Ijumaa tarehe Pili Agosti mwaka 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 30 Mfunguo Pili Dhulqaada 1440 Hijria sawa na tarehe Pili Agosti mwaka 2019.
Katika siku ya mwisho ya mwezi Dhulqaada mwaka 220 Hijria Imam Muhammad Taqi AS mmoja kati ya wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Mtukufu huyo alipewa jina la 'Jawad' likiwa na maana ya mtu mkarimu sana kutokana na ukarimu wake mkubwa. Imam Jawad alizaliwa katika mwezi wa Ramadhani mwaka 195 Hijria na kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ridha (as). Kipindi cha maisha ya Imam Jawad kilikuwa kipindi cha kuchanua utamaduni wa Kiislamu na kuenea kwa fikra, itikadi na falsafa na kujitokeza mifumo ya fikra za Wagiriki na Warumi katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam alifanya juhudi kubwa kulea kizazi chenye maarifa na kueneza elimu na mafundisho sahihi ya Uislamu kama njia ya kukabiliana na fikra za kigeni sambamba na kufichua siri na maovu ya watawala wa Bani Abbas. Suala hilo liliwakasirisha mno watawala hao ambao hatimaye waliamua kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (SAW) katika siku kama hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Mordad 1288 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi mjini Tehran Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri mwanachuoni mkubwa ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Qaajar hapa nchini Iran. Ayatullah Fadhlullah Nouri alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mapinduzi ya katiba na alisimama kidete kupinga sheria zilizopitishwa bungeni ambazo zilikuwa zikikinzana na miongozo na mafundisho ya Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Agosti 1934, alifariki dunia Fidel Hindenburg Rais wa zamani wa Ujerumani na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya majeshi ya nchi hiyo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Hindenburg alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Ujerumani mwaka 1925.

Tarehe Pili Agosti miaka 74 iliyopita, kongamano la Potsdam lilikamilisha kazi zake. Kongamano hilo la tatu na la mwisho la viongozi waitifaki walioshiriki katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, lilianza tarehe 17 mwezi Julai na kumalizika tarehe Pili Agosti 1945. Kongamano hilo lililofanyika katika mji wa Potsdam karibu na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin lilihudhuriwa na Joseph Stalin, Harry S. Truman na Winston Churchill, marais wa wakati huo wa Urusi ya zamani, Marekani na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala wa zamani wa Iraq ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutoa azimio lolote dhidi ya utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq ambao ulikuwa ukiungwa mkono na nchi za Magharibi, kwa kutumia silaha za kemikali. Masaa kadhaa baada ya kutolewa ripoti hizo, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia tena mji wa Ushnawiye kwa mabomu ya kemikali na kujeruhi watu 2400.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, jeshi la Iraq liliishambulia na kuikalia nchi jirani ya Kuwait. Huo ulikuwa uvamizi wa pili wa Iraq kwa jirani zake baada ya ule wa Iran wa mwaka 1980. Utawala wa Saddam ulikuwa ukidai kwamba, ardhi ya Kuwait ni sehemu ya ardhi yake. Mashambulio ya Iraq dhidi ya Kuwait yalikabiliwa na radiamali kali ulimwenguni. Nchi nyingi duniani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani uvamizi huo na kuvitaka vikosi vya Iraq kuondoka mara moja katika ardhi ya nchi hiyo. Nchi kadhaa zikiongozwa na Marekani zilituma vikosi vyao vya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi ili kuviondoa vikosi vamizi vya Iraq kutoka katika ardhi ya Kuwait na kuhitimisha uvamizi huo Februari 28 mwaka 1991.
