Dec 24, 2018 11:12 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 799 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 71, 72 na 73 ambazo zinasema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ

 Je! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.

وَذَلَّلْنَاهَا لَهُمْ فَمِنْهَا رَكُوبُهُمْ وَمِنْهَا يَأْكُلُونَ

 Na tumewatiisha kwao. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala. 

وَلَهُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَمَشَارِبُ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ

Na wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?

Aya hizi zinazungumzia moja ya ukarimu na neema za Mwenyezi Mungu kwa wanadamu pamoja na mchango wa wanyama katika maisha ya watu. Japokuwa sehemu kubwa ya wanyama hawawezi kufugwa na watu, na wanaishi baharini na nchi kavu, lakini baadhi ya wanyama wanafugika na maridhia kuweza kutiishwa na wanadamu kiasi cha kuwahisi ni milki zao za kuweza kuzitumia na kufaidika nazo kwa namna yoyote ile watakayo. Tusisitize pia kwamba katika zama za ustaarabu na maendeleo za hivi sasa, utumiaji wa wanyama wa miguu minne yaani nyamahowa, si tu haujapungua lakini kwa namna fulani umeongezeka pia. Ikiwa hapo zamani watu walikuwa wakipata kutoka kwa wanyama maziwa ya ng'ombe na kondoo na bidhaa nyingine chache za vilaji na vinywaji, leo wanadamu wanapata bidhaa nyingine kadha wa kadha za maziwa kutokana na maziwa tu ya wanyama. Kuna aina mbalimbali za nguo, mikoba na viatu zinazozalishwa kutokana na ngozi, sufu na manyoya ya wanyama. Katika zama zetu hizi, licha ya kutumika mada za viwandani kutengezea nguo na bidhaa nyingine zinazohitajiwa na watu lakini nguo zinazotengezwa kwa kutumia ngozi na sufu ya wanyama bado hazijapoteza hadhi na umaarufu wake. Hivi sasa katika maeneo mengi duniani na hata katika majeshi yaliyoendelea kwa zana za kisasa, wanyama kama farasi na ngamia ni vipando bora vinavyotumika kwenye maeneo magumu kupitika ya majangwani na milimani au kwa ajili ya kuvushia zana na bidhaa katika maeneo hayo. Kwa hakika sehemu kubwa ya mahitaji ya chakula cha mwanadamu inatokana na nyamahowa. Mfumo wa uumbaji umeyakidhi kwa namna mwafaka mahitaji ya kiumbe huyo kupitia kuzaliana kwa wakati kwa wanyama hao. Lakini ukweli ni kwamba mwanadamu si mshukurivu wa neema hiyo kubwa; na kama wapo, basi ni watu wachache ambao wamewahi kukaa hadi sasa, wakatafakari na kujiuliza itakuwaje kama itatokea siku wanyama hao wakawa hawapo tena au wakashindwa kufugika na kuwa maridhia kwa mwanadamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba wanyama wa miguu minne kama ng'ombe, kondoo, mbuzi na ngamia wameumbwa kwa ajili ya mwanadamu. Kwa hivyo kama wanyama, hasa wa miguu minne, hawatakuwepo, maisha ya wanadamu yatakuwa mashakani. Lakini kama wanadamu hawatakuwepo katika sayari hii ya dunia, wanyama hawatopata shida yoyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuwepo kwa wanyama na kuwa kwao maridhia kwa kuweza kufugwa na wanadamu ni miongoni mwa neema za Mola. Kwa sababu kama wasingekuwa hivyo ingekuwa tabu kubwa kwa mwanadamu kuwatumia kwa ajili ya kujipatia nyama, maziwa n.k. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutozingatia neema za Allah humfanya mtu ajisahau na kuwa mtovu wa ushukurivu kwa Muumba wa ulimwengu.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 74 hadi 76 ambazo zinasema:

وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لَّعَلَّهُمْ يُنصَرُونَ

Na wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!

لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَهُمْ وَهُمْ لَهُمْ جُندٌ مُّحْضَرُونَ

Hawataweza kuwasaidia. Bali wao (Siku ya Kiyama) kwa hayo masanamu watakuwa (mithili) ya askari wa jeshi lao watakao hudhurishwa.

فَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّا نَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ

Basi yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza.

Moja ya alama za utovu wa shukurani wa mwanadamu kwa neema za Allah ni kuwaelekea maabudu na miungu mingine badala ya Yeye Mola. Hili ni jambo ambalo washirikina wanalifanya kwa uwazi, na baadhi ya waumini huwa wanalifanya kwa kificho na bila ya kubainika hadharani. Shirki ya wazi ni ile mtu kusema: Mimi ninamwabudu mtu huyu au kitu hiki. Lakini shirki iliyojificha ni ya mtu kutotamka wazi neno kuabudu lakini akasema kwa mfano, ghairi ya Mwenyezi Mungu, mtu huyu amekuwa na nafasi kuu katika maisha yangu; na lau kama si yeye, mimi ningekuwa hohehahe sina sinani maishani. Au pengine akasema, ni kwa msaada wake yeye tu, ndo mimi nimeweza kufika hapa nilipofika. Hali ya kuwa jambo lililo wazi ni kwamba, vitu au watu hawawezi kufanya lolote lile katika maisha ya mtu bila ya kumtegemea Mwenyezi Mungu wala hawawezi kuwa na nafasi ya kuwa mshirika wa Yeye Allah. Kila jambo linafanyika kwa irada ya Allah, Naye hana mshirika yeyote yule. Tab'an huvifanya vitu au watu kuwa wenzo na kiunganishi, ili kupitia wao, mja fulani aweze kuipata neema au aweze kutekelezewa huduma na haja anayohitajia. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Wakati dhahiri na batini ya amali za mtu itakapobainika Siku ya Kiyama, washirikina watasimama nyuma ya masanamu waliyokuwa wakiyaabudu, utadhani masanamu hayo ni makamanda, na wao washirikina ni askari wa jeshi lao; kwa sababu walipokuwako duniani walikuwa hawaoni hawasikii isipokuwa kutii na kufuata mambo ya khurafa na uzushi waliyokuwa wakiyaabudu. Aya ya 76 inamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW na waumini kwamba: Msihuzunike wala kuvunjwa moyo na kukatishwa tamaa na maneno ya maudhi, kejeli na stihzai wanayosema washirikina na kumnasibisha nayo Mtume, Qur'ani na itikadi za dini yenu. Wao mwachieni Mwenyezi Mungu ambaye ni Mjuzi wa kila jambo; Naye atawalipa kwa kuwaadhibu kwa mujibu wa maovu wanayoyafanya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba hakuna kitu au mtu yeyote katika ulimwengu mwenye taathira iliyo mkabala na Allah SW. Visababishi vyote, iwe ni vya kimaada na visivyo vya kimaada ni wasita na kiunganishi kitokacho kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wala hakina nafasi na taathira ya kujitegemea katika maisha ya mwanadamu na inayotokana na kitu hicho chenyewe. Kwa hivyo shirki haina asili wala msingi wowote madhubuti wa kutegemea. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuomba msaada kwa mwengine yeyote, bila ya kuzingatia qudra na uwezo wa Allah ni aina fulani ya shirki na kukufuru. Kwa hakika kuwasaidia wengine kwa lolote kunategemea irada na kutaka Yeye Mola. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tutahadhari maneno ya maudhi na kejeli ya wapinzani wa dini yasije yakatudhoofisha na kutufanya tuvunjike moyo katika kutekeleza majukumu na wajibu wetu wa kidini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 799 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atutakase na kila aina ya shirki, kubwa na ndogo, za dhahiri na zilizojificha. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags