Nov 25, 2019 05:35 UTC
  • Jumapili, tarehe 24 Novemba, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 26 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria, mwafaka na tarehe 24 Novemba 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1097 iliyopita yaani tarehe 26 Rabiul Awwal mwaka 344 Hijiria alifariki dunia Ibn Sammak, mtaalamu mkubwa wa masuala ya itikadi ya Kiislamu huko Baghdad. Historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo, lakini ripoti zinasema kwamba aliishi mjini Baghdadi, Iraq na kupata elimu na maarifa kwa wasomi wa mji huo. Vilevile historia inasema Ibn Sammak alilea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Haakim Nishaburi. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Sammak ni kile cha "al Aamali" na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila na matukufu ya Ahlulbait wa Mtume Muhammad (saw).

Ibn Sammak

Siku kama ya leo miaka 387 iliyopita, alizaliwa Baruch de Spinoza mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu jamii wa Uholanzi. Spinoza alisoma kwa bidii na kukwea daraja za kielimu. Hata hivyo ukosoaji wake wa dini ya Kiyahudi ulimfanya akabiliwe na chuki na uhasama wa maulama wa dini hiyo. Njia na fikra za kifalsafa za Spinoza zilikaribiana na itikadi za kisufi. Msomi huyo wa elimu ya falsafa wa Uholanzi ameandika pia vitabu kadhaa kama The Philosophy of Spinoza na The Road to Inner Freedom. Baruch de Spinoza alifariki dunia mwaka 1677.

Baruch de Spinoza

Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kwa jina la ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara. Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.

Michael Faraday

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa wa Ufaransa, Henri Toulouse Lautrec. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Lautrec alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901.

Henri Toulouse Lautrec

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita yaani sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa hapa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazeti hilo alikuwa Adib al-Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri ya Taifa la Iran yaani Bunge la Iran.

Gazeti la 'Majlis'

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu. Abul-Makaarim Zanjani alizaliwa mwaka 1255 Hijiria mjini Zanjani, kaskazini magharibi mwa Iran ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo ya hawza mjini hapo. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alipata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Morteza Ansari. Aidha baada ya kufariki dunia baba yake, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alichukua jukumu la umarjaa wa masuala ya kidini na sheria za Kiislamu hususan mjini Zanjani. Katika kipindi cha mapinduzi ya kikatiba, msomi huyo na kama walivyokuwa wasomi wengine, alisimama kupambana na udikteta wa wakati huo hapa nchini Iran. Vitabu vya 'Makhaarijur-Rahman' na 'Miftaahud-Dhafar' ni miongoni mwa athari za Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani.

Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani

Na siku kama ya leo miaka sita iliyopita, yaani tarehe 24 Novemba 2013, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitiliana saini makubaliano ya muda na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani katika uwanja wa miradi ya amani ya nyuklia ya Iran. Makubaliano hayo yalitiwa saini huko Geneva Uswisi. Kutiwa saini makubaliano hayo kulifungua njia ya mazungumzo baina ya Iran na nchi za kundi la 5+1 yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, China, Russia pamoja na Ujerumani kwa ajili ya kutiwa saini makubaliano jumla ya kuondoa suutahafamu zote kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran na kuondolewa vikwazo vyote vya kidhalimu vya kimataifa na vya pande kadhaa. Hatimaye  makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yalitiwa saini Julai 2015 baina ya Iran na kundi la 5+1.

Tags