Apr 22, 2019 07:49 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Apr 22

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa…

Mieleka; Iran yaibuka ya 3 Uturuki, yazoa medali lukuki

Timu ya taifa ya mieleka ya kujiachia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka mshindi wa tatu katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo nchini Uturuki. Wanamieleka hao wa Iran wamezoa medali kochokocho zikiwemo tatu za dhahabu. Wanamichezo hao wa Kiirani waliozoa medali za dhahabu ni Mohammad Sadeq Firouzpour (70kg), Alireza Abdollahi (92kg) na Amir Hossein Zare (125kg). Aidha Wairani wengine wanne wameshinda medali za fedha katika vitengo mbalimbali.

Mwanamieleka chipukizi wa Kiirani akipambana na adui

Wanamieleka hao ni Erfab Jafarian (57kg), Ali Ashkivar (65kg), Abdollah Sheikh Azami (79kg) na Sajjad Habibi (86kg). Mwenyeji Uturuki imeibuka kidedea kwa kuzoa alama 200, ikifuatiwa na Azerbaijan iliyotia kimbindoni pointi 148. Mashindano hayo ya dunia ya mieleka yanayofahamika kwa Kiingereza kama Turkey International Tournament yalianza Aprili 18 na kufunga pazia lake Jumapili ya Aprili 21.

Bingwa wa Sataranji wa Iran akataa kucheza na Mzayuni

Bingwa wa mchezo wa sataranji (chesi) wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Sataranji ya Grenke Classic Chess huko nchini Ujerumani amekataa kucheza na mshindani wake kutoka utawala haramu wa Israel. Ali-Reza Firouzja mwanasataranji mashuhuri Muirani alikataa kumtambua mwakilishi wa utawala haramu wa Israel katika mashindano hayo kuonesha uungaji mkono wake kwa taifa la Palestina. Mchezaji huyo nyota wa chesi wa Iran alikataa kucheza na Mzayuni huyo Ijumaa jioni licha ya kuwabwaga washindani wake wote na kuwa na nafasi kubwa ya kuibuka mshindi. Amesema, "Hii ni ishara ya uungaji mkono kwa wapalestina, sambamba na kuitaka Israel iondoke mara moja katika ardhi za Wapalestina inazozikalia kwa mabavu." Wanasataranji nyota zaidi ya 900 kutoka nchi 48 duniani wanashiriki mashindano hayo ya kimataifa nchini Ujerumani.

Ali-Reza Firouzja mwanasataranji mashuhuri Muirani

Kijana huyo Muirani mwenye umri wa miaka 15, mwezi uliopita pia alikataa na kuchezaji na mshindani wake kutoka Israel, katika mashindano ya Kombe la Rilton nchini Sweden, kitendo ambacho kilipongezwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, alipokutana naye hapa Tehran. Firouzja ambaye ni mshindi wa mashindano ya chesi ya Iceland Chess 960, amefuzu kushiriki mashindano ya Chess 960 nchini Norway mwaka huu. Wachezaji wa michezo mbalimbali wa Iran wamekuwa wakikataa kucheza na mahasimu wao wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ili kuonesha uungaji mkono wao kwa Wapalestina madhulumu ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Serengeti ya Tanzania yadhalilishwa

Timu ya soka ya vijana wenye umri wa miaka chini ya 17 ya Tanzania (Serengeti Boys) imeaga kwa idhilali kubwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana Afcon U-17, baada ya kupoteza mechi zake zote. Siku ya Jumamosi timu hiyo mwenyeji ilijikuta ikikubali kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa Angola, katika mchuano wake wa mwisho wa hatua ya Makundi. Mchezo huo kwa Tanzania ulikuwa kama wa kukamilisha ratiba, na uliwafanya vijana wa Serengeti wajikute wamefungwa jumla ya magoli 12 na kufunga 6 katika mechi zao za makundi.  Kipigo hicho cha 4-2 kutoka kwa Angola ndicho kimewakwaza zaidi Watanzania kupoteza mechi zote licha ya kuwa mwenyeji. Mashabiki wa Serengeti Boys hapa wanaeleza hisia zao baada ya timu yao kuondolewa kichwa chini mikono nyuma.

