Nov 03, 2018 11:30 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (131)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu. Kama tulivyoashiria katika vipindi vyetu vilivyotangulia, kipindi hiki hujadili maudhuui mbalimbali za kijamii, kimaadili, kidini na kadhalika na kukunukulieni hadithi zinazohusiana na maudhui hizo kutoka kwa Bwana Mtume SAW na Maimamu watoharifu AS.

Kipindi chetu kilichopita kilijadili suala la kunong'ona yenye maana ya kusema kwa sauti ndogo na ya chini inayosikika tu na mtu aliye karibu nawe. Tulisema kuwa, Uislamu umeruhusu unong'onezaji na kunong'onezana watu kwa namna ambayo, hatua hiyo ilinde na kuchunga hisia za watu wengine na hatua hiyo isije kupelekea kutokea mifarakano na hitilafu baina ya watu. Aidha tulieleza kwamba, moja ya sababu za kukatazwa kumnong'oneza mtu kitu masikioni hali ya kuwa kuna mtu mwingine wa tatu ni kwamba, kitendo hicho kikawaida kinaweza kuleta dhana na fikra nyingine mbaya.

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemuu ya 131 ya mfululizo huu kitazungumzia mawaidha, waadhi au nasaha ambayo ni miongoni mwa mambo ambayo hutimia kwa kuutumia ulimi. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili muweze kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

*********

Waadhi, mawaidha au nasaha ni hitajio la kimaumbile kwa kila mwanadamu. Yumkini mtu akawa hana haja ya mafundisho ya watu wengine, lakini katu hakuna mtu ambaye si mwenye kuhitajia waadhi na nasaha au mausia. Hata wasomi na wanazuoni wakubwa, waja wema na maulama kuna wakati ni wenye kuhitajia nasaha, amawaidha na waadhi. Mtume SAW anazungumza uhusiano wake na Malaika wa Wahyi Jibril AS kwa kusema: Kila mara Jibril alipokuwa akinijia alikuwa akiniwaidhia na kuninasihi. Aidha Mtume SAW na Maimamu watoharifu AS walikuwa wakitumia mbinu hii kwa watu wao wa karibu hususan kwa ajili ya masahaba zao wa karibu.

Inasimuliwa kwamba, siku moja Imam Ali bin Abi Twalib AS alikuwa safarini na mmoja wa masahaba zake, kisha akamwambia sahaba wake yule: Niwaidhi na kuninasihi! Bwana yule kwa mshangao akamwambia Imam Ali AS, mtu kama mimi nikunasihi wewe? Imam Ali AS kama alivyosema Mtume SAW katika hadithi yake mashuhuri: Mimi ni mji wa elimu na Ali ni mlango wake, akamjibu Bwana yule kwa kumwambia: Ndio! Athari inayopatikana katika kusikiliza nasaha na mawaidha, haipatikani katika kujua na kufahamuu kitu.

Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume SAW katika aya ya 125 ya Surat an-Nahl:

Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anamtaka Mtume SAW awalinganie watu katika njia ya Allah kwa hekima, njia nzuri na mawaidha mema. Mawaidha ni kuzitumia hisia za wanadamu, kwani pindi hisia za zinapochochewa kwa njia sahihi zinaweza kukusanya na kuvutia watu wengi. Tab'an, mawaidha hayo yanapokuwa mema, yaani yasiyo na aina yoyote ile ya  uchafu kama kuteza nguvuu, kutwisha, kushinikiza, kulazimisha, kutumia mabavu, yasiyo na malengo maalumu na ambayo ndani yake hakuna udhalilishaji na udunishaji huwa na athari chanya na nzuri zaidi. Kinyume na hivyo, huwa na natija hasi ambayo ni uasi na ushindani usio na maana. Kwa msingi huo, mawaidha huwa na natija nzuri na kuleta mabadiliko katika moyo au nyoyo za watu wakati yanapochanganyika na nia njema, uzungumzaji mzuri ulioambatana na usafi na uzuri.

 

Imam Ali bin Abi Twalib AS akiwa baba mwenye huruma, anayeguswa na wanawe na mwenye kuwatakia kheri wanawe anasema katika Najah al-Balagha katika barua yake ya 31 kwamba:

Mwanangu kipenzi! Hakuna wakati mimi nilizembea katika kukuwaidhi na kukunasihi. Mwanangu kipenzi! Wewe daima unafikiria kheri na saada yako na mimi pia kupitia mapenzi ya baba ninafikiria mafanikio na wokozi wako."

Katika wasia huu ambao wenyewe ni mawaidha, Imam daima anamtaja mwanawe kwa sifa ya 'kipenzi' ili huba na mapenzi ya hali ya juu yaliyochanganyika na nia njema yadhihirike katika mawaidha. Kwa hakika mawaidha licha ya sifa zote yaliyonazo, lakini huwa na taathira matulubu na inayostahiki pale mtoa waadhi au anayenasihi anapokuwa na imani ya moyo juu ya kile anachokisema na awe ni mwenye kuikifanyia kazi kile anachokiwaidhi na si kutamka tu kwa ulimi na kinywa.

Kwa maana kwamba, mbali na mwenye kunasihi au kuuwaidhi kukumbusha jambo husika kwa ulimi anapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika amali na matendo. Kwani kama mnasihiwa au anayewaidhiwa ataona kuwa mwenendo wa msemaji unapingana na maneno yake, hawezi kuyapokea na kuyakubali maneno ya mtoa waadhi.

Imam Ja’afar bin Muhammad al-Swadiq AS anasema akibainisha hilo kwamba: Kila wakati alimu asipoifanyia kazi elimu yake, nasaha zake huteleza katika nyoyo kama matone ya mvua yanavyodondoka na kuteleza juu sehemu safi.

Kimsingi ni kuwa, taathira ya mawaidha na nasaha inafungamana na kiwango cha imani na uaminifu wa msikiaji kwa mzungumzaji. Kadiri kiwango cha uratibu na uwiano baina ya matendo ya mtoaji waadhi na nasaha na maneno yake kinavyokuwa kidogo, vivyo hivyo taathira yake kwa anayehutubiwa hupungua na kuwa kidogo.

Imam Hadi al Naqi AS

 

Kwa hakika unapokusudia kumnasihi mtu, basi unapaswa kufanya hivyo kwa njia ya siri na mbali na macho na masikio ya watu, kwani kwa njia hiyo hupokelewa vizuri na huondoa uwezekano wa nasaha hizo kuibua uasi na upinzani. Hasa kwa vijana na mabarobaro ambao wako wana unyeti maalumu kwa nasaha na mawaidha. Hata hivyo katika mawaidha na nasaha ambazo zinatolewa jumla na katika mkusanyiko wa watu, hakuna mushkili kwani katika muhadhara kama huo mawaidha huwa hayamlengi mtu maalumu.

Imam Ali an-Naqi al-Hadi AS anasema: Kila ambaye atamuaidhi na kumnasihi ndugu yake muumini kwa siri amemtengeneza, na kama anamuaidhi na kumuusia kwa dhahiri na (mbele ya kadamanasi), thamani yake itapungua.. Nukta nyingine ni kwamba, katika kunasihi na kuwaidhi, kuna haja ya kutumika njia ya polepole na ya hatua kwa hatua kwenda mbele sambamba na upole na ulaini wakati wa kuzungumza na kujiepusha na vitisho. Kwani kama nasaha na mawaidha hayataendana na ufahamu na udiriki wa anayewaidhiwa, aghalabu huwa na natija kinyume.

Kwa hakika kutoa nasaha na kumnasihi mtu kutokana na jambo baya au kumzindua mtu kutokana na hatari ya upotofu inayomkabili mbele yake, kuna umuhimu kiasi kwamba, Imam Muhammad Baqir (as) anawataja kuwa ni wafanya hiana na usaliti watu ambao wanajizuia kuwanasihi watu wengine. Anasema: "Endapo wasomi wataficha nasaha zao, basi watakuwa ni wenye kufanya khiana."

Wapenzi wasikilizaji, Nukta muhimu ni kuwa, mtoaji nasaha naye anapaswa kutumia mbinu nzuri na ya ujanja ili kumfanya yule anayemnasihi asiudhike sana, na hivyo kumuandalia mazingira ya kuipokea kwa mikono miwili nasaha na mwongozo anaompatia. Hekima na maneno mazuri sambamba na upole na ulaini ni jambo muhimu mno wakati wa kumnasihi mtu; kwani endapo mtoaji nasaha atatumia mbinu mbaya na ya maudhi au kutumia maneno ya kejeli atakuwa ameandaa mazingira ya mhusika kuikataa nasaha yake na hata wakati mwingine kuzusha tafrani na ugomvi baina yao.

Naam! kwa leo nalazimika kukomea hapa kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki. Ninakuageni huku nikimuoumba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa wanaosikiliza nasaha na maneno na wakafuata mazuri yake.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.