Nov 18, 2019 08:07 UTC
  • Sayansi na Teknolojia 101

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utaweza kunufaikan na niliyokuandalia.

Awamu ya Tatu ya Zawadi ya Mustafa SAW 2019 ilitangazwa Novemba 11 katika mji mkuu wa Iran, Tehran, ambapo wanasayansi watatu wa Iran na wawili kutoka Uturuki walitangazwa washindi.

Kwa mujibu taarifa wanasayansi waliopata tuzo ya Mustafa SAW 2019 ni pamoja na Ali Khadem Hosseini wa Iran na Ugur Sahin wa Uturuki katika kategoria ya 'Maisha, Sayansi ya Tiba na Teknolojia.'  Nao Umran S. Inan wa Uturuki, Mohammad Abdol-Ahad na Hossein Baharvand wa Iran wamepata tuzo ya Mustafa SAW 2019 katika kategoria jumla ya Sayansi na Teknolojia.  Profesa Ugur Sahin ambaye anafunza katika Chuo Kikuu cha Mainz Ujerumani amepata tuzo kutokana na kazi zake katika kuvumbua na kufanyia majaribio chanjo ya saratani. Naye Profesa Ali Khademhosseini ambaye anafunza katika Chuo Kikuu cha UCLA nchini Marekani ametunukiwa tuzo kutokana na utafiti wake katika uga wa teknolojia ya nano. 

Kwa upande wake Profesa Umran S. Inan ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Koc Uturuki ametunukiwa tuzo kufuatia utafiti wake wa kina kuhusu anga za mbali huku Profesa Hussein Baharvand wa Taasisi ya Royan akipata tuzo baada ya mafanikio yake ya kutibu ugonjwa wa Parkinson na ugonjwa wa jicho unaojulikana kama AMD kwa kutegemea seli shina. Kwa upande wake Dakta Mohammad Abdol-Ahad wa Chuo Kikuu cha Tehran ametunukiwa tuzo kutokana na utafiti wake kuhusu mbinu mpya za kutibu saratani.

Sherehe za kuwatunuku zawadi wanasayansi hao bingwa wa Kiislamu zimehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Iran Anayeshughulikia Masuala ya Sayansi na Teknolojia Dtk. Sorena Sattari.

Katika kuwania tuzo ya mwaka huu, zaidi ya kazi 150 ziliwasilishwa na kufanyiwa uchunguzi na jopo la majaji 500 kutoka vyuo vikuu 200 katika nchi 35 na hatimaye washindi wakatangazwa.

Zawadi ya Mustafa SAW ni zawadi ya juu zaidi ya sayansi na teknolojia ambayo hutunukiwa wanasayansi na watafiti na watafiti bora Waislamu duniani. Washindi wa Zawadi ya Mustafa SAW hupata zawadi ya nusu milioni dola pamoja na cheti.

Sherehe za kuwatangaza washindi wa Zawadi ya Mustafa SAW hufanyika katika Wiki ya Umoja wa Kiislamu nchini Iran kama sehemu ya kuadhimisha Maulid ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

@@@

Timu ya Iran ambayo imevumbua 'glovu erevu ya kielektroniki yenye joto' imefanikiwa kushika nafasi ya pili katika mashindano ya kimataifa ya uvumbuzi na ubunifu nchini Croatia.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la ISNA, watafiti Wairani wamefanya uchunguzi kuhusu matatizo ya wapanda milima na watu wanaofanya kazi katika maeneo yenye milima au baridi kali, na hatimaye wamefanikiwa kuunda glovu ambazo zina uwezo wa kufanya kazi kama simu ya mkononi.

Glovu hii erevu au automatiki ina uwezo wa kuchunguza alama muhimu katika uhai wa mwanadamu kama vile mapigo ya moyo, kiwango cha joto na shinikizo la damu. Aidha glovu hii ina uwezo wa kuunganishwa na mfumo wa mwasiliano wa GPS na hivyo iwapo mpanda milima atakumbwa na tatizo ana uwezo wa kutuma ujumbe kupitia mfumo huo.

Glovu hii iliyoundwa na wanasayansi wa Iran inamuwezesha mtumizi kustahamili baridi kali ya nyuzi joto chini ya 40. Wanasyanasi Wairani wametumia teknolojia ya nano kuunda kitambaa  kilichotumika kutengeneza glovu hiyo. Mashindano ya kimataifa ya uvumbuzi na ubunifu hufanyika Croatia kila mwaka katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Croatia katika mji wa Zagreb.

@@@2

Kwa mara ya kwanza ndege zisizo na rubani za droni zimetumiwa kwa majaribio ili kupambana na ugonjwa hatari wa malaria katika visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania kwa kunyunyizia dawa maalumu mashamba ya mpunga katika eneo la Cheju kusini mwa kisiwa cha Unguja.

Hatua hiyo kubwa katika kampeni ya kupambana na malaria imefikiwa mwezi huu wa Novemba na timu ya watafiti kutoka chuo kikuu cha Radboud cha nchini Uholanzi wakiongozwa na Bart Knols.

Kupitia mkakati wa kuangamiza mazalio ya mbu aina ya anopheles anayesababisha homa ya malaria, Knols amesema, wanatazamia kuudhibiti ugonjwa huo ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa unaua mtoto mmoja katika kila dakika moja na kuongoza kwa asilimia 75 ya vifo vyote vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Droni hizo zilizotengezwa na kampuni ya DJI ya China zitatumika kwa ajili ya kunyunyiza dawa maalumu ya kuangamiza mayai ya mbu wa malaria katika vidimbwi vinavyotuama maji kwenye mashamba ya mpunga, ambavyo hutumiwa na mbu wa ugonjwa huo kutagia mayai yao hayo. 

Unyunyiziaji dawa kwa kutumia droni unatumiwa kama majaribio ili kuona kama utaweza pia kuisaidia Zanzibar kufikia lengo lake la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2023, kulingana na mpango wa mkakati ulioandaliwa na Programu ya Kutokomeza Malaria Zanzibar.

Kwa mujibu wa Bart Knols aina hiyo ya unyunyiziaji dawa ni mfumo usio na gharama kubwa ya kuzuia kuzaliana kwa mbu wa malaria, ikizingatiwa kuwa upigaji dawa kwa kutumia mkono unachukua muda mwingi na unyunyiziaji wa kutumia helikopta una gharama kubwa. Meneja wa Programu ya Kutokomeza Malaria Zanzibar Abdullah Suleiman Ali amesema, lengo lao kuu katika kampeni ya kupambana na malaria ni kuhakikisha ugonjwa huo hatari unatokomezwa kikamilifu visiwani humo ifikapo mwaka 2023.

@@@

Sudan imezindua kwa kurusha angani satalaiti yake ya kwanza itakayoshughulika na utafiti wa kijeshi, kiuchumi na wa tekonolojia ya anga za mbali. Akizungumza katika kikao na maafisa waandamizi wa usalama, mkuu wa Baraza Kuu la Utawala la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametangaza kuwa, satalaiti hiyo imetengenezwa kwa ushirikiano na Jamhuri ya Watu wa China. Taarifa iliyotolewa na baraza hilo imesema, satalaiti hiyo imeundwa kwa lengo la kuendeleza utafiti katika teknolojia ya anga za mbali, kukusanya taarifa na vile vile kugundua maliasili kwa ajili ya mahitaji ya kijeshi ya nchi. Shirika rasmi la habari la China Xinhua limeripoti kuwa, Satalaiti ya Sudan ya Kukusanya Taarifa kutokea mbali inayoitwa SRSS-1 ilirushwa kuelekea angani Novemba 6 katika mkoa wa Shanxi, kaskazini mwa China.

Msemaji wa baraza la utawala la Sudan Mohamed al-Faki Suleiman amesema, baada ya muda wa miezi michache, satalaiti hiyo itakuwa inaongozwa kutokea Sudan. Ameongeza kuwa China imerusha satalaiti hiyo kama mshirika katika mradi wa uundaji wake. Sudan, ambayo inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi imekuwa ikiendesha mradi wa kitaifa wa teknolojia ya anga za mbali kwa muda wa miongo kadhaa sasa.

Mnamo mwaka 2013, serikali ya Sudan ya wakati huo iliyokuwa ikiongozwa na Omar al-Bashir ilianzisha Taasisi ya Utafiti wa Anga za Juu na Anga za Mbali (ISRA), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza teknolojia za anga za mbali.

@@@

Naam na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya Sayansi na Teknolojia.

 

Tags