Dec 24, 2018 11:23 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 801 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu wa aya ya 81 ambayo inasema:

أَوَلَيْسَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُم ۚ بَلَىٰ وَهُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ

Kwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwa nini! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi. 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia ishara kadhaa za qudra na uwezo wa Allah katika uumbaji wa mwanadamu kutokana na tone la manii na pia upatikanaji moto kutoka kwenye miti ya kijani kibichi. Aya hii ya 81 inaashiria uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika uumbaji wa mbingu na ardhi na kueleza kwamba: Ikiwa nyinyi mna shaka na uwezo wa Mwenyezi Mungu, kwa kuhoji kama kweli Yeye ni mweza wa kuwafufua na kuwahuisha tena watu waliokufa, kwa nini hamwangalii adhama ya mbingu na ardhi jinsi zilivyoumbwa na zikawa zinazunguka kwa kufuata nidhamu maalumu na ya kuajabiwa? Ukubwa na adhama ya mfumo wa ulimwengu wa maumbile ni mkubwa kiasi ambacho sayari yetu hii ya dunia inapolinganishwa na mfumo huo mzima huwa mithili ya chembe ya mchanga katika jangwa na uwanda mpana. Ardhi yenyewe pia ina anuai za viumbe wadogo wadogo na wakubwa wakubwa. Miongoni mwao ni milima na bahari kubwa, nyanda na mabonde pamoja na mito na aina mbalimbali za madini, wanyama wa nchi kavu na viumbe wa baharini na namna tofauti za mimea na miti ambayo idadi yao kamili iko nje ya uwezo wa wanadamu. Baada ya kuziona adhama zote hizo katika ulimwengu wa uumbaji, bado mngali mna shaka kama Mwenyezi Mungu ataweza kweli kukufueni tena Siku ya Kiyama? Hapa duniani, tone la mbegu ya uzazi inayotunga kwenye fuko la uzazi la mama hugeuka kuwa kiumbe kamili cha mtu. Lakini huko akhera, kama inavyokuwa punje ya mbegu inayopandwa kwenye udongo, kisha mche wake ukachipua kutoka ardhini, ndivyo chembe mojamoja ya mabaki ya kila mtu zitakavyoweza kwa qudra ya Mwenyezi Mungu kutoka ardhini na kuonekana kiumbe kamili sawa kabisa na yule aliyekuweko awali hapa duniani. Kama mtu atapitikiwa na shaka kwamba chembechembe za miili ya watu zimetapakaa duniani wala haijulikani ni wapi hasa zilipo inapasa afahamu kwamba elimu na ujuzi wa Allah vimeuhodhi na kuutawala ulimwengu mzima; Yeye ni mwelewa wa kila kitu na hakuna chochote kile kilicho nje ya elimu yake. Kwa hivyo Yeye ni Mweza wa kuzikusanya chembechembe zote za mwili wa mtu popote pale zilipotawanyikia na kumfufua tena kiumbe huyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika kukabiliana na shubha na utata unaozushwa na wakanushaji wa maadi, badala ya kutoa jawabu za moja kwa moja tunaweza kutumia mbinu ya kuwatupia masuali ya kuzizindua dhamiri zao ili waweze wao wenyewe kupata majibu ya masuali yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa uumbaji unahitaji elimu na uwezo; na Allah SW ni mwenye ujuzi mutlaki na uwezo usio na ukomo duniani na akhera. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba Yule mwenye uwezo wa kuumba ulimwengu wenye adhamu na mfumo wake wa uendeshaji wenye kustaajabisha mno, ni mweza pia wa kuwafufua wanadamu Siku ya Kiyama.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 82 ya sura yetu hii ya Ya-Sin ambayo inasema:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

Hakika amri Yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia kwa kutilia mkazo tena qudra na uwezo wa Allah SW kwa kusema: Uumbaji vitu ni jambo jepesi na sahali kwake Yeye. Si kwamba uumbaji wa mbingu ni kazi ngumu kwake, na uumbaji wa mdudu chungu au sisimizi ni jambo rahisi kwake, bali vitu vyote vina hali sawa kwake Yeye Mola; chochote kile atakacho kiwe, huwa kinakuwa kwa irada na kutaka kwake. Kwa maneno mengine, hakuna mpaka wa muda baina ya irada au kutaka kwa Allah na kuwa kwa kitu anachotaka kiwepo; ni kama ulivyo ule msemo maarufu kwamba ni sawa na mpepeso mmoja tu wa jicho. Sisi wanadamu pia tunao uwezo wa kutasawari kitu akilini mwetu kwa namna ambayo hakutakuwa na mpaka wa muda kati ya irada yetu na uletaji taswira hiyo. Lakini hatuna uwezo wa kulifanya hilo lithibiti katika dunia halisi ya nje ya akili zetu. Lakini Yeye Allah Jalla Fii Ulaah atakapo jambo liwe, huwa na huthibiti papo hapo katika ulimwengu huu wa nje. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba uumbaji wa vitu vyote, vikubwa na vidogo au vyepesi na vigumu vina hali moja tu kiuwezo kwa Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye akifanyae kila kitu na ndiye anayejaalia viumbe ambavyo havikuwepo abadani, viwe na uwepo na uhai. Kwa maneno mengine, Yeye Allah anaanzisha viumbe na kuvipa sura na maumbo yao kwa wakati mmoja, wakati sisi wanadamu tuna uwezo wa kuvipa vitu sura na umbo tu lakini hatuna uwezo katu wa kuanzisha na kuleta kiumbe ambacho hakikuwepo asilani.

Wapenzi wasikilizaji, darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 83 ikiwa ndiyo aya ya mwisho ya Suratu Ya-Sin ambayo inasema:

فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Basi Ametakasika Yule Ambaye mkononi Mwake umo Ufalme wa kila kitu; na Kwake Yeye mtarejeshwa.

Aya hii ambayo kama tulivyotangulia kueleza ndiyo aya ya mwisho ya Suratu Ya-Sin inatoa hitimisho jumla kwa kusema: Utawala na umiliki mutlaki wa mfumo mzima wa ulimwengu wa uumbaji uko mikononi mwa Allah SW; Naye ametakasika na kila ila, kasoro na upungufu au udhaifu wa kushindwa kufanya chochote kile. Kwa msingi huo, haipasi mtu yeyote yule kutilia shaka qudra na uwezo wa Allah wa kuwaumba tena wanadamu Siku ya Kiyama; na hakuna shaka yoyote kuwa, wao wote watarejea kwake. Ni jambo lililo muhali, lakini tujaalie kama mwanadamu angekuwa mmiliki wa asili ya kuwepo kwake mwenyewe, huenda angeweza kuwa na uwezo wa kukabiliana na irada hiyo ya Mola, lakini ukweli ni kwamba mwanadamu si mmiliki wa nafsi yake, bali yeye ni mmilikiwa wa Allah, wala hana chochote kitokanacho na yeye mwenyewe. Mwanadamu, ambaye hana mamlaka hata ya kujiamulia wakati wa kuja na kuondoka kwake duniani, ni kwa hoja gani anaitilia shaka Siku ya Kiyama? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba vipi tunamdhania Mwenyezi Mungu kuwa si mweza wa kuwafufua viumbe Siku ya Kiyama, ilhali Yeye ni Mweza wa kufanya lolote lile atakalo na ametakasika na kila ila na kasoro. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mwanzo na mwisho wa ulimwengu uko kwenye mamlaka ya Allah SW peke yake. Uumbaji umeanzia kwake, na viumbe vyote mwishowe vitarejea kwake Yeye. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 801 ya Qur'ani imefikia tamati na ndiyo inayotuhitimishia tarjumi na maelezo ya sura ya 36 ya Ya-Sin. InshaaAllah tuwe tumeaidhika na kuelimika na yote tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags