Jun 04, 2019 02:16 UTC
  • Jumanne, Juni 4, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 29 Ramadhani 1440 Hijria inayosadifiana na Juni 4 mwaka 2019 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Baada ya kutangazwa habari ya kufariki kwake dunia, ilimwengu wa Kiislamu uligubikwa na wingu la simanzi na huzuni. Imam Khomeini alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1902 huko katika mji wa Khomein katikati mwa Iran. Alianza harakati zake za kisiasa sambamba na shughuli zake za kielimu na kiutamaduni. Kutokana na shughuli zake za kisiasa zilizokuwa zikiukera sana utawala wa kidhalimu wa mfalme Shah, utawala huo ulimbaidisha Imam katika nchi za Uturuki na Iraq. Katika kipindi cha miaka 13 akiwa uhamishoni huko Iraq, Imam (MA) alilea na kuwafunza wanafunzi wengi na wakati huohuo kufichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah kwa ushirikiano wa karibu na Marekani. Baada ya kupamba moto mapambano na harakati za Kiislamu zilizokuwa zikiongozwa na Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah, hatimaye Imam alilazimika kutoka nchini Iraq na kuhamia Ufaransa, hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi hapa nchini hapo mwaka 1979. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, Baraza linalomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mfumo wa Kiislamu wa Iran lilimchagua Sayyid Ali Khamenei kuuongoza mfumo huu. Muda mfupi baada ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA), baraza hilo lilikutana kwa lengo la kumchagua kiongozi wa baada yake. Wanachama wa baraza hilo ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi, walichunguza uzeofu wa kimapinduzi na sifa nyingine muhimu za Ayatullah Khamenei zikiwemo za ushujaa, uwezo mkubwa wa kuchambua mambo ya zama, ujuzi mkubwa wa masuala ya kidini, fikhi na sheria ya Kiislamu, uadilifu, utawala bora na kumchagua kwa wingi wa kura kuwa Kiongozi Mkuu wa Mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, sawa na tarehe 4 Juni mwaka 1989, wanafunzi kadhaa wa vyuo vikuu vya China waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa na polisi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Beijing. Siku hiyo maelefu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya China walikuwa wamekusanyika katika Medani ya Tiananmen mjini Beijing, wakitaka kuwepo mazingira ya wazi ya kisiasa nchini humo, kupunguzwa uwezo wa Chama cha Kisoshalisti, kuongezwa uwezo wa Bunge na kuchaguliwa wawakilishi wake. Ingawa serikali ya China ilipiga marufuku maandamano hayo lakini wanafunzi waliendelea kukusanyika na mwishowe askari polisi na vikosi vya jeshi vikatumia silaha kuwakandamiza wanafunzi hao.

Medani ya Tiananmen mjini Beijing

Siku kama ya leo miaka 792 iliyopita alizaliwa mwanazuoni mahiri wa Kiislamu katika mji wa Hillah Iraq, Ayatullah Jamaluddin Hassan bin Yusuf mwenye lakabu ya Allamah Hilli. Awali alisoma kwa baba yake na mjomba wake na akiwa katika rika la ujana alikuwa tayari amefanikiwa kufikia daraja za juu za elimu katika taaluma kama fikihi, usul Fikih, hadithi na kadhalika. Mwanazuoni huyo alikuwa hodari pia katika uga wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vya Allamah Hilli ni Tadhkiratul al-Fuqahaaa, Irshadul Adh'han, na Kashful Murad. Alimu huyo aliaga dunia mwaka 726 Hijria.

Allamah Hilli

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression). Siku hiyo ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel. Ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto una sura na aina mbalimbali na unasababishwa na uzembe wa wazazi, viongozi wa kitaifa na kimataifa na makatili wasio na chembe ya huruma wanaojali maslahi yao ya kimaada.

 

Tags