Jan 02, 2019 06:35 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 807, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 39 ambayo inasema:

وَمَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

Wala hamtalipwa ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoashiria tuhuma za washirikina na makafiri dhidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW na vilevile adhabu kali watakayopata watu hao Siku ya Kiyama. Aya hii tuliyosoma inasema: adhabu ya Allah kwa waovu haitatokana na kinyongo na uadui dhidi yao au kukomoa na kulipiza kisasi, ila ni matokeo na matunda ya amali zao walizofanya hapa duniani. Kwa mujibu wa maandiko ya dini, fikra, maneno na mwenendo wa mtu vinaiathiri roho na nafsi yake mtu huyo na ndivyo vinavyojenga shakhsia yake. Katika mfumo wa malipo wa akhera msingi wa malipo ya thawabu na adhabu ni shakhsia ya mtu iliyojengeka duniani ambayo itadhihirika katika umbo linaloendana na mfumo huo wa akhera. Kukufuru na kukanusha, au kudhulumu na kutakabari, ni mambo yenye taathira haribifu na madhara kwa roho ya mtu na hayatokuwa na matokeo mengine Siku ya Kiyama isipokuwa adhabu ya moto wa Jahannamu. Inapasa kuashiria pia kwamba aghalabu ya adhabu na faini za duniani ni za upangaji na makubaliano. Kwa mfano kosa la dereva anayeitangulia kimakosa gari iliyo mbele yake, adhabu yake huwa ni faini ya pesa, ambazo kiwango chake kinatafautiana katika nchi mbalimbali. Lakini kosa hilo kwa nafsi yake lina matokeo ya madhara pia, ambayo ni hatari ya kupata ajali kwa kugongana na gari nyingine. Kwa hivyo adhabu ya faini ni suala la upangaji na makubaliano, lakini ajali ni matokeo ya kimaumbile ya kosa hilo. Adhabu za Siku ya Kiyama ni za aina ya pili na si ile ya kwanza! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba adhabu za Allah ni za uadilifu, kwa sababu zinaendana kikamilifu na amali ya mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa Siku ya Kiyama ni siku ya kudhihiri na kujitokeza matokeo ya fikra na mwenendo wetu; kwani kile tulichopanda duniani ndicho tutakachokivuna huko akhera.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 40 hadi 44 ambazo zinasema:

إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ

 Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu waliotakaswa.

أُولَـٰئِكَ لَهُمْ رِزْقٌ مَّعْلُومٌ

Hao ndio watakao pata riziki maalumu,

فَوَاكِهُ ۖ وَهُم مُّكْرَمُونَ

Matunda, nao watahishimiwa. 

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ

Katika Bustani za neema.

عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ

Wako juu ya viti wameelekeana.

Baada ya aya iliyotangulia iliyozungumzia hali ya watu wa motoni, aya hizi zinasimulia hali za watu wa peponi na kueleza kwamba: waja waliotakaswa na Allah watawekwa mbali na adhabu ya Siku ya Kiyama. Wataneemeka kwa anuai za neema za peponi na watakuwa kwenye raha na uneemevu kamili. Katika misamiati ya Qur'ani, neno mukhlis, ambalo ni jina la mtenda lina maana ya mtu anayejitahidi kuzifanya amali zake kwa ikhlasi, yaani kwa ajili ya Allah tu na anajitahidi kupiga hatua ya kujijenga na kufikia ukamilifu wa kimaanawi. Lakini neno mukhlas, lenye maana ya jina la mtendwa, linakusudiwa mtu ambaye, kutokana na ukamilifu wa kimaanawi alionao, Allah SW mwenyewe amemtakasa na kumfanya afikie kilele cha ukamilifu wa kimaanawi. Katika kumzungumzia Nabii Yusuf (as), ambaye kwa auni na msaada wa Allah aliweza kuiokoa nafsi yake na balaa kubwa la matakwa haramu ya mwanamke aliyeghilibiwa na matamanio ya kijinsia, Qur'ani tukufu imemzungumzia Mtume huyo kuwa ni miongoni mwa waja waliotakaswa na Allah. Ni wazi kwamba kama mtu mwenyewe hajataka kuwa mja mwenye ikhlasi na aliyejitakasa kwa ajili ya Allah, Yeye Mola hamtezi nguvu awe hivyo. Lakini yule anayejitahidi kufikia lengo hilo, akaichunga nafsi yake kutofanya lolote ghairi ya linalomridhisha Allah, Yeye Mola humpa auni na msaada mtu huyo na kumwongoza njia ya kumkurubisha kwake. Watu wa aina hii si tu wataepushwa na adhabu, lakini malipo yao ya thawabu pia hayatatokana na amali zao njema tu walizofanya. Bali hata kwa zile amali njema ambazo hawakufanikiwa kuzifanya, Allah atawapa malipo ya thawabu pia kutokana na nia njema na safi walizokuwa nazo kwa ajili ya kuzitenda amali hizo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa mja halisi kwa kumtii Allah SW humwekea mazingira mtu ya kutakasika na kila aina ya uchafu wa shirki na ria. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa adhabu ya waovu itatokana na uadilifu wa Allah na kulingana na amali zao, lakini malipo mema ya waja wema na watakasifu yatatokana na rehma na fadhila za Mola na kwa kiwango cha zaidi ya amali walizofanya. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba huko peponi, raha za kimaada na kimaanawi zitapatikana kwa pamoja; na kila mtu ataneemeshwa riziki ya kipimo na kiwango maalumu. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba kuonana na mawalii wa Allah na kuchanganyika na kuwa karibu nao ni moja ya neema za kimaanawi za watu wa peponi.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 45 hadi 49 ambazo zinasema:

يُطَافُ عَلَيْهِم بِكَأْسٍ مِّن مَّعِينٍ

Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem. 

بَيْضَاءَ لَذَّةٍ لِّلشَّارِبِينَ

Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao.

لَا فِيهَا غَوْلٌ وَلَا هُمْ عَنْهَا يُنزَفُونَ

Hakina madhara, wala hakiwaleweshi.

 وَعِندَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ عِينٌ

Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri. 

كَأَنَّهُنَّ بَيْضٌ مَّكْنُونٌ

 Hao wanawake kama kwamba wao ni mayai yaliyo hifadhika.

Katika sehemu ya mwisho ya aya zilizotangulia Qur'ani tukufu imeashiria kwamba watu wa peponi watakaaa kwenye viti maalumu huku wameelekeana na kusuhubiana kwa uchangamfu, furaha na upendo. Aya hizi zinaendeleza maudhui hiyo kwa kueleza kwamba: kandokando ya viti vyao watakuwepo wahudumu wa peponi wanaozunguka huku na kule ili kuwahudumia kwa vinywaji maalumu vya kuburudisha vya peponi. Ni vinywaji vitokavyo kwenye chemchem za peponi, ambapo wahudumu wa peponi watakuwa wakiteka na kuvijaza ndani ya bilauri na kuwazungushia watu wa peponi. Hapa duniani, baadhi ya jamii na kaumu za watu huwahudumia wageni wao anuai za mivinyo na vileo. Lakini aya tulizosoma zinazungumzia kwa namna fulani mivinyo ya peponi na ile ya hapa duniani. Ifahamike kwamba vinywaji vya peponi – ambavyo kwenye aya ya 21 ya Suratul-Insan vimetajwa kuwa ni 'sharaban t'wahura', (yaani kinwaji safi na kilichotoharika) – ni tofauti kabisa na vinywaji vya duniani. Na kinyume na vinywaji vya hapa duniani havileweshi wala kumfanya mtu aseme maneno au afanye vitendo visivyofaa. Katika sehemu ya mwisho ya aya hizi, Qur'ani tukufu inaashiria neema nyingine miongoni mwa neema za peponi na kueleza kwamba: wake wa peponi ambao hawawaashiki na kuwapenda watu wengine wowote ghairi ya waume zao, ni wanawake jamili na wazuri ajabu waliositiriwa na kuhifadhika pasina na kuguswa na yeyote. Kama lilivyo yai ambalo baada ya kuku kuliangua hulifunika na kulificha kwa mabawa yake, wanawake wa peponi yaani huurul-aini watakuwa wameisitiri na kuifunika miili yao kwa mavazi yaliyo mithili ya mabawa na manyoya ya ndege. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba maadi au ufufuo yatakuwa ya kimwili na kimaada. Na huko peponi kutakuweko na anuani za raha na starehe za kimwili kwa ajili ya watu wa peponi. Kama ambavyo watu wa motoni pia watakumbana na anuai za mateso na adhabu za motoni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa rangi nyeupe ni katika rangi za peponi ambayo ni ishara ya mwanga, jamali, utakasifu na unadhifu. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa wanawake wa peponi ni wazuri na warembo, na pia ni watakasifu na wenye staha.

Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 807 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na adhabu ya moto na atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake watakaorithishwa Pepo yake ya milele. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags