Nov 03, 2018 13:02 UTC
  • Ruwaza Njema (7)

(Kumfuata al-Mustafa (saw) katika maneno na kimya chake)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 7 ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambapo tunaendelea kuzungumzia maandiko matukufu ambayo yanatuangazia njia katika kufuata mfano na maadili bora ya Mtume Mtukufu (saw) ambapo kwa leo tutategemea maandiko hayo katika kujua na kufahamu vyema tabia na muamala wa mbora huyo wa viumbe (saw) kuhusiana na suala zima la kumnyenyekea Mwenyezi Mungu na kufanya utani mzuri na unaofaa, karibuni.

*************

Wapenzi wasikilizaji, ibada ya Mwenyezi Mungu ndio msingi wa kumnyenyekea na moja ya mifano ya wazi zaidi ya unyenyekevu tuliyofundishwa na mfanya-ibada ya kweli mtukufu Mtume (saw). Imepokelewa katika kitabu cha Hilyat al-Abrar cha Allama Sayyid Hashim al-Bahrani (MA) akimnukuu Amir al-Mu'mineen (as) kwamba: 'Mtume (saw) alipokuwa akisimama kuswali, uso wake ilikuwa ukibadilika kutokana na hofu ya Mwenyezi Mungu na sauti inayofanana na ya kuchemka na kutokota kitu kwenye sufuria (au pipa) ilisikika kutoka ndani ya kifua chake.'

 

Ndugu wasikilizaji na tunasoma katika kitabu cha az-Zuhd cha Hussein bin Said al-Ahwazi na al-Kafi cha Thiqatul Islam al-Kuleini akimnukuu Imam Swadiq (as) anayesema: Mtu mmoja alimletea Mtume (saw) maziwa na asali ili apate kunywa. Mtume akasema: Hivi ni vinywaji viwili ambapo mtu anaweza kutosheka na kimoja. Mimi sitakunywa kimoja na wala sikiharamishi lakini ninadhihirisha unyenyekevu wangu kwa Mwenyezi Mungu kupitia kitendo changu hiki. Hii ni kwa sababu kila mtu anayemnyenyekea Mwenyezi Mungu, humyanyua na kila anayemfanyia kiburi humteremsha. Kila mtu anayefuata nyendo za wastani maishani Mwenyezi Mungu humfikishia riziki yake na kila anayevuka mpaka na kufanya israfu Mwenyezi Mungu humnyima. Kila anayedhikiri na kumkumbuka kwa wingi Mwenyezi Mungu, humpa malipo yake.'

Na tunafahamu kutokana na Hadithi Hii tuliyosoma kwamba moja ya mifano ya kumyenyekea Mwenyezi Mungu ni kunufaika na neema zake bila kufanya israfu kama njia ya kushukuru neema hizo.

*********

Ndugu wasikilizaji, je, Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akiamiliana vipi na masahaba zake kuhusiana na suala zima la kufanya mzaha na utani? Ni jambo gani linalopasa kumfanya muumini afanye mzaha na utani unaofaa? Na ni masharti yapi yanayotakikana katika kutekeleza jambo hilo? Katika kujibu swali hili muhimu tunaanza kwa kunukuu Hadithi iliyopokelewa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Imam Swadiq (as) ambapo alimuuliza mmoja wa wafuasi wake kwa kusema: 'Je, mnataniana?' mfausi huyo akamjibu: 'Mara chache sana.' Imam (as) akamuuliza tena: Ni kwa nini hamtaniani? Hakika utani ni katika tabia njema, kwa sababu kwa kitendo hicho wewe huweza kumfurahisha ndugu yako. Mtume (saw) alipotaka kumfurahisha mtu alikuwa akimfanyia utani.'

 

Kwa kwa maelezo hayo, nia ya kwanza ya kufanya mzaha na utani inapasa kuwa ni kufuata mfano mzuri wa bwana wetu Mtume Mtukufu (saw) katika kunufaika na neema hii muhimu aliyotupa Mwenyei Mungu. Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kupitia Mummar bin Khallad kwamba alisema: 'Nilimuuliza Abal Hassan – yaani Imam Ridha (as) – kwa kusema: Nifanywe kuwa fidia kwa ajili yako! Je, mtu anapokuwa miongoni mwa watu na kujiri hapo mazungumzo na mzaha na kisha kuanguliwa kicheko, nini taklifu ya jambo hilo? Imam akasema: Hakuna tatizo kama hakutakuwa! Hapo nikadhani kwamba alikusudia kama hakutakuwa na matusi katika kufanya hivyo. Kisha akasema (as): Hakika bedui mmoja alikuwa akija kwa Mtume (saw) na kumletea zawadi na kisha kusema: Tupe zawadi mkabala wake! Hapo Mtume (saw) alicheka. Kila mara alipokuwa akihuzunika, Mtume (saw) alikuwa akisema: 'Bedui huyu alifanya nini?!! Laiti angelikuja tena kwetu!'

**********

Hivyo, miongoni mwa masharti ya kufanya mzaha na utani ni kujiepusha kutumia mambo machafu na matusi yanayowaudhi wengine na kujiweka mbali na batili. Hafidh al-Halabi anasema katika kitabu cha al-Manaqib: 'Mtume (saw) alikuwa akifanya mzaha na kutosema ila haki.' Naye Sheikh Tusi anasema katika kitabu chake cha Aamali akimnukuu Imam Ali (as): 'Kicheko cha Mtume (saw) kilikuwa ni kutabasamu.'

********

Wapenzi wasikilizaji, tunamwomba Mwenyezi Mungu ajaze nyoyo zetu sote furaha na nuru kwa baraka za kufuata mfano mwema wa Bwana Mtume (saw). Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo, panapo majaaliwa yake Mwenyezi Mungu, katika kipinid kingine cha Ruwaza Njema kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags