha kuzuka cheche za fitna ya hitilafu ndani ya mataifa ya Kiislamu.

Wakati huohuo kutokana na uhusiano wa kistratejia uliopo baina ya Marekani na Bahrain hususan kwa sababu ya kuwepo manowari ya tano ya Washington kwenye maji ya nchi hiyo, Marekani inaunga mkono sera za ukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa na muungaji mkono wake, yaani Saudi Arabia. Viongozi wa Washington wametupilia mbali madai yao yote ya kuguswa na demokrasia na haki za binadamu na kuamua kufumbia macho jinai zinazofanywa na Aal Khalifa huku wakishangiria kushadidi kwa mfarakano na uhasama kati ya nchi za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, kama tulivyoona, Saudi Arabia imekuwa mstari wa mbele katika mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen ya kutaka kuiangusha serikali inayoungwa mkono na wananchi na katika kukandamiza upinzani wa kiraia na maandamano ya amani ya wananchi wa Bahrain. Lakini ajabu ni kwamba badala ya kutoa jibu kwa fikra za waliowengi katika Ulimwengu wa Kiislamu kila mara imekuwa ikiituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba eti inaingilia masuala yake ya ndani na kuunga mkono wapinzani wa nchi hiyo. Inapasa tuelewe kwamba Mwamko wa Kiislamu maana yake si vuguvugu la kisiasa pekee dhidi ya watawala madikteta, lakini sehemu moja ya mwamko huo ni kupata uelewa wa sababu zilizopelekea kutokea utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu na hasa kuhusu namna nchi zenyewe za Kiislamu zilivyochangia kujitokeza kwa hali hiyo. Ni matumaini yangu kwamba kipindi chetu cha leo kimeweza kutoa mwanga juu ya suala hilo. Basi hadi wiki ijayo inshallah katika sehemu ya 69 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu, nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani…/

 

Tags