Alkhamisi, Mei Pili, 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Sha'aban 1440 Hijria, mwafaka na tarehe Pili Mei, 2019.
Siku kama ya leo miaka 1335 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa wakati huo. Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz hapo mwaka 101 Hijiria. Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa ni mtu wa karibu na ukoo wa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu mkubwa watu wa ukoo huo.

Siku kama ya leo miaka 685 iliyopita, alifariki dunia Ibn Faswih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria. Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifundisha pia elimu ya hadithi na kufikia ujuzi wa hali ya juu katika uwanja huo. Aidha msomi huyo mbali na elimu za dini, alisoma pia mashairi huku akiandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti ikiwemo fiqhi.

Siku kama ya leo miaka 500 iliyopita, alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia Leonardo da Vinci. Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Miongoni mwa michoro maarufu ya Leonardo Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa".

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 12 Ordibehesht 1358 Hijria Shamsia, mwanachuoni na mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Murtadha Mutahhari, aliuawa shahidi na kundi lililo dhidi ya Mapinduzi la Furqan hapa nchini. Tukio hilo lilitokea katika kipindi cha chini ya miezi mitatu tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa Iran. Shahidi Mutahhari alijistawisha kielimu kutoka kwa maulamaa wakubwa wakiwemo Ayatullahil Udhma Burujerdi, Allamah Tabatabai na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wakati wa kukaribia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Mutahhari alikuwa mmoja kati ya shakhsia muhimu wa kidini, kielimu na kisiasa katika harakati ya Kiislamu. Imam Khomeini, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimteua Shahid Mutahhari kuwa mwanachama na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Kiislamu. Ayatullah Murtadha Mutahhari ameandika karibu vitabu 80 katika nyanja mbalimbali. Kutokana na daraja la juu la Shahidi Ustadh Murtadha Mutahhari katika kueneza mafundisho ya Kiislamu katika vyuo vya kidini (Hawzah) na vyuo vikuu, siku ambayo aliuawa shahidi inajulikana nchini Iran kama 'Siku ya Mwalimu'.

Na siku kama ya leo miaka 19 iliyopita sawa na 26 Shaaban mwaka 1421 Hijria Qamaria, faqihi na mwanazuoni mkubwa Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani aliaga dunia. Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani alizaliwa mwaka 1343 Hijria Qamaria sawa na 1303 Hijria Shamsia katika mji mtakatifu wa Qum. Katika ujana wake alijifunza dini na alipofika umri wa miaka 20 alielekea katika mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baadaye wakati Ayatullah Boroujerdi alipowasili Qum, Ayatullah Rouhani alishiriki katika darsa zake za fiqhi ya "Kharij" (darsa ya daraja la juu kabisa la fiqhi) na kisha yeye mwenyewe akaanza kufunza darsa hizo. Ayatullah Rouhani alikuwa mwanazuoni wa kwanza katika Chuo Cha Kidini cha Qum (Hawzah) ambaye alianzisha vikao vya kitaalamu kwa lengo la kuchunguza itikadi ya Umaxi. Baada ya kuanza harakati ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA, alijiunga na harakati hiyo kubwa na kunufaika na fursa iliyokuwa imejitokeza ya kueneza itikadi za Uislamu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa mikoa ya Markazi na Qum katika Baraza la Wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Mwanazuoni huyo bingwa hatimaye, baada ya kuugua aliaga dunia tarehe 26 Shaaban mwaka 1421 Hijria Qamaria sawa na 3 Azar mwaka 1379 Hijria Shamsia akiwa na umri wa miaka 76 na alizikwa katika Haram Takatifu ya Bibi Maasouma mjini Qum.
