Matukio ya Spoti, Nov 12
Ufuatao ni ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, likiwemo Debi la Machester
Soka ya Ufukweni: Iran yatwaa ubingwa Dubai
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Soka ya Ufukweni baada ya kuisasambua Russia mabao 4-2 katika mchuano wa fainali uliopigwa mjini Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu. Wachezaji wa Iran walishuka dimbani wakijiamini, kwani dakika mbili baada ya kupulizwa kipenge na kuanza mchezo, kiungo wa Iran Mostafa Kiaani alipachika wavuni bao la mapema. Dakika chache baadaye, Mohammad Massoumi Zadeh aliongeza la pili, huku kipa Hamid Behzad-pour akifanya mambo kuwa 3-0 kabla ya kwenda mapumziko.
Baada ya kutoka mapumzikoni, Russia ilipata bao la kwanza lakini Massoumi Zadeh alifunga lake la pili na la nne kwa Iran na kuyumbisha kabisa jahazi la Warusi. Russia iliongeza bao la pili baadaye, lakini halikuweza kuitikisa timu hiyo ya Iran. Ilikuwa shangwe, nderemo na vifijo wakati Iran ikikabidhiwa kombe hilo la mabara katika mashindano hayo yanayojulikana kama Intercontinental Beach Soccer Cup yaliyofunga pazia lake Jumamosi katika mji wa Dubai, huko Imarati. Iran ilifungua kampeni ya kusaka ubingwa wa kombe hilo kwa kuisasambua Marekani mabao 8-1. Mbali na Iran, Russia na Marekani, nchi nyingine zilizoshiriki mashindano hayo ni Uhispania, Imarati, Misri, Tahiti na Brazil.
Soka ya Asia; Persepoli yamaliza ya 2
Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili baada ya kulazimishwa sare tasa na klabu ya Kashima Antlers ya Japan katika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Barani Asia iliyopigwa Jumamosi katika Uwanja Taifa wa Azadi hapa mjini Tehran. Jeshi Jekundu la Tehran lilishindwa kufurukuta mbele ya Wajapani, licha ya kucheza mbele ya mashabiki zaidi ya 70 elfu waliokuwa wamefurika kwenye uwanja huo.
Hata hivyo Shirikisho la Soka Barani Asia limeipongeza klabu ya Persepolis kwa kuonesha mchezo mzuri, licha ya kutofanikiwa kucheka na nyavu za Masamurai wa Japan. Aidha Gianni Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA amewapongeza Wairani kwa kuwa mashabiki kindakindani wa kabumbu, akisisitiza kuwa ushabiki huo ni hazina kubwa isiyo na mfano kwa ulimwengu wa kandanda. Aliyasema hayo pambizoni mwa fainali hiyo ya Jumamosi, katika mkutano wake na Masoud Soltanifar, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran hapa Tehran.
Kashima ya Japan imetwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Barani Asia, licha ya sare tasa Jumamosi, kwa kuzingatia kuwa ilikuwa imeilima Persepolis mabao 2-0 katika duru ya kwanza ya mechi zao, wiki iliyopita nchini Japan. Mashabiki wa Kashima Antlers wameruhia ushindi huo, ndani na nje ya Iran. Persepolisi ya Iran imebuika ya pili na kutwaa medali ya fedha.
Soka: Esperence Bingwa wa Afrika!
Klabu ya sok ya Esperance de Tunis ya Tunisia ndio mabingwa wapya wa taji la klabu bingwa barani Afrika, baada ya kuichabanga Al Ahly ya Misri, mabao 3-0 katika mzunguko wa pili wa fainali uliochezwa Ijumaa usiku. Ushindi huo uliiwezesha Esperance kubeba taji hilo, kwa ushindi wa mabao 4-3, licha ya kupoteza fainali ya kwanza ya mabao 3-1 ugenini nchini Misri. Saad Bguir, ndiye aliyekuwa shujaa wa mechi hiyo ya marudiano iliyochezwa mjini Rades, kwa kuifungia klabu yake mabao 2. Hili ni taji la tatu la Esperance katika fainali za klabu bingwa Afrika.
