Dec 19, 2018 11:50 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 793 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 28 hadi 30 ambazo zinasema:

وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ قَوْمِهِ مِن بَعْدِهِ مِن جُندٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَمَا كُنَّا مُنزِلِينَ

Na hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.

إِن كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ خَامِدُونَ

Hakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!

يَا حَسْرَةً عَلَى الْعِبَادِ ۚ مَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ

Nawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wanamfanyia stihzai.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa watu wa mji wa Ant'akiya katika eneo la Sham waliwaudhi na kuwapiga vita Mitume waliotumwa kwao ili kuwaelekeza kwenye uongofu na wakaukadhibisha wito waliolinganiwa na Mitume hao. Watu hao aidha walimuua mtu aliyekuwa akiitwa Habib ambaye alisimama kuwahami na kuwaunga mkono Mitume hao wa Allah. Katika aya hizi tulizosoma, Allah SW anasema: watu waliowakadhibisha Mitume na wakamuua yule mja muumini walistahili adhabu, tena ni ya papa hapa duniani. Kwa hivyo kwa amri ya Mola, ukelele mkali uliwashukia kutoka mbinguni na kuwaangamiza. Kimsingi hasa ni kwamba kuziangamiza kaumu potofu na za watu waovu ni jambo sahali na jepesi kwa Allah SW, wala halihitaji jeshi maalumu la kutoka mbinguni. Hakuna ulazima kwa Yeye Mola aliye muweza wa kila kitu kutuma jeshi la malaika ili kuwaangamiza watu hao; lakini kwa irada yake huibuka sauti kali na nzito kutokea ardhini na mbinguni ambayo huwazima na kuwapatiliza watu hao wakabaki wakiwa wafu waliotulia tuli bila ya harakati yoyote wala uwezo wa kutamka chochote.  Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Kuhasirika na majuto ni kwa waja wa Mwenyezi Mungu ambao, badala ya kuuamini uongofu utokao kwa Mola wao, mwenendo wao huwa sababu ya wao kuangamizwa. Mwenendo ambao huanza kwa kufanya kejeli na stihzai na kuishia kuwafanyia maudhi na hata kuwaua mawalii wa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba endapo jamii yoyote ile itawadunisha na kuwafanyia stihzai na maudhi mawalii wa Allah ingojee kushukiwa na adhabu ya Mola ambayo yumkini hata ikatokea ghafla. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa vitisho vya watumiaji mabavu na waistikbari visitutishe na kutufanya tuiache njia ya haki. Kama Allah SW atataka, maadui na madhalimu hao wanaweza kuangamizwa mara moja. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba imani zetu zisiyumbe kwa kufanyiwa stihzai na watu, wala tusiwe na ajizi katika kutekeleza wajibu wetu kidini. Tujue kwamba Mitume wote wa Allah walifanyiwa kejeli na stihzai lakini hawakuacha katu kushikamana na haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 na 32 za sura yetu ya Ya-Sin ambazo zinasema:

أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّنَ الْقُرُونِ أَنَّهُمْ إِلَيْهِمْ لَا يَرْجِعُونَ

Je! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao.

وَإِن كُلٌّ لَّمَّا جَمِيعٌ لَّدَيْنَا مُحْضَرُونَ

Na hapana ila wote watakusanywa na kuhudhurishwa mbele yetu.

Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kuwahutubu watu wote kwa kuwauliza: kwa nini hamutalii historia ya kaumu zilizopita na yale yaliyozisibu kaumu hizo? Hivi hamuoni nyinyi kama kuna kaumu nyingi zimepita kabla yenu na zote zimetoweka? Bali hata baadhi yao zilikuwa na nguvu, utajiri mkubwa wa mali na ustaarabu uliostawi, lakini leo hii hakuna athari yoyote iliyosalia na hakuna njia yoyote ya watu wa kaumu hizo kuweza kurudi duniani na kuishi na watu wanaoishi katika zama hizi. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba katika mambo yanayousiwa na Qur'ani ni kutalii na kusoma historia za kaumu na mataifa yaliyopita. Tab'an ni kutalii kutakakotufanya tupate ibra na mazingatio, si kwa ajili ya kujiburudisha na kujichangamsha! Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa desturi na kaida ya Allah ni thabiti na haibadiliki katika zama zote za historia; na hatima za kaumu zenye matendo ya namna moja ni zenye kufanana. Kwa hivyo kushuhudia taswira ya hatima ya kaumu moja kunatoa picha yenye mshabaha na hatima ya kaumu nyingine. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba baada ya mauti hakuna njia yoyote ya kurudi tena duniani. Kwa hivyo kwa mtazamo wa Qur'ani, itikadi ya tanasukh waliyonayo waumini wa dini ya Kihindu, kwamba watu hurudi tena duniani baada ya kufa kwa roho zao kuhamia kwenye viwiliwili vya viumbe wengine, haikubaliki na wala haina mashiko.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 33 hadi 35 ambazo zinasema:

وَآيَةٌ لَّهُمُ الْأَرْضُ الْمَيْتَةُ أَحْيَيْنَاهَا وَأَخْرَجْنَا مِنْهَا حَبًّا فَمِنْهُ يَأْكُلُونَ

 Na Ishara kwao ni ardhi iliyo kufa, tunaifufua tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!

وَجَعَلْنَا فِيهَا جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ وَفَجَّرْنَا فِيهَا مِنَ الْعُيُونِ

Na tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukachimbua chemchem ndani yake,

لِيَأْكُلُوا مِن ثَمَرِهِ وَمَا عَمِلَتْهُ أَيْدِيهِمْ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ

Ili wale katika matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?

Aya zilizotangulia zimezungumzia maudhui ya maadi na kuhudhurishwa viumbe mbele ya Allah Jalla fii Ulahu. Aya hizi tulizosoma hivi punde zinasema: moja ya alama na ishara za kufufuliwa viumbe zilizopo hapa duniani ni kuhuika ardhi yabisi baada ya kufa kwake. Ardhi hufa wakati wa msimu wa baridi kali na kusita kutoa mazao yoyote yale. Lakini unapowadia msimu wa machipuo, ardhi hiyo huhuika na kunawirika kwa kuchipua na kuchanua anuai na namna mbalimbali za mimea na miti, utaratibu ambao hukariri na kujirudia kila mwaka.  Katika msimu wa baridi kali haionekani ishara wala athari yoyote ya uhai katika mimea. Lakini linapochomoza jua la msimu wa machipuo maua huchanua na miti yote hunawiri kwa rangi ya kijani kibichi. Ajabu ni kwamba maisha ya wanadamu wenyewe katika sayari hii ya dunia yanategemea na yamefungamana na maisha ya mimea. Ikiwa itatokea siku mimea ikatoweka na wanyama wakafa, mwanadamu, ambaye mahitaji yake makubwa ya chakula yanategemea mimea na wanyama, hatoweza kudumu na kubaki hai tena. Na kati ya vilaji mbalimbali pia, Qur’ani tukufu inazipa umuhimu na mazingatio maaalumu tende na zabibu na kuzitaja kuwa ni neema maalumu za Allah. Huenda sababu yake ikawa ni kutokana na matunda mawili hayo kujulikana kuwa ni aina kamili ya vyakula vyenye anuai za vitamini zinazohitajiwa na mwili wa mwanadamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba maumbile ni kitabu cha uumbaji wa Allah ambapo kuutalii kila ukurasa wake kwa kina na tafakuri humuongoza na kumfikisha mtu kwenye utambuzi wa kumjua Muumba wa ulimwengu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa maadi na ufufuo wa wanadamu hauwezi kufanyika kivitendo hapa duniani lakini kufufuka kwa mimea na miti tunaweza kukushuhudia kwa macho yetu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba mwanadamu anapaswa kuwa mshukurivu kwa Mola wake kutokana na kujaaliwa anuai za matunda na vyakula. Lakini inasikitisha kuona akthari ya watu si washukurivu wa neema hizo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 793 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa washukurivu wa kauli na matendo wa neema anazotujaalia, kubwa na ndogo, tunazozijua na tusizozijua. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.