Serengeti Boys

Siku ya Jumatano Serengeti Boys ilishushiwa kichapo cha mabao 3 bila jibu na kujikuta ikipoteza mechi yake ya pili dhidi
ya Uganda. Awali, Serengeti Boys walipoteza mchuano wa ufunguzi waliposhuka dimbani kuvaana na Nigeria na kulazwa mabao 5-4. Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo ambaye anakabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu alikuwa na haya ya kusema baada ya vijana wake kuaga mashindano hayo ya kikanda.

Angola na Nigeria zimetinga nusu fainali ya michuano hiyo ya Afrika. Ndoto ya Uganda kutinga Kombe la Dunia nchini Brazil pia zilikatizwa baada ya kuambulia sare ya bao 1-1 katika mchuano wake na mwisho wa makundi ilipotoana jasho na Nigeria. Cameroon tayari imefuzu katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ya bara Afrika kwa vijana wasiozidi miaka 17 inayoendelea nchini Tanzania. Indomitable Lions walifika katika hatua hiyo baada ya kushinda mechi yake ya pili katika michuano ya Kundi B kwa kuifunga Morocco mabao 2-1 siku ya Alhamisi katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Chamazi.

Guinea nayo ilipata ushindi wake wa kwanza, baada ya kuisasambua Senegal mabao 2-1 na ni ya pili katika kundi hilo kwa alama tatu. Mataifa manne yatakayofika katika hatua ya nusu fainali, yatafuzu katika michuano ya Kombe la Dunia baadaye mwaka huu nchini Brazil.

Dondoo za Hapa na Pale

Barcelona ilifanikiwa kuichapa Manchester United magoli 3-0 katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ya kombe la Klabu Bingwa Ulaya. Barcelona ambayo mchezo wa kwanza ilishinda kwa goli 1-0, imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo kwa ushindi huo mtawalia. Lionell Messi aliandika goli la kwanza dakika ya 16, na dakika 4 baadae akaongeza jingne kutokana na makosa ya mlinda mlango wa Man U, De Gea. Goli la 3 la Berca katika mchezo huo lilipatikana katika kipindi cha pili kunako dakika ya 61 kupitia kwa Philippe Coutinho.

Masaibu ya Mashetani Wekundu hayakuishia hapo, Jumapili walipewa kichapo cha mbwa cha mabao 4-0 na Everton katika mchuano wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, na huenda mechi hiyo imezima matumaini ya Man U ya kumaliza katika nafasi ya nne bora ya EPL, baada ya kichapo hicho.

Gunners wakishangili bao

Aidha Arsenal wamejikuta wanaandamwa na zimwi linalowakodolea macho Man U, baada ya kutandikwa mabao 3-2 Crystal Palace siku ya Jumapili licha ya kuupigia nyumbani Emirates.

Man City ambao Jumamosi waliizaba Tottenham bao 1-0 wanasalia kileleni mwa jedwali la Ligi ya Premia, wakiwa ana alama 86, alama moja mbele ya Liverpool ambayo ilivuna alama tatu wikendi pia kwa kuiadhibu Cardiff City 2-0. Mabao ya Liverpool katika kipute hicho yalifungwa na Georginio Wijnaldum and James Milner. Kwa sasa orodha ya tatu bora inafungwa na Tottenham yenye alama 67, alama moja tu mbele ya Gunners wanaorodhika na nafasi ya nne kwa sasa.

Na kwa kutamatisha, Shirikisho la Wachezaji wa Soka la Kulipwa nchini Uingereza (PFA) limetangaza majina ya wachezaji wanaowania Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka nchini humo. Taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo imetaja wachezaji hao kuwa ni Sergio Aguero, Raheem Sterling na Bernardo Silva kutoka Manchester City, Virgil van Dijk na Sadio Mane kutokea Liverpool na mwingine ni Eden Hazard kutokea Chelsea.

Salah mwaka huu hawanii tuzo ya PFA

Mchezaji bora wa msimu uliopita Muhammed Salah raia wa Misri anayechezea Liverpool msimu huu sio miongoni mwa wanaowania tuzo hiyo. Mchezaji atakayeshinda atatunukiwa tuzo hiyo katika hafla itayofanyika jijini London mnamo April 28.

……………………….TAMATI………….………..