Feb 19, 2019 06:44 UTC
  • Ruwaza Njema (13)

Assalaam Aleikum Wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho hutufafanulia visa na mifano tofauti ya sifa na tabia njema za Mtume Mtukufu (saw), ili nasi tupate kufuata na kujipamba kwa tabia hizo njema.

Moja ya tabia hizo za kupigiwa mfano za Bwana wetu Mtume (saw) ni kuwa alikuwa akichukia sana kujifananisha kitabia na wafalme na akiwapenda sana watu masikini. Alikuwa pia akipenda sana kufuata tabia na mambo yote mema yaliyotajwa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Hili ndilo jambo tutakalolitolea mifano katika kipindi chetu cha leo kwa kutegemea marejeo ya vitabu vinavyoaminika kuhusiana na sira ya Mtume (saw), karibuni. Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu cha al-Mahasin akimsifu babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kusema: 'Mtume alikuwa akiketi kama anavyoketi mtumwa na kuweka mkono wake juu ya ardhi, na kula kwa kutumia vidole vitatu.' Kisha akasema: 'Hakika Mtume (saw) alikuwa akikula hivi na sio kama walivyofanya majabari (kwa kula kwa kutumia vidole viwili).' Na Imam (as) anasema katika Hadithi ya pili: 'Tokea alipopewa Utume hadi alipoaga dunia, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) hakuwahi kula chakula hali ya kuwa ameegemea kitu na alikuwa akichukia sana kujifananisha na wafalme.'

Abu Khadija amepokelewa katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Bashir ad-Dahaan alimuuliza Aba Abdillah as-Swadiq (as) nami nikiwa hapo: Je, Mtume (saw) alikuwa akila hali ya kuwa ameegemea upande wake wa kulia au kushoto? Akasema: Mtume hakula chochote hali ya kuwa ameegemea kulia au kushoto kwake bali alikuwa akiketi mkao wa mtumwa. Nikasema: Na ni kwa nini? Akasema: Kwa sababu ya kumyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu.'

 

Na miongoni mwa tabia za kupendeza na kuvutia za Mtume Mtukufu (saw) ni kuzingatia watu aliokula nao chakula na hasa akivutiwa sana kukula na masikini. Imam wetu mpendwa Muhammad Baqir (as) amepokelewa katika kitabu cha al-Mahasin akisema: 'Mtume (saw) alipokula chakula na kundi lolote lile la watu alikuwa wa kwanza na wa mwisho kula, ili watu wote wapate kula.' Na Imam Baqir (as) anasema katika Hadithi nyingine: 'Katika zama za Mtume (saw) masikini walikuwa wakilala msikitini. Usiku mmoja Mtume (saw) alifuturu pamoja na masikini hao waliokuwa msikitini hapo kwenye chombo kimoja cha chakula karibu na mimbar. Kwa baraka za Mtume (saw) walikula na kushiba kutoka kwenye chombo hicho watu thelathini na kisha chombo hicho kikarejeshwa kwa wake zake Mtume (saw) nao wote pia wakakula na kushiba kutoka kwenye chombo hicho.'

Imam Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu cha al-Mahasin akisema: 'Amirul Mu'mineen (as) ndiye aliyefanana zaidi na Mtume (saw) kuhusiana na suala la chakula. Alikuwa akila mkate, siki na mafuta ya zeituni na kuwapa watu mkate na nyama.'

**********

Tunasoma katika Riwaya kutoka kwa Imam Baqir (as) akisema: 'Mtume aliletewa kiwango fulani cha mali naye akamwambia Abbas: Ewe Abbas! Panua joho lako upate kuchukua sehemu ya mali hii.' Abbas alifanya alivyoombwa kufanya. Kisha Mtume (saw) akasema: Ewe Abbas! Hii ni sehemu ya maneno (mfano unaotelewa) ya Mwenyezi Mungu anayesema: Ewe Nabii! Waambie mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua kheri yoyote nyoyoni mwenu, basi atakupeni bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.

 

Miongoni mwa tabia njema na za kuvutia za Mtume Mtukufu, ambaye ni dhihirisho kamili la mafundisho ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani ni kile kisa kilichonukuliwa na Allama Tabatabai katika kitabu cha Sunan an-Nabii ambapo anasema: 'Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Ibn Ujlan kwamba alisema: Nilikuwa kwa Aba Abdillah as-Swadiq (as) ambapo mtu mmoja alifika hapo na kumwomba msaada Imam (as). Imam aliamka kutoka mahala alipokuwa ameketi na kumpa mwombaji huyo tende zilizojaa kiganja chake kutoka kwenye kikapu kilichokuwa pembeni yake. Mtu wa pili na wa tatu walifika kwa Imam (as) na kutoa ombi kama hilo lililotolewa na mwombaji wa kwanza naye Imam (as) akawapa kiwango kilekile kama alichompa mtu wa kwanza. Lakini wa nne alipofika kwake na kutoa ombi kama hilo la waliomtangulia alikataa kumpa tende hizo na kumwambia: 'Mwenyezi Mugu ataturuzuku sisi na nyingi.' Kisha Imam (as) akasema: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) hakuwa akiombwa kitu na mtu humu duniani ila alimpa.

Siku moja mwanamke mmoja alimtuma mwanaye wa kiume kwa Mtume (saw) na kumwambia: Enda kwake (saw) umwombe na iwapo atakwambia hana kitu, basi mwambie akupe nguo yake. Mtoto yule alienda kwa Mtume (saw) na alipoambiwa kuwa hakuwa na chochote, alimwomba Mtume (saw) ampe nguo yake, naye akafanya hivyo. MwenyezI Mungu alimkemea kwa makusudi kwa kumwambia: Wala usiufanye mkono wako kama uliofungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki mwenye kulaumiwa mwenye kuishiwa.

**********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.