Mbali na Bquir, Anice Badri alifunga bao la tatu, katika mchuano huo ulioshuhudiwa na makumi ya maelfu ya mashabiki wa Esperance chini ya ulinzi mkali. Mbali kutunukiwa kombe la CAF, Esperance imejishindia Dola za Marekani Milioni 2.5. Al Ahly ya Misri, imeshinda mataji manane. TP Mazembe ya DRC, Zamalek ya Misri imeshinda mara tano. Canon Yaounde ya Cameroon, Hafia (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco) zimeshinda mara tatu.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Afrika CAF limepanga ratiba ya michezo ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa (CAF Champions League) na michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, mchezo wa kwanza baina ya Simba na Mbabane Swallows utachezwa ama tarehe 27 au 28 mwezi huu Jijini Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki moja baadaye Mjini Mbabane. Mshindi baina ya Simba na Mbababe atachuana na mshindi baina ya Nkana ya Zambia na Uniao Desportiva Do Songo ya Msumbiji. Gor Mahia ya Kenya itachuana na Big Bullets ya Malawi, Asas Djibout Telecom ya Djibout itavaana na Jima Abijafar ya Ethiopia, huku Orlando Piratees ya Afrika Kusini itatoana udhia na Light Star ya Ushelisheli. Le Messenger Ngozi ya Burundi itakuwa mwenyeji wa Ismailia ya Misri huku AS Sonidep ya Niger ikiikaribisha nyumbani Zesco ya Zambia. APR ya Rwanda italimana na Club Africaine ya Tunisia, huku Al Hilal ya Sudan ikicheza na JKU ya Zanzibar. Vipers ya Uganda itaanzia ugenini kwa kuchuana na El Merreikh ya Sudan.
Katika Kombe la Shirikisho baadhi za awali zitakuwa kama ifuatavyo; Zimamoto ya Zanzibar itachuana na Kazier Chiefs ya Afrika Kusini; DC Motema Pembe itachuana na Les Anges De Fatima; AS Nyuki itaanzia ugenini dhidi ya Al Ahly Shandi ya Sudan; Mtibwa Sugar ya Tanzania itachuana na Nothern Dynamo ya Ushelisheli.
Dondoo za Hapa na Pale
Raga: Timu ya raga ya wanawake ya Kenya imeichachafya Uganda mizunguko 47-0 na kutwaa taji la Safari 7's la mwaka huu 2018, katika fainali ya aina yake iliyopigwa katika Viwanja vya RFUEA nchini Uganda Jumapili. Hata hivyo Samurai International walitwaa ubingwa kwa upande wa wanaume baada ya kuisasambua Shujaa ya Kenya 21-14 huko huko Uganda.
EPL: Katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Manchester United iligaragazwa mabao 3-0 iliposhuka dimbani kuvaana na watani wao wa jadi, Manchester City siku ya Jumapili katika Uwanja wa Etihad na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL.
Mabao ya City yalifungwa na David Silva, Sergio Aguero na Ilkay Gundogan huku Mashetani Wekundu wakiambulia bao moja la kufutia machozi lililofungwa na Anthony Martial kupitia mkwaju wa penati. Liverpool iliilaza Fulham mabao 2-0 na kufikisha alama 30, alama 2 nyuma ya City, wakati Arsenal ilikuwa ikilazimishwa sare ya 1-1 na Wolverhampton. Mchuano wa Everton na Chelsea ambayo ipo katika nafasi ya tatu kwa sasa ikiwa na alama 28 uliishia kwa sare tasa.
Iran Karate: Timu ya karate ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeng'ara katika mashindano Mabingwa wa Karate 2018 katika mji wa Madrid nchini Uhuspania, kwa kuzoa medali 5, ikiwemo dhahabu moja, fedha moja na shaba 3. Bahman Asgari iliipa Iran medali ya dhahabu katika kategoria ya wanakarate wenye kilo zisizozidi 75 katika mashindano hayo ya dunia yaliyowaleta pamoja makarateka 1,200 kutoka nchi 139 duniani.
……………………TAMATI………………